0
Mahakama ni chombo, cha Serikali, chenye mamlaka ya kutoa maamuzi katika migogoro baina ya pande mbili na pia kusimamia utawala wa sheria na kuamua kuhusu mashauri ya jinai na ya madai, kufuatana na sheria za nchi.
Katika nchi nyingi zenye tawala za kidemokrasia Mahakama (Judiciary), ni moja ya mihimili mitatu ya Dola. Mingine ni Utawala (Executive) na Bunge (Parliament). Kimuundo na kimatarajio, mihimili hii hutoa uangalizi na vizuizi (checks and balances) miongoni mwao, kwamba hakuna muhimili mmoja utapitiliza majukumu yake bila ya kutazamwa na kuzuiwa na mwingine.

Na ndiyo maana Katiba inasema wazi kwamba Bunge hutunga sheria, lakini hazitatumika hadi zisainiwe na Rais (Muhimili wa Dola), halafu hapo hapo Mahakama ina uwezo wa kufuta sheria yoyote iliyotungwa na Bunge (na kusainiwa na Rais) iwapo itaiona sheria hiyo inakwenda kinyume na Katiba ya nchi.

Isitoshe ingawa Rais humteua Jaji Mkuu, (msimamizi mkuu wa Muhimili wa Mahakama) na kumuapisha, lakini yeye Rais hawezi kushika madaraka ya nchi sharti kwanza aapishwe na Jaji Mkuu.

Mahakama kama itaendeshwa vyema bila kuingiliwa na Mhimili mwingine, lazima ihakikishiwe uhuru wa kutenda kazi yake (independence of the judiciary), kwani ni chombo kinachoweza kusukuma kuwepo kwa utawala wa sheria kama kitaweza kusisitiza haki na uzingatiaji wa sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa katika Katiba na sheria nyingine, na hivyo kudumisha utulivu na amani ya nchi.

Lakini mara nyingi Mhimili unaotuhumiwa kwa kupitiliza majukumu yake kikatiba na kisheria, ni ule wa Dola –kwa maana ya Serikali na taasisi zake zikiwemo zile zinazosimamia usalama wa raia – kama vile polisi.

Katika nchi nyingi Muhimili wa Dola huwa una kawaida ya kuidhibiti Mihimili mingine, hasa huu wa Mahakama – kwamba usitende haki inavyotakiwa kwa hofu ya Muhimili huo kuumbuka au kuathirika kwa namna moja au nyingine.

Jitihada za Muhimili wa Dola kuingilia uhuru wa Mahakama, hutokea katika nchi nyingi tu ingawa katika viwango tofauti. Hata serikali zenye demokrasia iliyopevuka kama vile nchi za Magharibi hufanya hivyo hivyo. Na hufanya hivyo kwa njia nyingi ikiwemo ile ya kuibania fedha za bajeti yake. Njia nyingine ni za kihuni, kibabe au ghilba tu.

Katika miaka ya 90 majaji wa Mahakama Kuu ya Malta, walisimamishwa kazi saa moja tu kabla ya kuanza kusikilizwa kesi muhimu iliyofunguliwa dhidi ya serikali. Na huko Pakistan, serikali mbali mbali zilizokuwa madarakani, zilikuwa zinateua majaji wa muda tu kukaimu nafasi hizo – kwani hali hii ya majaji hao kutokuwa na muda maalum (tenure) wa kufanya kazi, kuliwaweka katika hali ya kuyumbishwa kisiasa katika maamuzi yao.

Hali hiyo pia ilielezwa kuwepo nchini Gambia wakati wa utawala wa Yahya Jamme – alikuwa anateua majaji wa muda – wengine kutoka nchi za nje—kwa lengo la kuwayumbisha, ili wawe wanatoa maamuzi chanya kwa utawala wake. Hapa Tanzania Jaji Mkuu wa sasa naye anakaimu tu nafasi hiyo.

Hata hivyo wanasheria wanasema mamlaka iliyomteua, Rais John Magufuli, haikukiuka Katiba au sheria yoyote kufanya hivyo, ila tu wanasema hali ya kukaimu nafasi hiyo kutamfanya Jaji Mkuu huyo, asiweze kuwa huru zaidi katika kutekeleza majukumu yake.

Na nchini Uganda mwaka 2013, majaji na wanasheria walifanya mgomo kupinga uvamizi wa eneo la Mahakama Kuu uliofanya na makachero wa serikali kuwakamata watuhumiwa sita wa kesi ya uhaini ambao walikuwa wamepata dhamana. Na huko huko Uganda miaka miwili kabla hukumu, uendeshaji kesi dhidi ya kiongozi wa upinzani Kizza Besigye katika Mahakama Kuu ulisimama kwa muda baada ya vikosi vya majeshi kulizingira eneo hilo.

Hapa kwetu pia mambo yanayokaribiana sana na hayo, yamekuwa yakitokea. Katika  miaka ya 90 kelele kubwa katika tasnia ya sheria ziliibuka baada ya mwendesha Mashitaka Mkuu (DPP) alipoifuta kesi ya mauaji iliyokuwa ikimkabili mtoto wa kigogo mmoja wa Serikali.

Kilichowakasirisha wengi, ilikuwa ni kasi kubwa iliyokuwepo katika kuendesha kesi hiyo, na hasa ilipofahamika kulikuwapo ulazima wa DPP huyo kwenda ofisini siku ya Jumapili kulishughulikia jalada la kesi, ili siku ya pili yake Jumatatu tayari liwe mezani mahakamani likiwa na maelezo ya kuifuta kesi hiyo.

Hata hivyo matukio ya upande wa Jamhuri kupitia DPP, kufuta kesi dhidi ya watuhumiwa, bado yanaendelea kwa kutumia kifungu husika cha sheria. Hii inatokana na kwamba katika mfumo wetu (tulioiga kutoka mfumo wa Uingereza) wa uendeshaji kesi, mwendesha mashitaka (prosecutor) mkuu katika kesi za jinai ni Serikali – tofauti na nchi nyingine za Ulaya.

Aidha, inadaiwa ule mgogoro baina ya DPP na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU unadaiwa ndiyo ulisababisha watuhumiwa wakuu wa ufisadi, ambao ni vigogo wa Serikali kutoshitakiwa mahakamani –hasa wale vigogo waliotajwa katika kashfa za EPA, Deep Green, Meremeta na hata Tegeta Escrow.

Lakini hakuna suala lililoitikisa fani ya sheria na utoaji haki kama ule wa miaka 10 iliyopita – wa mlolongo wa matukio yaliyojiri baada ya kufunguliwa mashitaka ya mauaji kwa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Ukiwaona Ditople Mzuzuri.

Kesi ya mshitakiwa huyo ilisababisha mahabusu katika magereza ya Dar es Salaam na kwingineko, kugoma kuingia kwenye magari kwenda mahakamani kwa ajili ya kusikilizwa kesi zao. Mgomo huo wa siku tano haukuwahi kutokea nchini.

Upelelezi wa kesi dhidi ya Ditopile ulichukua miezi minne tu hadi mashitaka kubadilishwa kutoka mauaji ya kukusudia na kuwa mauaji ya kutokusudia, na hivyo kupewa dhamana.

Hilo liliwakasirisha sana mahabusu wengine waliokuwa wakingojea kesi zao (pamoja na zile kesi za mauaji), ambazo baadhi yao walikuwa mahabusu kwa miaka kadha. Walitaka nao wafanyiwe uharaka wa namna hiyo katika kuchunguza kesi zao, la sivyo dhamana ya Ditopile ifutwe.

Lakini katika siku za karibuni Mahakama inaonekana kama vile imeanza kutambua wajibu wake katika jamii kama ni mlinda haki mkuu wa jamii dhidi ya uonevu – kutokana na maamuzi inayotoa kuhusu kesi mbali mbali mbele yake.

Inafanya hivyo si kutokana na sababu nyingine, bali ni kuhimiza uzingatiaji wa sheria, kanuni na utaratibu uliowekwa. Kwa mfano, dhamana ni haki ya mshitakiwa yeyote, isipokuwa katika kesi chache zilizotajwa.

Hivyo kumnyima mshitakiwa dhamana bila ya misingi yoyote, isipokuwa labda ni sababu za kisiasa, ni suala lisilokubalika.

Post a Comment

Emoticon
:) :)) ;(( :-) =)) ;( ;-( :d :-d @-) :p :o :>) (o) [-( :-? (p) :-s (m) 8-) :-t :-b b-( :-# =p~ $-) (b) (f) x-) (k) (h) (c) cheer
Click to see the code!
To insert emoticon you must added at least one space before the code.

 
Top