Iwapo mtu atakubaliana na kauli inayotolewa basi tayari amekwisha amua kwamba huo ndiyo ukweli. Baadhi ya “ukweli” ni ule wa kishabiki tu, au watu wasiolielewa sawasawa jambo husika. Na “ukweli” mwingine ni ule unaofikiwa kwa kulichunguza jambo husika, utumiaji wa hoja mwanana na hata kwa kuweka hadharani mahesabu. Hali kadhalika “ukweli” mwingine unahusiana na hadhi ya mtu na mazingira aliyomo.
Wanafalsafa katika historia nao wamekuwa na maoni mbali mbali kuhusu “ukweli”. Miongoni mwao ni Robert Pirsig, Mmarekani aliyeishi karne ya 19 ambaye alisema: “Siku zote nimekuwa nikishangazwa na kitu hiki “ukweli.” “Ukweli” unagonga mlangoni na wewe unajibu “Nenda zako, mimi natafuta ukweli.” Na hivyo “ukweli” unaondoka. Yaani mtu anaukataa ukweli waziwazi. Inashangaza sana.”
Confucius, mwanafalsafa wa China aliyeishi miaka 600 kabla ya ujio wa Kristo alisema kuna vitu vitatu tu ambavyo havifichiki hapa duniani – jua, mwezi na “ukweli.” Mwanafalsafa huyu ndiye anahusishwa na ule usemi maarufu kwamba ”Siku zote ukweli hujitenga.”
Naye Mark Twain, Mmarekani mtunzi wa vitabu vya riwaya wa karne ya 19, akizungumzia tofauti kati ya ya ukweli na uongo alisema: “Uongo angalau nao unapaswa kuingia akilini basi.”
Na Richard Nixon, rais wa 37 wa Marekani katika miaka ya 1970 wakati awali akijitetea kwa nguvu kuhusu kutohusika kwake katika kashfa ya Watergate iliyomkumba alisema: “Hakuna ukweli unaofichwa ndani ya Ikulu yangu.” Lakini baadaye dunia nzima ilikuja kujua ukweli – kwamba binafsi alihusika na kashfa ile kutoka utosini hadi vidole vya miguu yake.
Arthur Conan Doyle, Mwingereza mtunzi wa vitabu vya kipelelezi ‘aliyemtengeneza’ mpelelezi maarufu wa kufirika mwishoni mwa karne ya 19, Sherlock Holmes alitafsiri ‘ukweli’ kwa kusema: “Baada ya kuondoa vitu vyote visivyowezekana, kinachobakia, hata kama ni hakiaminiki, basi huo ndiyo ukweli wenyewe.”
Hivyo mtu hawezi kuubadili ukweli, bali ukweli ndiyo unaweza kumbadili mtu – hususan watu dhaifu kifikra. Na kwa bahati mbaya huo nao ndiyo ukweli. Lakini katika siasa na kwa wanasiasa – ukweli huu hupishana nao kwa mbali sana.
Nimeweka utangulizi huo kutokana na hali iliyojitokeza ndani ya wiki mbili hivi zilizopita ambapo nchi ilitikiswa na matukio mawili makubwa ambayo kwa kiwango kikubwa yalihusiana. Katika matukio hayo “ukweli” ulipuuzwa, ulikwepwa, uliachwa ukining’nia, uligeuzwa chini juu na kadhalika.
Kwanza ni kuvamiwa kwa kituo cha utangazaji cha Clouds Media na kundi la watu wenye silaha waliovaa kiaskari wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda.
Yadaiwa lengo la uvamizi huo ni kukilazimisha kituo hicho kutangaza kipindi chenye maudhui binafsi ya Mkuu huyo wa Mkoa huyo, agizo ambalo watangazaji walikataa kwani wangekuwa wanakiuka miiko ya kazi yao, kwamba upande wa pili wa kilichomo katika kipindi hicho haujapatikana nao kupewa fursa ya kujieleza.
Tukio la pili, ambalo pia linahusisha silaha, ni lile la kada maarufu wa chama tawala – CCM na aliyekuwa waziri wa Habari, Utangazaji, Michezo na Utamaduni Nape Nauye ambaye masaa machache tu baada ya kuvuliwa uwaziri alijikuta akinyooshewa bastola na mtu anayedaiwa kuwa ni askari ili asizungumze na waandishi wa habari aliokuwa amewaita kuwaeleza ksakata lake la kuvuliwa kwake uwaziri.
Ikumbukwe siku moja kabla, Nape alipokea ripoti ya kamati aliyouinda kuchunguza uvamizi wa studio za Clouds Media ambayo ilithibitisha tukio – kwa tafsiri ya Arthur Conan Doyle hapo juu kuhusu ‘ukweli.’
Kamati iliagiza mamlaka husika zichukue hatua vilivyo. Hivyo kwa tafsiri hiyo hiyo ya Conan Doyle – kuvuliwa kwake uwaziri kunahusiana na alivyolishughulikia sakata la uvamizi wa Clouds Media – kitu ambacho alijua, au alipaswa kujua mamlaka za juu yake hazikupenda afanye.
Matukio yote mawili ni vigumu kuleta hoja kwamba hayakutokea kwa sababu yote yalinaswa na kamera na kusambazwa kwa haraka sana kwenye mitandao ya jamii – shukurani kwa teknolojia ya sasa.
Sehemu ya tukio la uvamizi wa studio za Clouds Media zilichukuliwa na kamera za usalama (CCTV cameras) zilizotegeshewa katika jengo hilo na kusambazwa mitandaoni. Hivyo kwa mamlaka za juu kupinga kutokea kwa tukio hilo ni vigumu na njia iliyobakia ni kujaribu kulipunguza uzito wake (water down) kwa kulipuuzia – yaani kwa kulinyamazia tu ili watu wasahau.
Lakini kwa kuwa tukio hilo limeainishwa kama ni kashfa kwa sababu limemhusisha mkuu wa mkoa, basi ni vigumu kwa vyombo vya habari kulinyamazia – kama jukumu lao la kuuhabarisha umma na kuziambia mamlaka husika zichukue hatua ili tukio kama lile lisirejewe na wengine.
Mara nyingi habari kuu katika vyombo vya habari huwa ni ile inayowahusu wakuu – ndani ya utawala au jamii – chanya au hasi, na hasa hasa hasi.
Na ndivyo ilivyokuwa kwa Nape – kwa nia njema alitaka kuzungumza na wanahabari, hivyo tukio la kuonyeshewa bastola hadharani lilikuwa la ukakasi mkubwa sana.
Lakini badala yake yeye ndiye kibao kikamgeukia, chama chake ghafla kikasahau mchango wake mkubwa alioutoa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa 2015 kukiwezesha kushinda dhidi ya upinzani mkubwa wa kihistoria uliokuwapo.
Inashangaza serikali kwa ujumla yake inashindwa kusikia na kupima hisia za umma katika matukio kama haya na badala yake inaamua ama kukaa kimya, kuwashughulikia wahusika au kutafuta namna ya kuyapoza au kuyafunika kabisa. Vyote hivi ni kujaribu kuupoteza ukweli.
Mchana kweupe mbele ya kadamnasi mtu anatoa silaha na kumtisha mtu muhimu kama Nape ni kitu kisichokubalika hata ikitajwa kwamba serikali haihusiki – kwa maana kwamba mtoa bastola huenda siyo mtumishi wa serikali. Kama ni hivyo basi kufanyike upelelezi haraka ajulikanne ni nani, na lengo lake lilikuwa nini.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba baada ya muda hatimaye alijikita katika tukio na kutoa agizo kwa IGP kulichunguza kwa lengo la kumbaini huyo mtoa bastola na kumshughulikia. Mapema wiki hii waziri huyo alisema mtu huyo hakuwa polisi na kishatiwa mbaroni na anashughulikiwa ipasavyo. Hakumtaja jina kwa usalama wake.
Kwa usalama wake? Si bora angetajwa tu kwa sababu wananchi wakimfahamu wanaweza kujua kwamba pengine alihusika katika matukio mengine yaliyohusu silaha?
Na iwapo hakuwa askari polisi inakuwaje polisi waliodaiwa kuwapo wakati wa tukio wasimkamate mtu huyo anayetoa bastola na kumtishia mtu mwingine mchana kweupe? Tunaweza kusubiri ukweli – kwani daima huwa haufichiki.
Post a Comment
Click to see the code!
To insert emoticon you must added at least one space before the code.