0

Nakusalimu katika Bwana, Ewe ndugu na jirani wa Madini Media kutoka moyoni,Pasipo kujali Dini, dhehebu, kabila wala itikadi, sina budi kukusalimu kwa kila salaam inayomtukuza Yesu Kristo, Tumsifu Yesu Kristo... Bwana Yesu apewe sifa... Kristo Kristo... Shalom shalom... Shalom mashujaa... Habari ya uzima... 
Ninayofura sana kuona kweli unayo dhamira ya ujua kuomba na hiyo kiu naiona ndani yako, hakika wewe unazifuata nyayo za mwanzilishi wa imani hii hata kuitimiza, na ukiendelea hivo naye atakubadilisha "UTUKUFU HADI UTUKUFU HATA UFIKIE CHEO CHA UTIMILIFU WAKE KRISTO"

Basi leo imenipendeza sana nikushirikishe machache kati ya mengi katika semina iliyoendeshwa mtandaoni na mtumishi wa Mungu, Vitus Silago, kuanzia June 22, 2013 ikadumu kwa takribani wiki tatu, kwa dakika kadhaa tuungane nae kujifunza somo la "MAOMBI YENYE NGUVU NA KIBALI MBELE ZA MUNGU"

Kufikia kumalizika kwa somo hili tutakuwa tumejifunza vitu vifuatavyo:-

1. Maana ya maombi. 

2. Faida za maombi.

3. Vitu vya kuzingatia uwapo katika maombi. 

4. Aina kuu za maombi na faida zake.
  • Maombi kabla.
  • Maombi baada. 
  • Maombi ya kawaida.
  • Maombi ya kufunga.

5. Aina nyingine za maombi.
  • Maombi ya Roho Mtakatifu.
  • Maombi ya kufunga na kufungua.
  • Maombi ya kusukuma.
  • Maombi kwa adui.
  • Maombi ya ushirika.
  • Maombi kwa wengine.
  • Maombi ya sifa.
  • Maombi ya shukrani.
6. Kuomba kwa kuzitaja ahadi za Mungu na sababu za kuomba kwa kuzitaja ahadi za Mungu.

Maana ya maombi.


Ni hitaji au tamanio la moyo wa mwanadamu ambalo yeye mwenyewe hawezi kujitosheleza, hivyo basi anahitaji msaada kutoka nje. Maombi ni moja ya silaha yenye nguvu sana katika ulimwengu wa roho; silaha inayoweza kuziharibu kazi za shetani, silaha inayoweza kufanya yasiyowezekana yawezekane.

Waefeso 6:11-13. Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za shetani. Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama.

Kama neno la Mungu linavyotuambia, hatushindani kwa damu na nyama; bali tunashindana na falme na mamlaka, wakuu wa giza na majeshi ya pepo wabaya. Moja kwa moja vita hivi havihitaji mwili kama mwili na silaha zionekanazo kwa macho ziingiie kupambana, kwa sababu vitu hivi haviwezi kuingia katika ulimwengu wa roho. Kwa hiyo inahitajika silaha inayoweza kuingia katika ulimwengu wa roho ilihali mpiganaji amevaa mwili wa damu na nyama. Nielewe, wote tunatambua ya kwamba tuna miili ya damu na nyama na wakati huo tuna roho, miili ya damu na nyama itakapokufa tutaishi katika roho, sasa hauhitaji kufa iliueweze kupigana katika ulimwengu wa roho dhidi ya shetani.

Ukiwa bado unaishi na mwili wa damu na nyama, bado unaweza kupigana vita dhidi ya falme za giza na majeshi yake, sasa silaha pekee unayoweza kuitumia ili kupigana vita hiyo, silaha ambayo inapenya katika ulimwengu wa roho na kuharibu kazi za shetani na kuyasulubu na kuyapa kipigo mapepo ni maombi pekee. Silaha nyingine zinakulinda wewe na uvamizi wa ufalme wa giza na majeshi yake, lakini hazikufanyi wewe upigane na ufalme wa giza na kuushinda. Ni maombi peke yake.

Marko 9:28-29. Hata alipoingia nyumbani (YESU KRISTO), wanafunzi wake wakamuuliza kwa faragha, mbona sisi hatukuweza kumtoa (pepo bubu na kiziwi)? Akawaambia, namna hii haiwezi kutoka (vita hii hamuwezi kuipigana) kwa neno lo lote, isipokuwa kwa kuomba.

Yesu Kristo mwenyewe anatuthibitishia katika mistari ya Biblia hapo juu kwamba, kuna vita nyingine hatuwezi kupigana na kushinda pasipo maombi. Ni lazima tuwe waombaji ili tuweze kuzishinda vita za namna hiyo, vita dhidi ya ulimwengu wa roho.

Vitu vya kuzingatia katika maombi.
  • Mahali au sehemu ya kufanyia maombi

Chagua sehemu yenye utulivu, isiyo na kelele na shughuli za wanadamu, ambapo unaweza kumtafakari Mungu na kuongea naye kwa urahisi zaidi. Unapokuwa sehemu yenye kelele na shughuli za wanadamu, ufahamu wako unashindwa kuzama zaidi katika kumtafakari Mungu. Sehemu nzuri unayoweza kufanya maombi kwa utulivu zaidi ni kanisani au mlimani. Ukiangalia mitume wa zamani na watumishi wa Mungu wa sasa wenye nguvu ni wale wanaojitenga na wanadamu wanapotaka kufanya maombi. Mathayo 8:1-2, Mathayo 26:36-39, Luka 6:12, Walawi 25:1, Kutoka 34:1-4.
  • Muda wa kufanya maombi.

Muda mzuri wa kufanya maombi ni wakati wa usiku, kwa sababu ni wakati tulivu na vita vinapiganika kwa ushindi zaidi.
  • Muda wa kudumu katika maombi. 

Huu ni urefu wa maombi yako; kwa mfano unafanya maombi ya kufunga labda masaa 12 halafu unaomba nusu saa au saa moja kutwa nzima, au unafanya maombi ya masaa 24 halafu unaomba masaa mawili au matatu, hakika hapo huna unachokifanya bali umeamua kushinda njaa, hayo ni maombi ya kawaida. Kama umefunga masaa 12, angalau fanya maombi kwa muda usiopungua masaa manne na kama umefunga masaa 24 angalau ufanye maombi yasiyopungua masaa nane.
  • Utakatifu. 

Unapoanza kufanya maombi lazima utubu makosa yako yote kwanza ndipo uanze kupeleka hoja zako mbele za madhabahu ya Mungu. Ni lazima utubu kwa sababu Mungu anasema maombi ya wenye dhambi ni kelele mbele zake, na maombi ya mwenye haki ni kama manukato. Kwa hiyo Mungu hawezi kusikiliza kelele (maombi ya mwenye dhambi), bali hupendezwa na harufu nzuri ya manukato (maombi ya mwenye haki). Isaya 59:1-2, Ufunuo 5:8, Mithali 15:8, 29, Zaburi 34:15, Yohana 9:31.
  • Imani. 

Ni mkono wa kupokelea majibu ya maombi yako kutoka kwa Mungu, huwezi kupokea majibu yamaombi yako kama huna imani. Luka 11:24, Luka 9:2, Mathayo 17:19-20, Yakobo 5:15.
  • Usifanye maombi ya kujiinua au kujisifu. 

Siku zote Mungu anapendezwa na mioyo iliyoshuka, mioyo inayonyenyekea. Moyo wa kujiinua ni chukizo mbele za Bwana. Luka 18:11-14.
  • Tunaomba kupitia Jina la Yesu Kristo. 

Ukiwa umejitakasa na umeambatanisha imani, ukilitumia Jina la Yesu Kristo hakika utayaona matokeo ya maombi yako. Hatuna jina jingine tuliloagizwa kulitumia katika maombi yetu, ni Jina la Yesu Kristo pekee. Yohana 14:13-14, Yohana 15:16.
  • Usilalamike, peleka hoja mbele za Mungu. 

Kuna baadhi ya watu wanapofika mbele za Mungu kwa ajili ya kuomba, badala ya kuomba wanaishia kulalamika. Kwa mfano umefikwa na ugonjwa, usilalamike bali muulize Mungu nini makusudi ya ugonjwa huo? Na mwambie kuwa unataka kupona, ili uendelee kuifanya kazi yake ambayo inasimama kwa sababu ya ugonjwa uliokupata. Unapopata nafasi ya kusimama mbele za Mungu, hakikisha unaongea hoja zenye nguvu na siyo unatoa lawama tu, Mungu hajawahi kujibu lawama za mtu hata siku moja. Isaya 43:26, Habakuki 2.
  • Kuna maombi hayaendi pasipo sadaka. 

Hapa ni lazima uwe makini kumsikiliza Mungu, unaweza ukawa umeombea jambo moja kwa muda mrefu halafu hupati majibu, huenda Mungu anasema na wewe kwa habari ya kumtolea sadaka lakini unashindwa kumuelewa. Mungu anaweza akasema na wewe kwa sauti ndani ya moyo wako uwapo katika maombi, ama akasema na wewe kupitia watumishi wake. Yona 2:1 na 9-10, hapa ni maombi ya Yona ndani ya tumbo la samaki, licha ya kuomba maombi marefu yule samaki hakumtapika Yona, lakini katika mstari wa 9, Yona alisema nitatoa sadaka an kuziondoa nadhiri zangu, Biblia inasema, Mungu akasema na yule samaki naye akamtapika Yona. Kwa hivyo, kuna maombi yanasukumwa na sadaka. Ukitaka kubalikiwa kwa habari ya mwili, toa fungu la kumi (zaka). Malaki 3:10-12.
  • Uvumulivu. 

Uombapo, mngoje Bwana akupe majibu sahihi kwa wakati sahihi. Kuna watu wamepokea majibu yasiyokamilika kwa sababu ya kukosa uvumilivu. Bwana anajua unatakiwa kupewa nini kwa wakati gani, ukiwa umefanya kwa sehemu yako ya kuomba, hapo mngojee Bwana naye afanye kwa sehemu yake, kukujibu. Zaburi 40:1, Warumi 8:25, Waebrania 6:15.

 Faida za maombi.

Njia ya kumjulisha Mungu haja za mioyo yetu. Tunapokuwa na mahitaji ya kiroho na kimwili mbele za Mungu, hatuwezi kumtuma mtu atupelekee hizo haja zetu mbinguni, bali tunazipeleka sisi wenyewe mbele za Mungu kwa njia ya maombi. Isaya 43:26, Isaya 1:18, Wafilipi 4:6.

Kupitia maombi, Mungu huongea nasi kwa njia ya maono au sauti ya wazi mioyoni mwetu. Matendo ya Mitume 10:9-15, hapa ni wakati Mungu anasema na Petro kwa habari ya mtumishi wake Kornelio. Mungu aliongea na Petro kwa njia ya maono wakati Petro alipokuwa katika maombi.

Maombi ni jibu la kila kitu. Maombi yakisindikizwa na vitu kama; utakatifu, imani na sadaka, hutoa jibu la kila jambo. Hufungua vifungo vya shetani, huponya magonjwa, huinua walemavu na hata magonjwa sugu na yasiyo na tiba hupata kupona. Mathayo 21:22.

Maombi hutufanya tukue kiroho. Tunapoongea na Mungu, na anapotufunulia siri za ufalme wake tuwapo katika maombi, na imani yetu inapokuwa kupitia matendo ya Mungu yatokanayo na maombi yetu, tunakuwa kiroho. Mathayo 17:14-21.

Aina kuu za maombi na faida zake.
  • Maombi kabla. 

Haya ni maombi ambayo muhusika anaomba kabla hajafikwa na jambo, kwa mfano unapoamua kuombea maisha yako ya badae, familia (mke au mume na watoto) yako ya badae ilihali haujaoa au kuolewa. Unapofika wakati huo, unashangaa mambo yanaenda vizuri, ni kwa sababu ulishaomba kabla.

Mathayo 26:41a. “Kesheni mwombe, msije mkaingia majaribuni”. 

Yesu mwenye anasema kesheni mwombe siyo muwapo majaribuni, bali msije mkaingia majaribuni. Anamaanisha tuombe sasa, ili majaribu yajapo tusije tukaingia kwayo, kwa hiyo anatuambia tuombe sasa kwa ajili ya maisha yetu ya badae.

Waebrania 4:16. “Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji”. 

Inawezekana kabisa kupata rehema na neema ya maisha na wakati wetu ujao sasa, ili tunapoyafikia maisha yetu ya baadae au kupata mahitaji katika wakati ujao tayari tunakuwa tumefunikwa na rehema na neema za Mungu na hivyo kutufanya tusimame imara. 

Faida ya maombi haya ni maombi yenye mafanikio sana, kwa sababu muombaji huomba kwa ile imani aliyonayo mbele za Mungu kupitia jina la Yesu Kristo. Hapa muombaji haombi kutokana na nguvu inayomsukuma kutoka nje, bali huomba kwa sababu anamwamini Mungu na kumfanya Mungu kuwa ndiye tumaini lake.
  • Maombi baada. 

Haya ni maombi ambayo mwombaji huomba baada ya kuingia katika jambo analoliombea. Yaani mwombaji anakuwa ameingia katika shida, ndipo anamkumbuka Mungu tena baada ya njia nyingine zote kushindwa. Ina maana, anakuwa na imani na vitu vingine tofauti na Mungu, vile vitu vinaposhindwa ndipo anamtafuta Mungu.

Zaburi 69:1-2. “Ee Mungu uniokoke, maana maji yamefika mpaka nafsini mwangu. Ninazama katika matope mengi, pasipowezekana kusimama. Nimefika penye maji ya vilindi; mkondo wa maji unanigharikisha”.

Maombi haya siyo mazuri sana kama maombi kabla, kwa sababu muombaji huomba kutokana na msukumo anaoupata kutoka na shida, tatizo au hitaji alilonalo.
  • Maombi ya kawaida.

Ninaposema maombi ya kawaida ninamaanisha maombi yasiyoambatana na kufunga (not fasting prayers). Maombi haya yana majibu pia, hasa ukiyaambatanisha na imani na utakatifu na ukifuata vitu vya kuzingatia uwapo katika maombi au kabla ya maombi.
  • Maombi ya kufunga (fasting prayers).

Haya ni maombi ambayo muombaji huamua kuingia katika maombi pasipo kula au kunywa kwa kipindi cha muda maalumu. Kwa mfano inawezekana kufunga kwa muda wa masaa 12, 24, 48 au 72, n.k ikitegemea ukubwa na umuhimu wa kile unachokiombea.

Kufunga kunakufanya uoneshe ni jinsi gani una nia ya dhati kuelekea kile unachokiombea, na kunamfanya Mungu akutegee sikio la umakini zaidi na hivyo kuitimiza haja yako kwa wakati.

1 Wafalme 21:27-29. “Ikawa, Ahabu alipoyasikia maneno hayo, akayararua mavazi yake, akavaa magunia mwilini mwake, akafunga, akajilaza juu ya magunia, akaenda kwa upole (mbele za Mungu). Neno la Bwana likaja kwa Eliya Mtishbi, kusema, Huoni jinsi Ahabu alivyojidhili mbele yangu? basi kwa sababu amejidhili mbele yangu, sitayaleta yale mabaya katika siku zake”.

Kwa njia ya maombi ya kufunga na ya unyenyekevu mbele za Mungu, Mungu akaiondoa hasira yake mbele za mfalme Ahabu.

 Aina nyingine za maombi.

Aina hizi za maombi zinaweza zikawa ndani ya aina mojawapo au mbili ya aina za maombi nilizoziongelea hapo juu katika aina kuu za maombi. Inaweza ikawa ni maombi kabla, au maombi kabla na ya kufunga ukiombea maisha yako ya baadae au watoto wako Mungu atakaokupa. 

Kwa mfano unaweza ukawa unafanya maombi ya kufunga na kufungua vifungo ambayo pia yakawa ni maombi kabla (unaombea maisha ya badae) halafu na ukawa umefunga, kwa hiyo hapo unakuwa umefanya maombi ambayo yamo ndani ya maombi makuu mawili; maombi kabla na maombi ya kufunga.
  • Maombi ya Roho Mtakatifu.

Waefeso 6:18. “kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha katika jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote”.

Haya ni maombi ambayo muombaji anaomba akiwa amezama rohoni, na Roho Mtakatifu ndiye anayehusika kuomba kwa ajili ya muombaji. Kwa nini basi tuombe katika Roho, tuangalie kifungu cha Biblia hapa chini;

Warumi 8:26-27. “Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo; lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa. Na yeye aichunguzaye mioyo, aijua nia ya Roho ilivyo, kwa kuwa huwaombea watakatifu kama apendavyo Mungu”.

Kuna sababu kubwa mbili za kutulazimu kuomba kwa Roho; hatujui kuomba ipasavyo na Roho hutuombea kama apendavyo Mungu. Kwa hiyo unaweza ukawa unafanya maombi ya Roho ukiombea maisha yako ya badae au familia yako au upate kazi.
  • Maombi ya kufunga na kufungua.

Hapa ninaposema maombi ya kufunga na kufungua simaanishi maombi ya kutokula wala kunywa, ni maombi ambayo mwombaji anatumia mamlaka aliyopewa na Yesu Kristo kuvifungia au kuvifungua vitu fulani katika maisha yake.

Mathayo 18:18. “Amini, nawaambieni, yo yote mtakayoyafunga duniani yatakuwa yamefungwa mbinguni, na yo yote mtakayoyafungua duniani yatakuwa yamefunguliwa mbinguni”.

Kwa hiyo unaweza ukafunga kabisa magonjwa katika maisha yako na hutaweza kuugua, ama unaweza ukafungua mifereji ya baraka za rohoni na mwilini kwa watoto wako hakika watabarikiwa. Kanuni ni moja tu; imani, kwa sababu Yesu mwenyewe amesema, “amini, nawaambieni”. 

Unganisha utakatifu na vitu vingine vya kuzingatia katika maombi, ukiwa umebeba imani hakika utamuona Mungu katika viwango vya juu zaidi. Kwa hiyo unaweza ukawa unafanya maombi haya ukiyaambatanisha na maombi kabla na maombi ya kufunga.
  • Maombi ya kusukuma.

Haya ni maombi ambayo muombaji hung’ang’ana na kuomba hadi apokee majibu ya maombi yake, na mara nyingi waombaji wa maombi haya huwa kuna jibu wanalokuwa wanalitegemea kutoka kwa Mungu, hivyo hung’ang’ania kuomba hadi watakapolipata jibu hilo.

Luka 11:5-9. “Akawaambia, ni nani kwenu aliye na rafiki, akamwendea usiku wa manane, na kumwambia, rafiki yangu nikopeshe mikate mitatu kwa sababu rafiki yangu amefika kwangu, atoka safarini, name sina kitu cha kuweka mbele yake; na yule wa ndani amjibu akisema, usinitaabishe, mlango umekwisha fungwa, nasi tumelala kitandani mimi na watoto wangu; siwezi kuondoka nikupe? Nawaambia ya kwamba ijapokuwa aondoki ampe kwa kuwa ni rafiki yake, lakini kwa vile asivyoacha kumwomba, ataondoka na kumpa kadiri ya haja yake. Nami nawaambieni, ombeni nanyi mtapewa; tafuteni nanyi mtaona; bisheni nanyi mtafunguliwa”.

Kabla hujaingia katika maombi haya ni vema ukamuuliza Mungu nini makusudi yake, kwani unaweza ukang’ang’ana kuomba majibu yasiyo yako, Mungu anaweza akawa amekukadilia mahali pa juu sana lakini kwa kutojua ukaomba maombi haya ukiwa umejikadilia mahali pa chini mno. Siyo kwamba Mungu hatakupa haki yako, utaopata lakini lazima uanzie kule ulikoomba ndipo upande juu.

Aina hii ya maombi, nayo unaweza ukaiambatanisha na mojawapo au zaidi ya aina zile kuu nne za maombi kutegemea na uhitaji wako.
  • Maombi kwa adui.

Hii ni aina ya maombi ambayo ni ngumu sana, na Wakristo wengi huwa hawaombi maombi ya aina hii. Haya ni maombi ambapo mwombaji huwaombea watesi na adui zake, huwaombea baraka, ushindi, mafanikio na ikiwezekana hata kuomboleza kwa ajili yao ili Mungu awape rehema.

Mathayo 5:43-44 na 48. “Mmesikia kwamba imenenwa, umpende jirani yako na umchukie adui yako, lakini mimi (Yesu Kristo) nawaambia, wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi. Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu”.

Kuwaombea adui zetu, ni agizo la moja kwa moja kutoka kwa Yesu Kristo mwenyewe. Lakini ni Wakristo wangapi leo wanaowaombea adui zao? Na siyo tuwaombee laana, maisha mafupi, kukosa kibali, la hasha, tumeagizwa kuwaombea Baraka. Hebu tuangalie kifungu cha Biblia kifuatacho:-

Warumi 12:14. “Wabarikini wanaowaudhi; barikini, wala msilaani”.   

Hapa neno la Mungu halituagizi kubagua kwamba ni nani aliyetuudhi na awe amutuudhi nini, yeyote na chochote alichotuudhi, tumeagizwa kumbariki.
  • Maombi ya ushirika.

Haya ni maombi ambayo wanajumuiya, au Wakristo wa kanisa fulani wanashirikiana kwa umoja katika kuliombea jambo fulani; aidha linahusu kanisa au linamuhusu mshirika mmoja.

Matendo ya Mitume 1:12-14. “kisha wakarudi kwenda Yerusalemu kutoka mlima ulioitwa wa Mizeituni, ulio karibu na Yerusalemu, wapata mwendo wa sabato. Hata walipoingia wakapanda orofani, walipokuwa wakikaa; Petro, na Yohana, na Yakobo, na Andrea, Filipo na Tomaso, Bartholomayo na Mathayo, Yakobo wa Alfayo, na Simoni Zelote, na Yuda wa Yakobo. Hawa wote walikuwa wakidumu kwa moyo mmoja katika kusali, pamoja nao wanawake, na Mariamu mama yake Yesu, na ndugu zake”.

Faida ya maombi haya ni kwamba, yanaonesha umoja na ushirikianao wa kanisa au jumuiya na pia yana nguvu zaidi kuliko maombi ya mtu mmoja. Siyo lazima ufanye maombi ya ushirika na kanisa zima japo ni vizuri zaidi, lakini unaweza ukafanya na baadhi ya jamaa wachache.

Mathayo 18:19. “Tena nawaambia, ya kwamba wawili wenu (ushirika) watakapopatana duniani katika jambo lolote watakaloliomba, watafanyiwa na Baba yangu (Yesu) aliye mbinguni”.
  • Maombi kwa wengine.

Haya ni maombi ambayo muombaji hutenga siku maalumu au huamua kufanya maombi maalumu kwa ajili ya kuombea wengine, yeye hajihusishi kabisa katika maombi haya. Anakwenda mbele za Mungu akibubujika na kulia kwa sababu yaw engine.

Unaweza ukaliombea kanisa lote, Mungu alisimamishe imara na kulipa kibali, alizidishie upendo, tena ikiwezekana kwa kuwataja majina washirika wa kanisa hilo. Na siyo lazima liwe kanisa unaloabudia, unaweza hata kuliombea kanisa la jirani. Au hata kuiombea familia ya jirani yako, Mungu ailinde, aibariki na mambo mengine mazuru mengi.

Wakolosai 1:9. “Kwa sababu hiyo sisi nasi, tangu siku ile tuliposikia, hatuachi kufanya maombi na dua kwa ajili yenu, ili mjazwe maarifa ya mapenzi yake katika hekima yote na ufahamu wa rohoni”.

2 Timotheo 1:3. “Namshukuru Mungu, nimwabuduye kwa dhamiri safi tangu zamani za wazee wangu, kama vile nikukumbukavya wewe daima, katika kuomba kwangu, usiku na mchana”.

Kuombea wengine (tofauti na maombi ya kuombea adui), ni agizo kwa kanisa pia; kwa sababu tusipowaombea wengine, tunaonesha ubinafsi, na kama tutakuwa wabinafsi basi kumpenda Mungu hakupo ndani yetu. Na kama hatumpendi Mungu, tunafanya dhambi.

1 Samweli 12:23. “Walakini mimi, hasha! Nisimtende Bwana dhambi kwa kuacha kuwaombea ninyi; lakini nitawaelimisha katika njia iliyo njema, na kunyoka”.
  • Maombi ya sifa.

Haya ni maombi ambapo mwombaji anayatafakari matendo makuu ya Mungu aliyomtendea katika maisha yake, sehemu ngumu alizokuvusha amabzo kwa akili zako ilishindikana, wema wote ambao Mungu amekufanyia, kukuweka kuwa hai na wakati wapo uliozaliwa nao tarehe moja, mwezi mmoja au mwaka mmoja hawapo.

Ndipo muombaji hububujika na sifa mbele za Mungu wake, moyo wake humshangilia Bwana mchana na usiku.

Zaburi 34:1 na 3. “Nitamhimidi Bwana kila wakati, sifa zake zi kinywani mwangu daima. Mtukuzeni Bwana pamoja name, na tuliadhimishe jina lake pamoja”.

Sehemu nyingine katika Biblia, maombi haya ya sifa yamefananishwa na sadaka mbele za Mungu.

Hosea 14:2. “Chukueni maneno pamoja nanyi, mkamrudie Bwana; mkamwambie, ondoa maovu yote, uyatakabali yaliyo mema; na hivyo ndivyo tutakavyotoa sadaka za midomo yetu kana kwamba ni ng’ombe”. 
  • Maombi ya shukurani.

Maombi haya kidogo yafanane na maombi ya sifa, lakini tofauti yake ni kwamba maombi ya sifa unamtolea Mungu sifa za midomo yako kulingana na matendo yake wakati maombi ya shukrani ni kwamba unampa Mungu shukrani kwa mema yote aliyotenda kwako na hata kwa wanaokuzunguka.

Waefeso 5:20. “na kumshukuru Mungu Baba siku zote kwa mambo yote, katika jina lake Bwana wetu Yesu Kristo”.

Wakolosai 3:17. “Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba kwa yeye (Yesu Kristo)”.

Kuomba kwa kuzitaja ahadi za Mungu.

Isaya 55:10-11. “maana kama vile mvua ishukavyo, na theluji, kutoka mbinguni, wala hairudi huko; bali huinywesha ardhi, na kuizalisha na kuichipuza, ikampa mtu apandaye mbegu, na mtu alaye chakula; ndivyo litakavyokuwa neno langu (Bwana Mungu), litokalo katika kinywa change; halitanirudia bure, bali litatimiza mapenzi yangu, nalo litafanikiwa katika mambo yale niliyolituma”.

Hayo ni maneno ya Mungu mwenyewe, anasema neno (ahadi) lake ni kama mvua ishukavyo toka mbinguni kuinyeshea ardhi isivyorudi mbinguni, ndivyo neno (ahadi) lake lisivyokuja tupu pasipo kutimiza mapenzi yake yaliyopo ndani ya neno (ahadi) lake. 

Unaweza ukajiuliza kama neno la Mungu lazima litimize mapenzi yake, kwa nini basi tunapaswa kuomba? Ahadi ya Mungu ipo inatuzunguka wote, kama neno lake linavyosema yeye huwanyeshea mvua wote wenye haki na wasio haki (Mathayo 5:45). Lakini ili ahadi ya Mungu itimie katika maisha yako ni lazima uombe. Tuangalie kidogo neno:-

Isaya 43:26. “Unikumbushe (ahadi yangu); na tuhojiane (uiombe); eleza mambo yako, upate kupewa haki yako (kutimiziwa ahadi ya neno langu)”. 

Hapo juu pia ni maneno ya Mungu mwenyewe, kwa nini niende mbele za Mungu kuomba anitimizie ahadi ya neno lake? Kwa nini nimkumbushe, ina maana amesahau? La hasha, Mungu hajawahi kusahau na hatakuja kusahau, tunapokwenda mbele za Mungu, tunakili na kuthibitisha imani yetu kwake. Hicho ndicho kitu, Mungu anapenda kutoka kwetu. Ndiyo maana Yesu Kristo alipokuwa akiwaponya wagonjwa alikuwa akiitazama imani iliyomo ndani ya mioyo yao.

Mungu hajawahi kudanganya na hatakuja kudanganya, lakini lazima tuombe ili tuikili na kuithibitisha imani yetu kwake. Tofauti ya imani kati kati yetu, hufanya tofauti ya kupokea kwetu kutoka kwa Mungu. Unaweza ukawa hujanielewa, ni hivi; mwenye imani haba hupokea haba na mwenye imani nyingi hupokea vingi. Kwa sababu Mungu huwatendea wanadamu wote kulingana na imani ndani ya mioyo yao.

Hebu tuangalie mistari michache ya maombi yanayounganisha ahadi za Mungu;

Maombi ya Mfalme Daudi; 2 Samweli 7:27-29. “Kwa kuwa wewe, Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, umenifunulia mimi, mtumwa wako, ukisema, Nitakujengea nyumba (ahadi); kwa hiyo mimi, mtumwa wako, nimeona vema moyoni mwangu nikuombe dua hii. Na sasa, Ee Bwana Mungu, wewe ndiwe Mungu, na maneno yako ndiyo kweli (ahadi yako ni hakika), nawe umemwahidia mtumwa wako jambo hili jema; basi, sasa, uwe radhi, ukaibarikie nyumba ya mtumwa wako, ipate kudumu milele mbele zako; kwa maana wewe, Ee Bwana Mungu, umelinena (umeahidi); na kwa baraka yako nyumba ya mtumwa wako na ibarikiwe milele”.

Zaburi 119:170. “Dua yangu na ifike mbele zako, uniponye sawasawa na ahadi (ya uponyaji; Kutoka 23:25) yako”.


Kwa nini uombe kwa kuzitaja ahadi za Mungu.
  • Ahadi za Mungu zimehakikishwa (ahadi timilifu).

2 Samweli 22:31(b). Mungu, njia yake ni kamilifu; ahadi ya Bwana imehakikishwa; Yeye ndiye ngao yao wote wanaomkimbilia.
  • Mungu hasemi uongo.

Hesabu 23:19(a). Mungu si mtu, aseme uongo.
  • Mungu ni mwaminifu, hutekeleza alichoahidi.

Kumbukumbu 7:9. Basi jueni ya kuwa Bwana, Mungu wenu, ndiye Mungu; Mungu mwaminifu, ashikaye agano lake na rehema zake kwao wampendao, na kushika amri zake, hata vizazi elfu.
  • Tukiomba sawasawa na mapenzi (ahadi) yake, atusikia.

1 Yohana 5:14. Na huu ndio ujasiri tulio nao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake (sawa sawa na neno au ahadi yake), atusikia.
  • Ni lazima atimize ahadi yake kwanza, kwa sababu ameikuza kuliko jina lake.

Zaburi 138:2. Nitakusujudu nikilikabili hekalu lako takatifu, nitalishukuru Jina lako kwa ajili ya fadhili zako na uaminifu wako, kwa maana umeikuza ahadi yako kuliko jina lako lote.

Ni maombi yangu, Bwana Mungu; afungue vilivyofungwa, arejeshe vilivyonyang’anywa, ainue huduma zilizolala, afufue huduma zilizo kufa, abariki palipo laaniwa, na akuinue mtumishi wake kutoka utukufu uliopo akupandishe juu zaidi, kwa jina la Yesu Kristo. Amina! 

Kumbuka kwamba hiyo ilikuwa ni semina iliyoendeshwa mtandaoni na mtumishi wa Mungu Vitusi Silago, kupitia blogu ya SILAGO2.BLOG, hivo usiache kutembelea blog yake ili ukue zaidi kiroho, na kama somo hili umelipenda na ungetamani kupata copy yake ya PDF basi bonyeza (HAPA)

Post a Comment

 
Top