Nimekitaja hiki chama kwa sababu ndicho kimekuwa madarakani tangu uhuru miaka 56 iliyopita – tukijumlisha na mtangulizi wake TANU.
Serikali hiyo imezinduka kwa namna tofauti – siyo kwa kuchukua hatua madhubuti ya kuiboresha elimu, hatua ambazo lazima ziambatane na mageuzi makubwa katika sekta hiyo, bali imezinduka kwa kuanza kupambana na matokeo (manifestations) ya elimu mbovu.
Na harakati za namna hii zinaonekana kama fasheni katika utendaji wa serikali, wa awamu hii na nyingine zilizopita hivi karibuni. Kwa maneno mengine mara nyingi kiini cha tatizo huwa kinakwepwa – bila shaka kwa makusudi kwa sababu za ugumu (complexity) na ukubwa wake – hali iliyotokana na kupuuzwa kwa muda mrefu.
Halafu kuna suala la watawala kupenda kuonekana kwamba wanafanya kazi kupitia utamaduni huu wa sasa wa matukio, au mazoezi (exercises) ambayo huanzishwa kwa sauti kubwa lakini muda si mrefu hupotea pole pole na kusahaulika, achilia mbali kuyafanyia tathmini ya matokeo yake.
Kwa mfano katika zoezi la mapambano dhidi ya dawa za kulevya ambalo kila mtu aliona lilikuwa la nia njema labisa – wananchi bado hawajaona matokeo yake – hasa kutokana na sauti kubwa zoezi hilo lililokuja nalo na majina makubwa kutajwa.
Hatujaona, kwa mfano mapaketi kwa mapaketi ya dawa za kulevya aina ya unga (heroin na cocaine) yaliyokamatwa na kuteketezwa, isipokuwa tuliona bangi (kwa magunia) ikikamatwa na mashamba ya mihadarati hiyo ekari kwa ekari yakifyekwa na/au kuchomwa moto. Tukio hilo limepita lakini limeacha maswali mengi katika jamii.
Nirejee mada yangu ya elimu. Hakuna anayepinga kwamba elimu ina gharama kubwa, kifedha, lakini mbadala wake — yaani ‘ujinga’ pia una gharama kubwa kwa taifa na hasa kwa serikali yake ambayo ndiyo yenye kubeba jukumu la kuona wananchi wake wanapata elimu.
Hapa Tanzania elimu ni miongoni mwa vitu viwili ambavyo vimekuwa vinaibua mijadala mizito – kwa wanasiasa, wasomi na wananchi kwa ujumla – na hasa katika kuporomoka kwa viwango vyake. Lingine ni kilimo, lakini afya nayo imeingia katika kundi hili. Hata hivyo elimu ndiyo nguzo kuu ya hivyo vingine kwani ubora wake ndiyo huweza kuendesha hivyo vingine.
Miaka 56 iliyopita Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Nyerere alitaja vitu vitatu ambavyo ndivyo vilikuwa changamoto kuu zilizokuwa zinalikabili taifa changa la Tanganyika – ujinga, umasikini na maradhi – katika mtiririko huo.
Kimakusudi mazima alilipa suala la elimu kipaumbele mkubwa na katika bajeti sekta hiyo ilikuwa inatengewa zaidi ya asilimia 40 ya bajeti ya serikali. Sasa hivi kiwango huwa hakizidi asilimia 20 hasa ukilinganisha uiano wa idadi ya watu wakati ule – 9 milioni – na sasa hivi karibu 50 milioni.
Ilikuwa bora enzi zile kwa sababu serikali haikuwa inaizungumzia elimu kwa ndimi mbili – kwani iliposema elimu ni chombo cha maendeleo, ilikuwa inajua inasema nini na kumaananisha nini. Sasa hivi mtu anaweza kuandika kurasa elfu kadha kuhusu kuporomoka kwa viwango vya elimu na kwa nini ilitokea hivyo na bila serikali kuonekana kuguswa.
Katika hali ya namna hii – ya serikali kutoonekana kuguswa kwa viwango vya elimu kuporomoka – kuwepo vyeti feki vya elimu au watu kutumia vyeti vya watu wengine ili watimize malengo yao kimaisha kamwe kusingeweza kuepukika.
Tatizo la vyeti feki ni mpacha wa lile lingine katika sekta hiyo hiyo – tatizo la kuvuja kwa mitihani. Watu wanatafuta njia za mkato kupata mafanikio maishani, kwani wanafahamu kushinda mitihani katika mazingira ya sasa hivi ya kupata elimu bora huwa changamoto kubwa.
Na kama vile katika uvujaji wa mitihani ambapo kuna madai baadhi ya wazazi kuhusika katika ‘kuwapasisha’ vijana wao kwa udanganyifu, ni hivyo hivyo kwa suala la vyeti feki – ambapo madai pia yapo kwa baadhi ya wazazi au watu wa familia kuhusika.
Lakini hili la vyeti feki mamlaka za uajiri katika serikali na mashirika yake zinahusika moja kwa moja – ama kwa kutokuwa makini wakati wa usaili, au katika mazingira ya ufisadi. Hali hiyo imeifanya sasa serikali kubeba mzigo.
Kuna mambo kadha yamejitokeza kutokana na zoezi hili la kusaka wafanyakazi wenye vyeti feki, mengine yalikuwa hayajulikani na umma – kwani hayakuwa yameelezwa rasmi. Moja ni kwamba jamii ya wanasiasa (political elite) wanaoongoza nchi huwa wana tabia ya kujipendelea. Yanapokuja masuala ya kuwajibika wao huwekwa pembeni.
Kwa mfano imeelezwa kwamba zoezi la kuwashughulikia wafanyakazi wa umma wenye vyeti feki halitawahusu watu walio katika siasa – suala ambalo tayari limeibua mjadala mkubwa katika mitandao ya jamii.
Wakati anakabidhi ripoti ya zoezi la kuwabaini watumishi wa umma wenye vyeti feki Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah J. Kairuki alisema zoezi halikuwahusu viongozi wa kisiasa ambao wako serikalini kama vile wakuu wa mikoa na wa wilaya ambao mamlaka za uteuzi wao ndiyo zinajua ufanisi wa kazi zao.
Sasa wananchi wanaanza kupata mwanga kwa nini hatua za maendeleo ya nchi zinasuasua. Ni vigumu kukwepa kutaja viwango duni vya elimu ya wanasiasa wengi ambao wamekuwa wakiongoza taifa hili kwa muda mrefu.
Wanasiasa wetu – ma-DC na ma-RC ndiyo wasimamizi wakubwa wa sera za serikali iliyopo madarakani – hasa maeneo ya vijijini hivyo kama baadhi yao hawana elimu ya kutosha inayoweza kumpa uelewa wa mambo mengi ya kimaendeleo, basi huwa ni mtihani mkubwa kwani utiifu pekee kwa mamlaka hausaidii kuibua maendeleo.
Halafu kuna baadhi ya watu wanasema hatua ya kuwatenga wanasiasa wasihusishwe katika zoezi hili la kitaifa kunaondoa ile dhana nzima ya haki na usawa. Kwani vyeti feki ni vyeti feki tu, haijalishi ni aina gani ya mtu katika utumishi wa umma amefanya jinai hiyo au nani aliyemteua. Na hapa pia wanatajwa wafanyakazi katika majeshi yetu.
Kwa mfano katika jeshi la Polisi haitakuwa haki kwa baadhi ya maafisa wa jeshi hilo vyeti feki kusimamia na kuwashughulikia watumishi wengine wa umma waliokutwa na vyeti feki. Si haki hata kidogo.
Hapa Tanzania kuingia katika siasa siyo lazima uwe na elimu kubwa – na sifa kubwa kuwania ubunge au diwani ni kujua kusoma na kuandika tu. Wenzetu Kenya walilibadilisha hili siku nyingi, juzi juzi wamefanya marekebisho kwamba kuwa Mbunge lazima mgombea awe na digrii angalau moja haidhuru.
Mfano ufuatao unawezekana kabisa upo: Inawezekana kuwepo kwa mtumishi serikalini alikuwa na cheti feki cha Kidato cha Nne. Lakini miezi kadha baadaye aliacha kazi serikalini baada ya kuteuliwa kuwa DC.
Sasa kutokana na kauli ya Mheshimiwa Kairuki, mtu huyo ‘kasepa’ (kapona) kung’olewa au hata kushitakiwa kwa kuwa na cheti feki kwani utumishi wake sasa ni wa kisiasa – haguswi na zoezi hili. Kwa maneno mengine hapa Tanzania kwa wafanyakazi wa umma‘ufeki’ wa cheti cha elimu hautokani na maana halisi (definition) ya neno hilo bali unatokana na mamlaka ipi iliyemteua.
Post a Comment
Click to see the code!
To insert emoticon you must added at least one space before the code.