0

Mmmmm….!!!
Kila nikiangalia picha hii najikuta tu nahama kimawazo, nauli yangu ni maswali nasafiri kifikra hadi stendi kuu ya chozi iliyopo Rhotia Karatu ambapo naongezewa nauli ya kurudi May 6, 2017.

Ndugu zangu, washiriki wa Madini Media, kwanza kabisa nitoe pole kwa wote walioguswa na jambo hili, huku nikiwasihi kufuta machozi kila mmoja kwa leso yake maana huwezi jua, wenda ya mwenzio ina pilipili.

Shukrani zangu za pekee ni kwao wote waliofanikisha kuisitiri miili ya wenzetu katika nyumba maalumu, kama heshima anayostahili kila mwanadamu pindi anapomaliza safari yake ya hapa duniani.

Wakati naandika haya mmoja akasema, “Hili la ajari limepitwa na wakati…” sikutaka kuongelea hizo habari zake ili asije akaelewa, nachoshangaa naye ni mwandishi, nachoshukuru si wa Media hii maana angetutia hasara.

Linapotokea jambo zito kama hili hakuna ulazima wa kukimbizana ku-copy na ku-pest habari za hivi punde ‘breking news’ kwa raia badala ya kukimbizana katika ofisi mbalimbali za kuweza kutoa msaada wa haraka.

Kwa sababu hamkupata kutoa ya moyoni kupitia hii media ambayo wengi mnapachukulia kama nyumbani, basi leo nakupa hiyo fursa kupitia comments lakini kwanza nikushirikishe machache ninayotafakari hata sasa:

⇗Vifo 35 Ni Shangwe Fb Na Insta.
⇗Kauli za kikatili kutoka tabaka la juu.
⇗Thamani ya misiba katika vyombo vya habari.
⇗Muarobaini…!!!

Kwa wale wenzangu wenye bifu na maandishi wanatamani niishie hapo, weee… thubutu! Lazima niendelee mpaka mwisho na nifafanue kila kimoja, na bila kuchoshana tuanze na hii pointi ya kwanza.

⇛VIFO 35 NI SHANGWE FB NA INSTA.

Asilimia kubwa ya jamii walipokea hizi habari kupitia mtandao wa Facebook, na waliozipokea kwa njia ya instagram pia ni wengi, kutokana kwamba hii mitandao inasifika sana kwa picha na ni rahisi kuitumia.

Sema kuna jambo nimegundua, yaani watumiaji wa mitandao hii wako speed kuliko muda na ni majasiri hujawahi ona, hata hawatoi ufafanuzi zaidi ya kutupia tu picha za miguu na vichwa vya watoto.

Mapokezi ya picha hizi ni makubwa sana kutokana na maelfu ya watu walioonesha kuzipenda ‘likes’, kila mmoja akijitahidi kusema chochote ‘comments’ na pendo katika kushirikishana ‘shares’.

Hakika hizi ni zama za swala kuwinda simba, mambo yamebadilika, imefika wasaa binadamu wana roho za kinyama, imekuwa heri mara mia mwanadamu kufanya urafiki na wanyama flani-flani wana roho za utu.

Fanya utafiti leo katika post zote zinazohusu ‘kuzuia ajali za barabarani’ utakuta hazina likes wala comments, kisha geukia hizi zinazoonesha vipande vya miili utakuta zina mamia ya likes na comments.

Furaha ya wana-fb na insta ni kuona matukio mabaya ya kusisimua, ila wana areji na post zinazohusu mbinu za kujikinga na mabaya, ndio maana nikasema, “VIFO 35 NI SHANGWE FB NA INSTA”

⇛KAULI ZA KIKATILI KUTOKA TABAKA LA JUU.

Naskia baba yenu kasema wanahabari hawana uhuru kama wanavodhani, ila hii kauli sidhani kama inanizuia kutoa pole kwa mwakilishi wa jimbo la Arusha mjini kwa msiba huu maana unamgusa moja kwa moja.

Tuliokuwepo wakati wa kuaga miili tulimwona na tulitaraji ataongea chochote lakini ikawa tofauti, kumbe mama yenu aligoma kumpa nafasi, hata kaka Mbowe alipomkumbusha mama bado juhudi ziliangukia ziro.

Ni mengi yameongelewa kuhusiana na hili pigo tulilopata, wenye busara zao na hata vifata upepo wote wameonesha ushirikiano katika kuishauri serikali ili ikiwezekana jambo kama hili lisitukie tena hapa nchini.

Hoja zenu za msingi naamini wahusika watazifanyia kazi kwa kadri mlivyowaamini hata kuwapa dhamana ya pale walipo, ila nina neno juu yao kuhusiana na kauli walizokuwa wakitoa, na hizi ni baadhi:-

  • Wanafunzi ni taifa la kesho.

Watu wengine bwana, Mungu awasamehe tu maana hawajui wayanenayo, au mmesahau kuwa uzima na mauti u kinywani mwenu, kinywa huumba, leo unatamka kuwa thamani ya wanafunzi itaonekana kesho.

Ndio maana hata hamjali usalama wao leo, kachunguze vyakula, mahari wanapolala, gusa na nidhamu, ukitoka huko ingia kwenye school bus, kuna wakati utakutana na benchi ndio siti, na dreva lazima awe ndugu.

Serikali ya viwanda lazima iwe makini hasa kwa hawa wanafunzi tunaowategemea baadae, serikali ya vibanda ndio wakati wowote inaweza kuharibiwa kwa upepo na kuleta mauaji kutokana na udhaifu wa misingi yake.

  • Kupunguza ajari.

Kuna kipindi nawaza mpaka nachukia, yaani na hiyo mikakati yote ya usalama barabarani, majumbani, viwandani, mashuleni, mahospitali na kwingineko, kumbe nia na madhumuni ni kupunguza ajari, kupunguza tu!

Bajeti kubwa inatengwa kwa ajili ya kulipia matangazo katika vyombo mbalimbali vya habari, kununua air-time redioni, show-time katika runinga na space katika machapisho, kumbe yote hayo ni mbinu za kupunguza tu.

Unaweza kupunguza ajari 9 kati ya 10 (90%), ila hiyo moja tu uliyoiruhusu ikaandika historia kubwa kuliko hii, sitaki kumfundisha kazi awaye yote ila nachoamini kuwa bora ni mbinu za kuzuia ajari na sio kupunguza tu.

  • Msiba wa kitaifa.

Nakumbuka sana eneo hili la tukio, maana ndipo alipopatia ajari babu na bibi wakiwa wamebebana kwenye baiskeli wakitoka hospitali na wote wakafa, sikuskia habari za uchunguzi maana huo ulikuwa ni msiba wa kiukoo tu.

Maisha ya A yaliishia pale pale kwa pikipiki, akafata B akiwa na NOAH, hawa wote ni ndugu, na tabaka la juu halikuongea chochote kwa sababu haihusiani na taifa, tulipojaribu kuomba msaada tukaambiwa ni msiba wa kifamilia.

Leo chunusi imegeuka jipu ndio mnakimbizana kusimika bendera ya taifa, kisa msiba wa kitaifa, kivipi wakati mwakilishi wa taifa katika eneo hilo alinyimwa nafasi ya kutoa hata pole, maslahi binafsi bifu hadi msibani, waone!

⇛THAMANI YA MISIBA KATIKA VYOMBO VYA HABARI.

Utakubaliana nami kuwa kazi kuu tatu za vyombo vya habari ni kuhabarisha, kuelimisha na kuburudisha jamii, ila kwa media za kibongo ni nadra sana tangu mamluki walipovamia hii tasnia kwa masilahi yao binafsi.

Tabaka la juu katika hii tasnia kumejaa kukuru-kakara hadi nguo ikachanika mmoja katishiwa bastola, aliyenunuliwa nguo mpya ndio kwanza haielewi ni ya kike au ya kiume, usimuulize, sababu nguo ni nguo na tayari katokelezea.

Tabaka la chini wamekula chunvi nyingi katika darasa la hii tasnia, leo wanadai ni muda wao sasa wa kulamba sukari, wanaisaka kwa udi na uvumba, kwa njia halali na hatari wao wamo tu mradi ulimi uguse kiganja.

Mpaka kesho wasaka kiki katika media wanajua, hakuna kiki kubwa kuliko kufa, maana hapo kazi zako zitasapotiwa bila gharama, hata mdogo wako wa mwisho atafanyiwa interview, any way, tuangazie baadhi ya media.

  • Milard Ayo

Huyu kijana anasifika ndani na nje ya nchi kutokana na bidii zake katika kutoa habari za haraka na makala zenye ukweli na usahihi, zinazogusa jamii na anatajwa kuwa changamoto kwa wanahabari wa Tanzania.

Nilipoona picha za ajari fb, nikakimbilia kwenye blog yake nipate ufafanuzi zaidi, ndio kwaaaza kabadilisha front view kajaza picha na habari za Frola mbasha kusifiwa na mume wake mpya na picha za hamo-wolper.

Sababu namuamini nikaanza kufuatilia posts, sasa yeye kazidi wote kwa post za vipande vya miili ya watu, ndo nikajiuliza ni chuo gani alichosoma huyu jamaa hata hajui sheria, sera na maadili ya uandishi wa habari.

  • Bongo5

Baada ya kaka yenu kunichanganya ikabidi nisitoke haraka mtandaoni bali nipitie na blog nyingine sababu naamini kuna wanahabari wengi wanafanya poa kuliko yeye, ndo nikaangukia nyumbani Bongo kwa mara ya kwanza.

Kufunguka tu nilipokelewa na matangazo ya makampuni makubwa-makubwa Tanzania, nikahisi hapa ndio penyewe, kumbe ndio kwaaanza wanaungana na udaku kusema chanzo cha ajari ni dreva kupigwa busu na mwanafunzi.

Siwezi kumbuka niliumia kiasi gani nachokumbuka nilizima simu kwa zaidi ya siku, na baadae sana nikafungulia redio nipate kuskiliza kuhusiana na taratibu za mazishi, nikaanza na hawa wenye mitambo mikubwa.

  • Clouds Fm.

Hii ni redio ya kiburudani, nisijue kama ndio sababu ilikuwa radhi kusinzia siku kadhaa ili zisirushwe habari za huzuni, au ndo vile kihamorapa tayari, nikae na Samson Petter ‘Spy-D’ tumchunguze anayelia sana msibani.

Mbona sijasikia habari za kufuliza siku kadhaa kwa ajili ya kutoa elimu juu ya usalama wa watu na mali zao bila malipo, ili wasikilizaji wajielewe na kutambua jinsi gani wanaweza kujiepusha na maafa yanayotukia kila siku.

Angelikuwa mwanamziki ndio kafa, e eeee… ungeshuhudia hiyo shughuli yake anavopewa promo na zitachezwa kazi zake hata alizoandaa akiwa kijijini sinazokoroma, zisizo na ubora zinalembwa kama mwanamwali vile.

⇛MUAROBAONI.

Nikupongeze kabisa ewe ndugu ulieketi nami jirani kwa kwa nia moja hata sasa, kwa umakini ukipata hekima mbili tatu, katika machungu ukachukuliana nami nia na madhumuni tufikie hapa ulipo muarobaini wa yote.

Changamoto nilizoainisha ni chache sana kulinganisha na movie nzima ya kila siku tunayoshuhudia vibandani, kwa habari ya viwanda wanajua wawekezaji na wakubwa, na kama utajitoa kuhoji pia uwe radhi kujitoa kitoweo.

Walipo wengi halishindikani jambo, mawazo yangu ni 1 ya 3 ya suluhisho, nawe ukitoa 1/3 na yule 1/3 tayari 3/3=100% ya suluhisho itapatikana, basi fanya hivo sasa kwa kukomenti maoni na ushauri wako kwa jamii nzima.

Asante kwa kutembelea Madini Media, nakusihi sana kwa muda huu kagua vipengele mbalimbali katika blog hii ili ujue mengi sana kuhusu maisha yako, na jitahidi basi kila siku upitie hapa uone tumekuandalia nini.

©M(F)25MA17-03
Author:         Fiacrius K. Otto
Editor:          Samson P. Duttu
Allowed:       Share, copy&paste
Don’t try:      To edit any.

Post a Comment

 
Top