0
Na Fiacrius K. Otto, Morogoro

Wazazi wa wanafunzi wa shule ya msingi area 5 iliyopo kata kichangani manispaa ya morogoro, wamehamasika kujiunga na shirika la Umoja wa Walimu na Wazazi (UWAWA) ili kudumisha uhusino na walimu huku shule hiyo ikikumbwa na changamoto ya ukosefu wa huduma ya choo.




Kupitia mkutano wa wazazi uliofanyika asbuhi ya jumatatu hii kwenye eneo la shule hiyo, mwalimu mkuu, Brandina Muhai, ametambulisha shirika hilo mbele ya wazazi, walimu na jamii nzima iliyohudhuria mkutano huo na kueleza dhamira yao katika mashule.

Amesema UWAWA ni shirika lisilo la kiserikali, lililosajiliwa na serikali kwa lengo la kujenga ukaribu na maelewano mazuri kati ya wazazi na walimu, kuhusiana na taarifa za maendeleo ya wanafunzi na kuchangia mawazo juu ya uamuzi bora unaofaa ili kuleta matokeo chanya.

Mwalimu mkuu amesema, “unajua mtoto wako akifeli wa kwanza kulaumiwa ni mwalimu, shule ikishika mkia mwalimu mkuu anakabidhiwa kinyago. Sasa shirika hili linataka tuubebe wote mzigo wa wanafunzi, na watoto wenu pia ni watoto wetu, tushirikiane sasa kuwakuza.”

Ameeleza kuwa mawasiliano mazuri kati ya wazazi na walimu hujenga mahusiano mazuri kati ya wanafunzi na walimu, ambapo itawapa urahisi wa kujua changamoto zinazomkabili mtoto anapokuwa shuleni na hata nje ya mazingira ya shule na njia bora ya kumsaidia.

Wazazi wakashangilia aliposema, “Mtawachagua wajumbe wenu hapa watakaowawakilisha, nao watakuwa na uhuru wa kutembelea shule, waingie hata madarasani kukagua au kuwauliza wanafunzi swali lolote, na kwa lolote anaruhusiwa kuhojiana na walimu, pia mmoja wao atakuwa katika wageni waalikwa katika vikao vya kamati ya shule.”

Amewahakikishia wazazi kuwa matokeo makubwa ya umoja huu ni kukuza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi katika masomo, kuwa na afya bora pia kuhakikisha kuwa wanafunzi wote wanadumu katika maadili mema wakiwa ndani na hata nje ya mazingira ya shule.

Bi. Brandina amewataka wazazi kumwamini huku akitoa mifano mbali mbali ya baadhi ya shule zilizofanikiwa kutokana na umoja huu, hivo kuwaasa kujiunga kwa mafanikio ya wanafunzi na jamii kwa ujumla, kisha akawapa nafasi wazazi kuuliza maswali na kutoa maoni ili kutambua utayari wao.

Wazazi wameonesha kuhumasika na sera za UWAWA na kuonesha utayari wa kujiunga, na kwa yeyote aliyeinuka na kuunga mkono hoja amepigiwa shangwe kubwa ya makofi na vigelegele, na katika wote hakuna aliyetoa hoja ya kupinga wala kuukosoa umoja huu.

“Tumeskia matukio mengi ya walimu kupigwa, walimu kulazwa makaburini, walimu na wazazi wamekuwa maji na mafuta hadi wengine hawaishi kwa amani katika mitaa yetu. Lakini katika UKAWA mimi nina wanangu watatu hapa, ila tayari nimeanza kuona wanafaulu. Mimi binafsi nimelipokea kwa furaha hasa ulipogusia swala la afya na maadili…” amesema mzazi wa Assad Said.

Bi. Brandina amewapongeza wazazi kwa uelewa wao juu ya hoja za maendeleo, akatoa utaratibu wakachagua wawakilishi tiyari kuanza kazi, na akitaka kuthibitisha utayari wao kushirikiana akaingiza ajenda ya choo, akisema, “Ongeza makofi kwa wajumbe wa UWAWA na kwa umoja tuchangie ujenzi wa choo.”

Ghafla zikasikika sauti za kuguna na kunong’ona, akaendelea kuwaeleza kuwa ni zaidi ya siku tano shule haina huduma ya choo kabisa kutokana wa nalichokuwa wakitumia walimu na wanafunzi kuharibika na tiyari muhandisi amekifunga kwa maandishi ya barua aliyoanza kuisoma.

Akawataka wazazi kwenda katika choo hiyo ili kuthibitisha hatari waliyonusurika wanafunzi baada ya sakafu ya choo hiyo kubomoka na baadi ya sehemu kutitia, ampapo uongozi wa shule ulipiga marufuku wanafunzi na walimu kujisaidia katika choo hiyo.

Akionesha uso wa huzuni akauliza, “Tumekuwa tukijibana huko huko na wanafunzi, wakiwa darasani tunaenda sisi, kipindi cha break wao ndio wanaenda kujazana. Sasa jiulize watoto wenu sasa wakipata haja wanaenda wapi, au ndio mnaendelea kutupa mzigo wa kuzoa?”

Akasema kabla ya kuitisha mkutano wa wazazi, walikaa kikao cha walimu na kujadili suluhisho la haraka litakaloweza kunusuru afya ya walimu na watoto, ambapo waliandika barua katika idara husika, iliyomtuma muhandisi kwa ajili ya uthibitisha na kukifunga kwa maandishi.

Mhandisi huyo alisema ujenzi wa choo mpya ya kisasa utagharimu zaidi ya Tsh. 3,400,000 na taarifa kutoka idara ya maafa zinadai kuwa kwa sasa hakuna bajeti inayoweza kukidhi adha hii, na kushauri shule kufungwa, wanafunzi na walimu kuhamishiwa shule nyingine.

Hutua hii ilimlazimu Bi. Brandina kuitisha kikao cha kamati ya shule, ambapo waliafikiana kujenga choo cha muda kitakachogharimu Tsh 800,000 ambayo watachangia wazazi kwa sababu shule haina akiba ya hela yeyote kwa ajili ya dharula, ujenzi ama ukarabati.

Hadi mwisho wa mkutano wa wazazi walikubaliana kila mzazi kuchangia Tsh. 10,000 na kutoa kipindi cha mpito cha siku tano, na baada ya hapo Bi. Brandina akahaidi kusimamia ujenzi na kuhakikisha umekamilika ndani ya wiki moja moja mara tu baada ya kupokea michango.

Amesisitiza, “Nimefanya kazi na nyie kwa zaidi ya miaka 9 mpaka leo hamjawahi kuniangusha. Natarajia kuwaita hapa baada ya wiki moja au mbili ili mjionee kazi ya hela yenu ambayo mmejitolea. Kuweni waaminifu mchangie hiyo helandani ya siku tano nianze kazi.”

Madini Media imeongea na baadhi ya wazazi baada ya mkutano, hapa Bw. Maneno Julias anatoa mtazamo wake, “Namshukuru sana mwalimu mkuu ametuepusha na hii ya watoto kuhamahama maana ingetugharimu pesa nyingi, hakika ametusaidia sana.”

Wazazi wametoa shukrani zao kwa jamii nzima inayoizunguka shule hiyo ambayo wamedhihirisha upendo wao kwa wanafunzi kwa kuwawezesha kupata huduma ya choo bila kizuizi katika makazi yao hadi pale changamoto hii itakapopatiwa utatuzi.


Mwishoni mwa mwaka 2016 baadhi ya vyumba vya madarasa ya shule ya msingi area 5 viliezuliwa kutokana na mvua kubwa iliyoambatana na upepo, kwa umoja wazazi wakashirikiana kufanya ukarabati ili masomo yaendelee kisha wakajenga kisima cha maji. 



Post a Comment

 
Top