0
RUFAA ya aliyekuwa Mbunge wa Longido, mkoani Arusha, Onesmo ole Nangole (Chadema), inatarajiwa kusikilizwa leo na kesho katika kikao chake cha Mahakama ya Rufaa chini ya majaji watatu kitakachofanyika jijini Arusha.


Majaji wa Mahakama ya Rufaa watakaosikiliza kesi hiyo ni Sauda Mjasiri ambaye atakuwa Mwenyekiti wa kikao hicho akisaidiwa na Mussa Kipenka na Ibrahimu Juma.


Nangole katika rufaa yake anapinga uamuzi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha uliotolewa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Bukoba, Silvangirwa Mwangesi, Juni 29 mwaka huu ambaye alitengua ushindi wake wa ubunge wa Longido.

Alitengua ubunge huo katika kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi namba 36 ya mwaka jana iliyowasilishwa na mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Stephen Kiruswa.

Nangole anawakilishwa na mawakili wawili waliomtetea Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha ambao ni Method Kimomogolo na John Materu na Dk Kiruswa alikuwa akitetewa na mawakili watatu Dk Masumbuko Lamwai, Edmund Ngemera na Daud Haraka.

Mawakili wa Nangole wamewasilisha sababu sita za kupinga uamuzi wa Jaji Mwangesi wa kutengua ubunge wa mteja wao na wameiomba Mahakama ya Rufaa kutengua hukumu hiyo kwa kumtangaza Nangole kama mshindi halali wa kiti cha ubunge jimbo la Longido.

Moja ya sababu za rufaa ya Nangole ni pamoja na kudai kuwa Jaji Mwangesi alikosea kisheria kwa kushindwa kuamua iwapo kilichotokea kwenye chumba cha majumuisho kilikuwa vurugu ama mzozo tu wa maneno.

Kimomogolo na Materu katika madai yao pia walitoa sababu kuwa Jaji alipotoka kwa kusema kulikuwa na kasoro nyingine tano zilizosababisha msimamizi wa uchaguzi Jimbo hilo kutangaza matokeo bila ya kuwapo kwa Dk Kiruswa.

Sababu nyingine ni pamoja na Jaji kukosea kisheria kutotambua ujanja wa Dk Kiruswa alipodai kwamba yeye na timu yake hawakuwahi kufanya majumuisho yao wenyewe ya kura alizopata kwa mujibu wa fomu 21b za vituo vyote 175 vya Jimbo la Longido.

Wakili Dk Masumbuko Lamwai kwa niaba ya mteja wake amewasilisha rufaa kitanzi yenye sababu mbili kwa Jaji Mwangesi alikosea kwa kutotilia maanani ushahidi wa matamshi ya kashfa yaliyotolewa na Nangole na mawakala wake.

Post a Comment

 
Top