0
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema serikali ya awamu ya tano imedhamiria kuondoa ucheleweshwaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu ili kuondoa migogoro kati ya wanafunzi na serikali yao.


Ameyasema hayo Jumanne hii jijini Dar es Salaam wakati akifunga kilele cha maadhimisho ya miaka 55 ya chuo kikuu cha Dar es Salaam ambapo alisema serikali inasimamia utendaji wa umakini na haitavumilia tena ucheleweshwaji wa makusudi wa malipo ya fedha za mikopo ya elimu ya juu.
“Sherehe kama hizi hutoa fursa kwa wahusika kutathmini kwa makini mafanikio waliyoyapata na changamoto wanazopambana nazo katika kipindi kilichopita ni fursa pia kufikiria maendeleo ya taasisi husika kwa siku zinazofuata,”alisema Majaliwa.

“Serikali haitavumilia tena ucheleweshwaji wa makusudi wa malipo ya fedha za mikopo ya chuo. Kama kuna tatizo, taarifa zitolewe haraka ili kuzuia migogoro kati ya wanafunzi na serikali yao,”aliongeza.

Aidha Majaliwa amesema serikali ya awamu ya tano imedhamiria kuondoa malimbikizo ya madai kwa watumishi wa umma na kwa sasa inakamilisha uhakiki wa taarifa za watumishi ili kubaini watumishi hewa ambao hadi sasa wamepatikana elfu 16,500.

Post a Comment

 
Top