0
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
 Menejimenti ya Utumishi wa Umma
 na Utawala Bora, Angella Kairuki
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki amesema serikali imelazimika kusitisha ajira mpya za watumishi 71,496 serikalini, mwaka huu hadi pale tatizo la watumishi hewa litakapopatiwa ufumbuzi.

Akifungua mafunzo kuhusu maadili ya viongozi wa umma kwa wakurugenzi watendaji wa halmashauri za wilaya, miji, manispaa na majiji Ikulu Dar es Salaam jana, Kairuki alisema tangu oparesheni ya kutafuta watumishi hewa ianze hadi sasa watumishi 12,246 wameshaondolewa.

Kairuki alisema tatizo la watumishi hewa nchini bado ni kubwa kwani uzoefu unaonesha kuwa nchi nyingi zilizokumbwa na tatizo hilo, ni asilimia ndogo tu ya watendaji ndio iliyokuwa inawajibika.

Alisema kwa sasa serikali imelazimika kusimamisha masuala mengi ya utumishi wa umma ili ipate taarifa kamili ya aina ya watumishi waliopo, na kwamba ma-DED hao kuhakikisha wanasimamia vyema oparesheni hiyo kwani hadi sasa watumishi hewa waliobainika, takribani asilimia 90 wanatokea katika Serikali za Mitaa.

Aidha, Kairuki alisema pamoja na kugundulika kuwa tatizo la watumishi hewa ni kubwa nchini, pia serikali imebaini kuwepo kwa watumishi watoro wasiotimiza wajibu wao.

“Nawataka mkahakikishe mnawabana hawa maofisa utumishi, haiwezekani kuwepo na tatizo la watumishi hewa kubwa kiasi hiki huku pia kukiwa na tatizo la watumishi watoro, hawa maofisa kwani walikuwa na majukumu gani?” Alihoji Kairuki.

Alisema endapo serikali itabaini kuwa maofisa utumishi hao wamehusika katika matatizo hayo ya watumishi hewa na utoro, wataondolewa mara moja. “Serikali haina mchezo kila ofisa katika eneo lake, awe ofisa elimu, afya na kilimo wafanye kazi zao,” alisema.

Post a Comment

 
Top