Viongozi wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) wakiwa ndani ya Mahakama ya Wilaya ya Dodoma wakisubiri kusomewa mashitaka yao |
Mahakama imewaonya washtakiwa hao, kutofanya kosa lolote la jinai wakiwa nje kwa dhamana, vinginevyo dhamana yao itafutwa.
Washitakiwa hao wametajwa kuwa ni Patrobas Katambi (33), mkazi wa Dar es Salaam ambaye ni Mwenyekiti wa Bavicha Taifa, Julius Mwita (30) Katibu wa Bavicha Taifa mkazi wa Dar es Salaam na George Tito (28) Mwenyekiti wa baraza hilo mkoani Mbeya.
Katika kesi hiyo, upande wa mashtaka uliwakilishwa na mawakili wa serikali, Beatrice Nsana na Lina Magoma huku upande wa washtakiwa wakitetewa na mawakili watatu wa kujitegemea, Fred Kalinga, John Gigongo na Isack Mwaipopo.
Akiwasomea shtaka lao mbele ya Hakimu Mkazi James Karanyemaha, Wakili wa Serikali Lina Magoma alisema washtakiwa wanadaiwa kukutwa na maandishi yenye lugha ya uchochezi kinyume na Kifungu cha 32(2) cha Sheria ya Magazeti Namba 229 iliyofanyiwa marejeo 2002.
Alidai Julai 9, mwaka huu katika baa ya Cape Town Manispaa ya Dodoma, washtakiwa walikutwa na fulana zenye maandishi ya “Mwalimu Nyerere Demokrasia Inanyongwa na Tuungane tuukatae Udikteta Uchwara.”
Washtakiwa walikana shtaka hilo huku upande wa mashtaka ukisema unaendelea na upelelezi na kuomba tarehe ya kutajwa kwa shauri hilo. Alisema hauna pingamizi la washtakiwa hao kuachiwa kwa dhamana.
Hakimu Karayemaha alisema dhamana iko wazi kwa washtakiwa kwa kila moja kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika wenye barua kutoka kwa mtendaji kata na wawe na mali isiyohamishika, yenye thamani isiyopungua Sh milioni moja.
Pia aliwataka wadhamini kuhakikisha washtakiwa wanahudhuria mahakamani kila tarehe ya kesi na kama kuna sababu ya msingi mdhamini afike mahakamani kutoa taarifa. Alisema mshtakiwa ambaye atafanya kosa lolote la jinai akiwa nje kwa dhamana, dhamana yake itafutwa.
Washtakiwa walitimiza masharti na kuachiwa kwa dhamana na kesi hiyo imepangwa kutahjwa tena Julai 26, mwaka huu. Katika kesi nyingine, Mjumbe wa Baraza Kuu la Chadema Taifa, Joseph Kasambala (32) alipandishwa kizimbani kujibu shtaka la kutumia maandishi ya uchochezi.
Ilidaiwa na Wakili wa Serikali, Beatrice Nsana kuwa Julai 9, mwaka huu katika Kituo cha Kikuu cha Polisi, mshtakiwa alikutwa akiwa na fulana yenye maandishi ya Mwalimu Nyerere Demokrasia imenyongwa. Mshtakiwa alikana shtaka hilo na kuachiwa kwa dhamana na kesi hiyo itatajwa tena Julai 26, mwaka huu.
Post a Comment