0
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka
 ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA),
Hamza Johari (kushoto)
MAMLAKA ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imesema kwamba rada iliyoko kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Dar es Salaam imepitwa wakati, na katika vipaumbele vyake imepanga kununua rada nne kuanzia mwaka huu wa fedha wa 2016/17 ikitenga Sh bilioni 8.8.

Katika mkutano wao na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari ofisini kwao Banana jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Hamza Johari na Kaimu Mkurugenzi wa Udhibiti wa Usafiri wa Anga, Gideon Msheri, walikiri kuwa rada hiyo iliyofungwa mwaka 2002 ni ‘kongwe’ kwani kwa viwango, rada inatakiwa kutumika kwa miaka 10 hadi 12, hivyo iliyopo sasa ina umri wa miaka 14.



Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu Johari, ununuzi wa rada ni moja ya vipaumbele vya TCAA na wataanza na rada mbili kwa Dar es Salaam na nyingine jijini Mwanza katika mwaka wa fedha 2016, na kununua nyingine mbili kwa Kilimanjaro na Mbeya kwa nia ya kuifanya Tanzania iweze kuona anga yake kwa ufanisi na kwa uhakika.

“Katika mwaka huu wa fedha (2016/17) tumetenga fedha za kununua rada kwa fedha zetu za ndani. Tunataka tuwe na rada nne ambazo tunaamini zitatuwezesha kudhibiti na kuona anga yetu vizuri. Kwa sasa hali siyo nzuri, na rada iliyopo imepitwa na wakati,” alisema Johari na kubainisha kuwa mwaka huu wametenga Sh bilioni 8.8 na kiasi kama hicho kimechukuliwa kutoka fedha zilizotengwa katika bajeti ya 2015/2016.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Udhibiti wa Usafiri wa Anga, Msheri alisema gharama ya kununua rada moja ni kati ya Sh bilioni 12 hadi 16 kulingana na vigezo vya mnunuzi, huku akibainisha kuwa rada iliyopo sasa imepitwa na wakati na inahitaji kuletwa mpya na kutaja athari za kuwa na rada chakavu.

Alisema rada hiyo chakavu inainyima mapato serikali kwa sababu ndege zinatumia muda mwingi kabla ya kutua, na hivyo licha ya kupoteza mapato, lakini pia inasababisha uharibifu wa mazingira kwa sababu ndege inaposubiri muda mrefu angani inachoma mafuta mengi na kuzalisha kiwango kikubwa cha dioksidi ya kaboni na pia katika masuala ya kiusalama inaweza kuwa tatizo katika udhibiti wa ndege zinazoingia au kuruka katika anga ya Tanzania.

Rada ya sasa ilinunuliwa wakati wa Serikali ya Awamu ya Tatu na ilileta matatizo makubwa baada ya kugundulika kuwa kampuni ya BAE System ya Uingereza iliyoiuzia rada hiyo serikali iliongeza cha juu katika bei, hali ambayo baadaye ililazimika kurudisha chenji hiyo kwa Tanzania na fedha hizo zimetumika kununulia vitabu.

Post a Comment

 
Top