0
TUME ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) inatarajia kutoa mwongozo wa vigezo vya kujiunga na chuo kikuu kwa mwaka wa masomo wa 2016/17 muda wowote kuanzia wiki ijayo.

Akizungumza na gazeti hili, Ofisa Habari Mwandamizi wa TCU, Edward Mkaku alisema kwa sasa mwongozo wa vigezo hivyo uko katika hatua za mwisho kukamilishwa.

“Mwongozo wa sifa za kujiunga na vyuo vikuu iko katika hatua ya mwisho kukamilika, kamati ambayo iko chini ya kitengo cha kudahili inafanyia kazi hiyo kwa haraka ili mwongozo huo utoke kabla ya kutolewa kwa matokeo ya kidato cha sita, wahitimu waweze kuomba mara moja,” alisema Mkaku.



Mkaku ametoa kauli hiyo kutokana na taarifa zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii ikinukuu TCU kuwapo kwa mabadiliko ya alama za wanafunzi kujiunga na chuo kikuu, ambazo hata hivyo amekanusha kuwa hazijatolewa na taasisi yake.

Taarifa hizo zinaonesha kuwa, sifa za kujiunga na vyuo vikuu kwa waliomaliza kidato cha sita kabla ya mwaka 2014 ni kuwa na alama mbili za D ikiwa na jumla ya pointi nne huku wale waliomaliza mwaka 2014 na 2015 wanatakiwa na alama C mbili zenye jumla ya pointi nne.

Na kwa waliomaliza kidato cha sita mwaka 2016 wanatakiwa kuwa na alama mbili D zenye jumla ya pointi nne huku sifa za kutambua kufuzu kabla ya kujifunza, mwombaji anatakiwa kuwa na daraja B+ wakati wale wenye sifa zinazolingana wanatakiwa kuwa na angalau D na kuendelea kwa elimu ya Kidato cha Nne, basi awe amefaulu kwa alama nne.

Kwa wale wanaoingia kwa elimu ya Stashahada wanatakiwa kuwa na GPA 3.5, na wale wa cheti cha ufundi wanatakiwa kuwa na alama B huku wanaoomba kusoma Stashahada ya Ualimu na Ofisa Tabibu wanatakiwa na alama B.



Pia taarifa hiyo inayoonesha kutolewa na TCU Julai 11, mwaka huu, inaonesha kuwa programu ya kozi za awali kwa wanafunzi wasio na sifa, lakini wanaweza kuanzia ngazi ya chini, zimesimamishwa.

Post a Comment

 
Top