0
MKAZI wa Kijiji cha Rebu Kata ya Turwa, Tarafa ya Inchage wilayani Tarime mkoani Mara, Vedastus Nkwaya (44) kwa jina maarufu Kokoliko, amehukumiwa kwenda jela maisha baada ya kupatikana na hatia ya kumnajisi mtoto wa kike mwenye umri wa miaka minane ambaye ni mwanafunzi wa darasa la kwanza Shule ya Msingi Bogoti.

Akisoma hukumu hiyo juzi, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya Tarime, Marther Mpaze alisema ameridhishwa na kuungana na ushahidi wa mashahidi sita, akiwamo mtoto mwenyewe aliyemtambua na kumfahamu kwa jina la Kokoliko na kudai ni jirani yao.



Hakimu alieleza kuwa mwingine ni ushahidi wa fomu ya PF 3 uliotolewa na upande wa mashitaka ukiongozwa na Mwendesha Mashitaka wa Polisi, Bukuru Bugombe ambao mtuhumiwa alikuwa na ushahidi wake na mtu mwingine aliyejaribu kutaka kumsaidia mtuhumiwa aliyekana shitaka hilo.

Awali Mwendesha Mashitaka wa Polisi, Bugombe alidai kuwa mtuhumiwa Nkwaya, Desemba 23, 2015 saa moja jioni katika maeneo ya Mkuyuni (mtoto huyo jina limehifadhiwa) alipokuwa akitoka viwanja vya michezo shuleni kwao, alikutana na Kokoliko ambaye alimdanganyia kumpa pipi na kumpeleka nyumbani kwake na kumfungia ndani na kuanza kumnajisi, kitendo kilichosababisha mtoto huyo kupiga kelele za kuomba msaada na mtuhumiwa kukamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria. Hakimu Mpaze alisema:

“Nikubaliana na ushahidi uliotolewa upande wa mashitaka bila shaka lolote kwa kuthibitisha kosa na ninamtia hatiani mtuhumiwa Vedastus Nkwaya kwenda jela maisha ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hiyo ya kuwabaka watu wengine wakiwemo watoto.”



Kokoliko aliomba mahakama kumpa adhabu ndogo na kudai anaumwa ugonjwa wa kifafa na ana familia inayomtegemea, lakini mwendesha mashitaka aliiomba mahakama kutoa adhabu kali ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia hiyo.

Post a Comment

 
Top