0
King alipoteza mikono yake ajalini miaka mitatu iliyopita

Uingereza imefanikiwa kufanya upasuaji na kumpandikiza mgonjwa mikono ya mtu mwingine.

Oparesheni hiyo imefanyika katika hospitali kuu ya Leeds ambako mgonjwa mwenyewe amesema amefurahia kurudishiwa viungo hivyo muhimu mwilini.

'Nina furaha sana, furaha niliyo nayo yashinda hata kushinda zawadi ya pesa nyingi za bahati nasibu,'' Chris King amenukuliwa kusema.

Chris King anayetokea Doncaster huko Uingereza alipoteza mikono yake yote miwili katika ajali aliyoipata akiwa kazini wakati mikono yake ilipopondwa na mashine ya chuma miaka mitatu iliyopita.

Alipewa mikono aliyobandikwa kutoka kwa mtu mwengine ambaye alifariki.

Prof Simon Kay aliyeongoza upasuaji huo anasema King, mwenye umri wa miaka 57, ni mtu wa pili tu kufanywa upasuaji huo lakini ni wa kwanza kubandikwa mikono yote miwili hapo hospitali ya Leeds.

Bw King anasema tayari anapata hisia za mguso kupitia mikono yake hiyo mipya na anaipenda kwelikweli kwani inamfanya kujisikia amekamilika.

Prof Kay, anasema inahitaji si kuwa tu makini sana katika oparesheni kama hizo bali pia ubunifu wa hali ya juu kwani mikono ni kitu kinachoonekana mara kwa mara hivyo inakuwa kazi ya ziada kuifanya ionekane kawaida.

"Unajua unapopandikiza viungo vya ndani ya mwili kama figo, cha muhimu ni bora ifanye kazi, hamna anayejali eti inafanana vipi lakini kwa kiungo cha mwili cha nje ni tofauti,” anasema Prof Kay.

“Kwa hivyo mara nyingine kunaweza kutokea athari za kisaikolojia. Pia ni jambo ambalo halijazoeleka hata kwa watu wanaotoa viungo vya wapendwa wao waliofariki 'amefafanua Prof Kay.

Post a Comment

 
Top