Washitakiwa walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam na kusomewa mashitaka matatu chini ya Sheria ya Uhujumu Uchumi na Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori.
Washitakiwa hao ni raia wa Guinea, Ally Sharif (28) na Fatoumata Saumaolo (24); na Watanzania Victor Mawalla (29) na ndugu yake, Calisti Mawalla (22), Haruna Kassa (37) na ndugu yake Ismail Kassa (53), Abbas Hassan (40), Solomon Mtenya (46), Mussa Vigagabile (59) na Khalfan Kihengele (64).
Walisomewa mashitaka na jopo la mawakili wanne wa serikali wakiongozwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali Faraja Nchimbi akisaidiwa na Paul Kadushi, Simon Wankyo na Salim Msemwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Dk Yohana Yongolo.
Akisoma mashitaka, Wakili Nchimbi alidai katika tarehe tofauti tofauti kati ya Aprili 6 na Juni 26, 2016, Dar es Salaam kwa pamoja wanadaiwa kupanga, kuratibu, kusimamia na kufadhili mtandao wa uhalifu kwa kuuza, kupokea na kusafirisha nyara za serikali.
Inadaiwa nyara hizo ni vipande 660 vya meno ya tembo yenye thamani ya Dola za Marekani 2,105,181 sawa na Sh 4,570,547,951 bila kuwa na kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori.
Aidha ilidaiwa, katika tarehe hizo, washitakiwa walijihusisha na nyara za serikali kwa kununua, kupokea na kusafirisha meno ya tembo yenye thamani hiyo, bila kuwa na kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori.
Katika shitaka la tatu linalowakabili Sharif, Mawalla, Calist, Haruna na Hassan, inadaiwa Juni 23, mwaka huu katika eneo la Mbezi Msakuzi, Kinondoni, Dar es salaam, walikutwa wakiwa na nyara za serikali ambazo ni vipande 660 vya meno ya tembo yenye thamani hiyo.
Hakimu Yongolo alisema washitakiwa hawatakiwa kujibu mashitaka kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo isipokuwa Mahakama Kuu.
Upande wa Jamhuri ulidai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa.
Kabla kesi hiyo haijaahirishwa, mshitakiwa Victor alidai anaumwa kwa sababu ya kupigwa wakati akiwa kwenye kituo cha polisi, hivyo aliiomba mahakama itoe maelekezo ili apewe matibabu.
Hakimu Yongolo alisema Jeshi la Magereza lina fungu maalumu kwa ajili ya kutoa matibabu kwa wafungwa na mahabusu hivyo aliamuru mshitakiwa huyo apewe matatibu akiwa gerezani. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Julai 28 na washitakiwa walirudishwa rumande kwa kuwa mashitaka yanayowakabili hayana dhamana.
Post a Comment