Historia inaonyesha kwamba mali asili, kwa namna moja au nyingine, zimekuwa zikizitesa nchi nyingi duniani kuliko hata kuziletea faraja na tija – kimaendeleo na kuboresha maisha ya watu wake.
Baadhi wanasema mali asili, na hasa madini yanoyochimbwa kutoka ardhini yametokea kuwa kama laana kutoka kwa Mwenyezi Mungu (resource curse).
‘Laana ya mali asili’ ni hali ambayo huzikuta nchi ambazo zina uwingi wa madini hayo yasiyojizaa au kujiongeza (non-renewable) lakini hazina maendeleo ya maana au hata kutokuwa na maendeleo kabisa. Hii hutokea pale ambapo nchi huelekeza nguvu zake zote katika sekta hiyo ya uzalishaji – lakini wanaofaidika zaidi ni wawekezaji wa nje, baadhi ya watawala, familia zao na maswahiba wao wa kibiashara.
Mara nyingi laana hii ya malo asili hutokea katika nchi zinazojitokeza katika masoko (emerging markets) hasa baada ya kugundulika kwa wingi rasilimali hiyo nchini.
Lakini kibaya zaidi ni kujitokeza kwa ufisadi katika safu za uongozi wa juu katika nchi husika, na hii ni kwa sababu uwiano katika haki ya umiliki wa rasilimali hiyo, pamoja na namna ya kuigawa kwa jamii haijawekwa bayana, na hivyo kuibua manung’uniko makubwa miongoni mwa wananchi na hata kujikuta inaingia katika mifarakano mkubwa.
Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizojaliwa kuwa na utajiri mkubwa wa maliasili ya madini pamoja na gesi asilia bila shaka pamoja na mafuta yasiyosafishwa. Lakini pamoja na neema hii bado hali za wananchi ni duni sana.
Lakini miaka michache iliyopita tulishuhudia vurugu zilizotokea Mtwara kutokana na kutangazwa kugunduliwa matrilioni ya futi mraba ya gesi asilia katika eneo hilo.
Wananchi wa huko ambao walikuwa na manung’iniko mengi ya mkoa wao kusahauliwa kimaendeleo kwa miongo mingi walionekana kupandwa na ghadhabu kuambiwa kwamba gesi asilia hiyo, baada ya kuvunwa itasafirishwa hadi Dar es Salaam. Waliingia mitaani katika maandamano yaliyokuwa na vurugu.
Inaelezwa Rais wa Awamu ya Nne Jakaya Kikwete alifanya kosa kubwa pale alipozindua ujenzi wa bomba la gesi asilia kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam katika tukio lilofanyika Kinyerezi, nje kidogo ya Dar es Salaam mapema Novemba 2012. Bila shaka Wana-Mtwara na wakazi wengine wa mikoa ya kusini waliliona ni tukio ambalo liliashiria kwamba mambo ni kama siku zote – maendeleo ni Dar es Salaam na sehemu nyingine kwanza.
Kwa nini tukio hilo lisifanyike Mtwara, au eneo lolote huko huko kusini? Yumkini Wana-Mtwara waliona wamepuuzwa, pamoja na kwamba nishati hiyo iko chini ya ardhi yao. Hata kama serikali ina mipango yake, angalau Kikwete angekwenda huko kuzindua ujenzi wa bomba, na kuwahutubia wakazi wa huko kwa kuwaambia:
“Ndugu wananchi nimekuja kwenu kuzindua tukio la kihistoria katika mkoa wenu, tukio ambalo limewezeshwa na kuwapo kwa maliasili kubwa maeneo yenu ambayo serikali yenu (chini ya ‘uongozi bora wa CCM’) itahakikisha kwanza kabisa inawanufaisheni nyinyi kwa kutambua kwamba bado mikoa yenu haijapiga hatua kubwa za maendeleo……….n.k. n.k.” na blah, blah nyingine.
Lakini sasa hivi Rais wa awamu ya tano John Magufuli amejitosa kuangalia mali asili zetu zinanufaisha wananchi — ameanzia na dhahabu yetu ambayo imekuwa ikichimbwa na makampuni ya kigeni kwa takriban miaka 18 sasa huku nchi ikinufaika kidogo sana.
Kwa bahati mbaya waliofanikisha dhulma hiyo dhidi ya wananchi ni raia wa Tanzania, viongozi wenye dhamana kubwa katika kulinda masilahi ya nchi, ambao hawakufanya hivyo. Walishirikiana na wawekezaji katika kuwaibia wananchi kupitia mikataba mibovu ya ukamuzi. Hili lilidhihirika mapema wiki hii wakati wa uzinduzi wa Ripoti ya pili ya madini iliyowakilishwa kwa Rais.
Na kwa bahati nzuri Tanzania bado ni shwari kutokana na suala la laana ya mali asili ikilinganishwa na nchi jirani kama Congo DRC ambayo iko kwenye ukanda mmoja wa neema ya madini (mineral belt) katika Bara la Afrika. Inadaiwa ukanda huu una kila aina ya madini hapa duniani, yanayojulikana na yasiyojulikana.
Lakini DRC Congo ni nchi ambayo haijapata kuwa na amani tangu ilipopata uhuru wake miaka 57 iliyopita. Madini yake yamekuwa yakivunwa na kuondolewa kiholela kama vile nchi haina wenyewe au kuwa na mamlaka.
Kadhalika nchi za Sierra Leone na Liberia – ziliwahi kuwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe vya muda mrefu – vita ambavyo vilisababisha vifo vingi na uharibifu mkubwa wa mali. Sierra Leone ni nchi ya utajiri mkubwa wa madini ya almasi.
Kadhalika Angola, baada ya kupata uhuru ilipigana vita ya wenyewe kwa wenyewe kwa zaidi ya nusu karne na inadaiwa upande wa waasi (UNITA) ulikuwa unaigharamia vita hiyo kutokana na almasi na mbao zilizokuwa zikivunwa maeneo waliokuwa wakiyashikilia, na upande wa serikali uligharamiwa na mafuta yasiyosafishwa kutoka visima vya Cabinda. Lakini hadi sasa wananchi wengi wa kawaida wa Aangola wamezama katika dimbwi la umasikini.
Mfano mwingine ni Nigeria, nchi ambayo imekuwa ikizalisha na kusafirisha nchi za nje mafuta yasiyosafishwa tangu mapema miaka ya 1950 lakini wananchi bado hali zao duni. Aidha katika miaka ya 60 nchi hiyo ilipigana vita ya wenyewe kwa wenyewe ya umwagaji damu mkubwa, vita ambayo kwa kiasi kikubwa ilisukumwa na akiba (reserve) kubwa ya mafuta yaliyokuwapo upande mmoja kati ya pande mbili zilizokuwa zikipambana.
Aidha Wanaijeria waliendelea kufa kwa mamia kila mwaka kwa ajali za moto wakati wanapojaribu kugida mafuta kutoka kwenye mabomba ya kusafirishia nishati huyo yanayopita chini ya ardhi katika maeneo yao yenye ufukara mkubwa au hata kuyaharibu kwani waliona hayana faida kwao.
Lakini hakuna sehemu moja kubwa duniani ambayo imekuwa katika farakano za muda mrefu pamoja na vita za umwagaji damu mkubwa kama Mashariki ya Kati, eneo ambalo lina utajiri mkubwa wa mafuta yasiyosafishwa, utajiri ambao kwa kiasi kikubwa ulisababisha kuwepo kwa hali hiyo.
Lakini si kila mtu hutazama mafuta kama laana juu ya binadamu. Bi Golda Meir, Waziri Mkuu wa Israel katika miaka ya 70 aliwahi kulalamika mbele ya waandishi wa habari: “Ngoja niwaambieni kitu kwa nini si Waisraeli tuna ugomvi sana na Nabii Musa. Alituzungusha jangwani kwa miaka 40 ili tu kutuleta katika sehemu moja Mashariki ya Kati ambayo haina hata tone moja la mafuta!”
Post a Comment