Bob Marley ambaye pia alikuwa mahiri kwa gitaa aliyefariki kwa kansa ya ubongo katika Hospitali ya Cedars of Lebanon mjini Miami, Marekani mwaka 1981.
Ni kifo kilichopokewa kwa simanzi kubwa huku nadharia kinzani zilizohusisha kifo hicho na kuuawa zikiwa zimeenea.
Hata hivyo, hakukuwa na ushahidi wowote kuwa aliuawa pamoja na kwamba Bob aliwahi kunusurika kifo kwa risasi katika shambulio lililoendeshwa nyumbani kwake, ambapo alijeruhiwa mkononi katikati ya miaka ya 1970 nchini Jamaica.
Mtu aliyejaribu kumuua katika tukio hilo linalohusishwa na siasa hajulikani hadi leo hii.
Aidha, inaelezwa kwamba wakati akiwa nyumbani Jamaica miaka minne kabla hajafariki, aliumia kidole gumba wakati akicheza mpira wa miguu na marafiki zake.
Daktari aliyechunguza jeraha alibaini kuwapo dalili za saratani akamshauri dole hilo gumba likatwe, lakini Bob alikataa kwa kile alichokisema imani yake ya rastafari hairuhusu kitendo hicho.
Kwa hali hiyo, saratani ilisambaa mwilini taratibu hadi kummaliza.
Mazishi yake yaliyofanyika siku chache baadaye nchini Jamaica, yalikuwa ya hadhi ya kifalme ambapo mamia kwa maelfu ya watu, akiwamo waziri mkuu wa kipindi hicho walihudhuria.
Wakati wa uhai wake, alisifika kwa kusaidia kusambaza staili ya muziki wa Reggae na dini ya Urastafari duniani.
Muziki wa Bob ulijikita katika mambo ya kijamii, kisiasa na utamaduni si tu yaliyotokea Jamaica, bali nje ya mipaka ya nchi hiyo ikiwamo utetezi wa haki za wanyonge hasa weusi.
Katika taifa hilo, Wajamaica wengi wanamuona mwanamuziki huyo kama nembo na shujaa wa taifa.
Mtangazaji wa Jamaica, Jeremy Verity, aliwahi kusema: “Kutokana na kwamba Bob Marley alikuwa kama alivyo na alikuwa Rastafarian na kwamba alivalia na kuishi kwa jinsi alivyo hadi wakati anakufa wakati huo huo akiwa mwanamuziki na msanii mkubwa duniani huku akiwa mtetezi wa wanyonge,” ilitosha kumfanya awe kipenzi cha wengi.
Bob Marley alizaliwa katika Kijiji cha Nine Mile katika Parokia ya Mtakatifu Ann, Jamaica kwa mama mweusi kijana aliyeitwa Cedella Booker na baba wa Kizungu, Ofisa wa Jeshi la Uingereza aliyeitwa Norvall Sinclair Marley.
Baba yake huyo alikuwa Mjamaica mwenye mchanganyiko na Uingereza ambaye familia yake ilitokea Essex, England.
Norval alikuwa nahodha wa manowari za Jeshi la Uingereza, wakati alipomuoa Booker aliyekuwa na umri wa miaka 19. Norval alichangia fedha kwa mke na mtoto, lakini alionana nao kwa nadra kwa vile alikuwa haishiwi na safari.
Mara ya mwisho baba yake akiachana na mama yake, wakati Bob akijulikana kama Nesta Robert Marley, alikuwa bado mdogo sana.
Marley akaambatana na mama yake hadi Kingston ambako Booker alilenga kusaka ajira.
Mwaka 1955 wakati Bob Marley akiwa na umri wa miaka 10, baba yake huyo alifariki dunia kwa shambulio la moyo akiwa na umri wa miaka 70.
Marley alikabiliwa na maswali mengi kuhusu utaifa wake halisi kipindi chote cha maisha yake.
Wakati fulani aliitikia: “Siwezi kujikana mwenyewe. Baba yangu alikuwa mzungu na mama mweusi. Wananiita shombeshombe au vyovyote wanavyojisikia sawa. Siko upande wowote. Sizamii upande wa weusi wala weupe. Naegemea kwa Mungu ambaye aliniumba na kwa sababu natoka kwa mweusi na mweupe.”
Pamoja na kuwa mchanganyiko wa rangi, kipindi chote cha maisha yake na kwa sababu ya imani yake ya urastafari pamoja na kwamba alikulia katika Ukatoliki, Bob alijihesabu kama Mwafrika mweusi, akifuata dhana za viongozi wa Umajumui wa Kiafrika.
Marley alieleza kwamba alivutiwa zaidi na Marcus Garvey na Mfalme Haile Selassie wa Ethiopia.
Mwaka 1980 Serikali ya Zimbabwe ilimkaribisha Marley na Wailers kupiga muziki wakati wa sherehe za uhuru na Marley alihesabu hiyo kama heshima kubwa sana katika maisha yake.
Baada ya kutua Kingston, Bob alijitosa katika muziki na alijiunga na madarasa ya muziki yaliyoendeshwa na mwalimu maarufu wa muziki Joe Higgs.
Marley kama ilivyokuwa kwa vijana wengi wa Jamaica, aliuona muziki kama silaha ya kuyakimbia mateso ya ugumu wa maisha.
Aliunda makundi mbalimbali ya muziki yaliyohusisha marafiki kama vile Neville ‘Bunny’ Livingston na Peter Tosh na wanafamilia na mwishoni bendi ya Wailers ikazaliwa.
Mwaka wa 1962, Bob Marley na kina Wailing Wailers ikihusisha marafiki zake wa chanda na pete Buny na Tosh wakafanikiwa kurekodi nyimbo zao mbili za kwanza zilizoitwa ‘Judge Not’ na ‘One Cup of Coffee’.
Bob alimwoa Rita Anderson mnamo 1966, ambaye naye akajiunga na kundi lao akiwa kama mwitikiaji.
Kwa pamoja wawili hao wamefanikiwa kupata watoto watano akiwamo Ziggy Marley ambaye amefuata nyayo zake kimuziki kwa vile ni mwimbaji maarufu wa reggae.
Mwaka wa 1974, kundi la The Wailers likavunjika kwa sababu wanachama wake wakuu watatu walitaka kujiendeleza kila mtu awe msanii wa kujitegemea.
Hata hivyo, inaelezwa mafanikio ya kundi hilo lililoiteka dunia, yalishuhudia Marley akipewa heshima mno kuliko rafikize, hali ambayo haikuwafurahisha Tosh na Bunny.
Aidha, Tosh hakuonekana kufurahishwa jinsi Marley alivyoonekana kupewa uongozi wa bendi, kwa sababu zisizojulikana akisusa kushiriki ziara nyingi za kimuziki barani Ulaya na Marekani.
Lakini Bob Marley aliendelea kuita bendi yake jina la Bob Marley and the Wailers na kuingiza wanachama wapya na kuendelea kupiga muziki kama kawaida.
Mwaka wa 1975, Bob Marley akatoa kibao chake cha kwanza kilichovuma kimataifa na kiliitwa ‘No Woman No Cry’.
Baadhi ya vibao vyake vikali ni pamoja na ‘I Shot the Sheriff’, ‘No Woman No Cry’, ‘Could You Be Loved’, ‘Stir It Up’, ‘Jamming’, ‘Redemption Song’, ‘One Love’ na ‘Three Little Birds’.
Ngoma nyingine kali ni pamoja na Together with The Wailers, ‘Three Little Birds’, ‘Buffalo Soldier’ na ‘Iron Lion Zion’.
Albamu ya Legend yenye kujumuisha vigongo vyake vikali ambayo iliachiwa miaka mitatu baada ya kifo chake. Hiyo ni albamu ya reggae iliyouza sana, ikifika mara 10 kwa mauzo ya Platinum (Diamond) huko Marekani na kuuza nakala milioni 25 duniani kote.
Wakati akiendelea na safari za kimuziki Ulaya na Marekani, afya yake ilianza kudhoofu mwaka 1980, lakini hakukatisha ziara hizo.
Wakati akifanya mazoezi katika Central Park, Marekani alianguka na kukimbizwa hospitali. Alikutwa na uvimbe katika ubongo na kuambiwa kuwa ana mwezi mmoja wa kuishi.
Marley alisafiri kwenda Ujerumani kwa matibabu tata ya kansa, lakini hakuweza kupona na alitaka arudishwe akafie Jamaica, lakini halikuwezekana alifariki dunia Mei 11, mwaka 1981 mjini Miami na mwili wake kurudishwa nyumbani Jamaica kwa mazishi.
Post a Comment
Click to see the code!
To insert emoticon you must added at least one space before the code.