0
BAADA ya msanii wa Bongo Fleva, Shariff Thabeet ‘Darassa’ kuachia wimbo wake unaoitwa Muziki, kilichofuata ni kupata faida kubwa iliyozaa deni ambalo ni lazima alilipe kwa mashabiki wake.

Faida kubwa aliyoipata ni pale alipoifungua milango ya muziki wake ambayo hapo awali alishindwa kuitikisa, ila aliporudi nyuma na kujitafakari na kuja na muziki wa aina ya kipekee, alipata maonyesho ya kutosha kiasi kwamba promota asipopanda dau analolitaka akawa na jeuri ya kukataa kufanya shoo.

Ila Muziki ni wimbo uliomfanya Darassa ageuke kuwa keki ya moto na tamu kwa mashabiki, hivyo kufanya ziara sehemu nyingi ambazo ni ngumu kuingia, yeye mwenyewe anasema ukiona msanii amekubalika maeneo kama Burundi, Kongo, Mombasa Kenya na kwingineko, basi ujue kweli umefanya kazi.

Katika kipindi ambacho Darassa amefanya biashara ya muziki, basi ni mwaka 2016 mpaka mwanzoni mwa mwaka huu, ambapo ngoma yake ya Muziki ilikuwa inafananishwa na National Anthem, yaani wimbo wa Taifa na kila mwenye sikio aliinasa baadhi ya mistari ya wimbo ule.

Unaweza kuona mpaka Rais Dk John Pombe Magufuli katika hotuba zake aliwahi kuchombeza mistari kama ‘Unataka kukimbia na hauna break, what do you expect’ na kufanya ukubwa wa wimbo huo kuonekana.

Wabunge baadhi waliutumia wimbo wa Darassa kupigana vijembe na kujenga hoja zao ndani ya Bunge na hiyo haikutosha, kwani hadi viongozi wa kidini katika ibada zao walichombeza mistari kama ‘Wacha maneno weka muziki’, jambo ambalo si rahisi sana kwa msanii anayefanya muziki wa kidunia kupenyeza wimbo wake sehemu hizo.

Huku mtaani ndiyo usiseme, kwani baada ya Darassa kuleta kizaazaa na Muziki, nadhani utakuwa shahidi kwa kuwa ulishuhudia video fupi zikionyesha watu wenye rika mbalimbali wakiucheza wimbo huo kwa mitindo ya kipekee na wengine wakahatarisha maisha yao kwa kupagawa na utamu wa Muziki.

Kwa hiyo kadri wimbo huo ulipozidi kutoboa sehemu mbalimbali, ndivyo alivyozidi kutengeneza mashabiki wapya ambao wengi wao walitaka kuuona ujio wake mpya utakuwaje, huku wengine wakidai Darassa ameotea au amebahatisha kutoa wimbo huo wenye hadhi ya National Anthem.

Darassa ametambua tabia ya mashabiki wake, ile ya kulinganisha wimbo uliopita na ngoma mpya, hivyo alituliza akili yake na akapuuza presha za mashabiki, hivyo kuendelea na mipango yake bila kusikiliza mashabiki wataongea nini juu ya ujio wake mpya.

Wiki iliyopita akaachia wimbo mpya unaoitwa Hasara Roho, hii ni ngoma nyingine ya Darassa ambayo ni mwendelezo wa uandishi mzuri, staili na floo zake za kipekee, huku akiwatumia watayarishaji watatu, Mr Vs, Abba na Mr T Touch katika kutengeneza audio yenye ladha ya muziki alioubuni yeye.

Ni wimbo mzuri, unaochezeka, umebeba ujumbe murua kupitia mistari yake aliyoiandika kiufundi na imeonyesha wazi kuwa wakati anautoa wimbo huu hakuangalia mashabiki zake watasema nini juu ya ujio wake mpya.

Hanscana ameitendea haki video hii iliyofanyika kwenye mandhari nzuri tulivu huko visiwani Zanzibar, haichoshi macho na inarandana kabisa na soko la video la sasa, hivyo bila ushabiki wa kulinganisha wimbo uliopita na huu mpya, Hasara Roho unaweza kuwa na jibu, ingawa sijui kama utafika kiwango cha Muziki kiasi cha kukaririwa mashairi yake na viongozi wakubwa wa nchi, wa dini na raia wa kawaida.

Hii ni projekti mpya ya Darassa, ngoja tuipe muda tuone itakapofika, sababu toka ameuachia unazidi kufanya vizuri

Post a Comment

Emoticon
:) :)) ;(( :-) =)) ;( ;-( :d :-d @-) :p :o :>) (o) [-( :-? (p) :-s (m) 8-) :-t :-b b-( :-# =p~ $-) (b) (f) x-) (k) (h) (c) cheer
Click to see the code!
To insert emoticon you must added at least one space before the code.

 
Top