0
Mabenki yameonekana yako tayari kwa mabadiliko kadiri siku ziendavyo na faida zao kibiashara kuongezeka kufikia mwishoni mwa mwaka jana.

Sekta ya benki ilitetereka kwa kiasi  kikubwa mwanzoni mwa mwaka jana, baada ya mabadiliko kadhaa kufanyika na kuikuta sekta hiyo haijawa tayari kwa upepo wa mabadiliko uliofanywa na Serikali katika uwajibikaji wake kwa umma.


Ujio wa Rais Dk. John Magufuli uliandamana na mabadiliko mengi, yakiwamo kuboresha upatikanaji huduma na uwajibikaji wa dola kwa watu wake na kupunguza ubadhirifu wa mali ya umma na kubana matumizi holela  na yasiyo ya lazima.

Aliwawajibisha watendaji vilivyo na kuimarisha utawala wake kwa ‘kuwatumbua’ walio wabovu na hivyo kuleta ari na mtazamo mpya kwa kuacha kufanya kazi kwa mazoea.

Dk. Magufuli ameingiza utamaduni  mpya wa kuhoji na kudadisi kila kitu ili kupata ukweli wa mambo  na hivyo kufanikiwa kwa mengi.

Sekta ya benki na fedha iliathirika mwanzoni mwa mabadiliko ya Serikali pale ilipogundulika wanafanya kazi kwa mazoea  bila kuwekeza kwenye kazi za kibenki.

Rais na watendaji wake wakagundua kuwa Hazina haina fedha wakati benki yamesheheni fedha za Serikali, nayo ikizihitaji wanaitoza riba hali iliyomchefua Rais Magufuli.

Hivyo aliamua kukomesha kadhia na hali hiyo ya kijanja janja iliyoshamiri  kwa kukosa uwajibikaji na ubunifu wa kuendesha mambo  kileo.

Mrajisi wa Hazina, Lawrence Mafuru ambaye ana uzoefu wa kufanya kazi benki, alipewa agizo na Serikali la kukusanya fedha zake popote  zilipo  kwenye mtandao wa mabenki na kuziwasilisha Hazina kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Agizo hilo liliipoka sekta hiyo takribani zaidi ya Sh bilioni 500 na kuacha benki nyingi hoi na muda wa wiki mbili uliotolewa  kutekeleza  amri, ulikuwa shubiri na muhali kwa benki nyingi nchini.

Karibu ripoti nyingi za mwaka jana za sekta ya fedha nchini kwa benki, zinaonesha kuwa baadhi ya benki zimeimarika na kuongeza matawi,  kuajiri wafanyakazi wapya na huku nyingine zikifanya vibaya lakini si kwa kiwango cha kutisha kama ilivyohofiwa awali na wadau wengi.

Wadadisi wa uchumi wanasema kuimarika kwa benki ni sawa na kunywa uji wa mgonjwa.  
Kimantiki na kimaadili  kutolewa kwa ripoti za benki hizo kumepunguza hofu ya wadau wa fedha na uchumi ambao walipatwa na sintofahamu na taharuki nyingi kwa kile kilichohisiwa kuwa ni kuiangamiza sekta hiyo na haswa ilipotoka taarifa za robo ya tatu ya mwaka 2016, iliyobainisha baadhi yao kupata hasara na nyingine zikishindwa kujiendesha.

Kimsingi, benki nyingi nchini zilibweteka na kuacha kufanya kazi ya kibenki na kubaki kubangaiza mijini na kucheza na fedha ya Serikali kwa kutumia akiba, miamala na amana  za fedha ya Serikali kukopesha  taasisi, watu na Serikali yenyewe kwa faida kubwa isiyo na matatizo kwani Serikali ililipa ‘madeni’ yake.

Kitendo kilichonekana na wengi kukerwa, ni Serikali kujikaanga na mafuta yake yenyewe kama samaki ngoima wa Kilifi  au nyama ya nguruwe.

Rais Magufuli aliifuta hali hiyo na kusababisha benki zilaani na kutaharuki kwa kuwaumbua na kukosa la kufanya zaidi ya kulaumu na ‘kusema mbaya’.

Chanzo kikubwa  cha mapato halali kinachotakiwa kwa benki ni mapato  ya riba yatokanayo na mikopo inayotolewa kwa wateja wake na hivyo hufanya juhudi ya kutafuta wakopaji popote walipo na kutoa mikopo kwa wale wanaofikia vigezo, kwani benki bidhaa yake ni fedha nayo kwayo itainufaisha kama sekta na si vinginevyo.

Benki zetu kwa kujali  faida kubwa zimeshamiri mijini, hazitoi mikopo ila kwa Serikali na hivyo kukosa wateja wengine, ilikuwa  changamoto kubwa kwao.

Benki ya CRDB inayohudumia zaidi ya robo ya wateja wote wa sekta hiyo, ilitangaza kupata hasara ya takribani Sh  bilioni  2 ambayo ilifutwa na hesabu za robo ya mwisho wa mwaka jana wakati Benki ya TADB iliporomoka  na kusitiriwa na Serikali  iliyodhamini mikopo yake holela, huku Twiga Bancorp ikaishia kusimamiwa na BoT ingawa ilikwisha kutoka  hatarini miezi sita iliyopita na kuanza kupata faida ya kuridhisha.

Duru na dalili zote zinaonesha kuwa benki hiyo ilitolewa kafara kwa sababu nyingine na si za kibenki, kwani kimahesabu ilishatoka zoni ya hatari kibenki.

Benki hii iliwekwa chini ya uangalizi wa BoT kwa madai kuwa imeshindwa kujiendesha, huku akitafutwa mwendeshaji mpya.

Wadau wanaiomba Serikali iwe muwazi hapa kuleta imani ya wadau kwani benki  hiyo ilianza kutanuka kwa kuajiri na kufungua matawi mapya na hapo ndipo panga la kusimamiwa likatua.

Tuache yote, mnunuzi wa Benki amepatikana lakini hakuna la maana analoambiwa kuhusu ununuzi huo. Kwanini?



Ripoti za mwaka za benki sita zilizotathminiwa na MTANZANIA, tano zimeweza kukua kwa kuongeza  faida na idadi ya wafanyakazi wake, huku tano zikipunguza wafanyakazi kwa sababu mbalimbali ikiwamo  kuongeza matumizi ya teknolojia ya Tehama .



Benki za NMB, CRDB, KCB Maendeleo na FNB zimeajiri jumla ya wafanyakazi wapya 750, huku Letshego, UBL, TADB, DCB, Access na NBC zimepunguza wafanyakazi jumla ya 210 na hivyo kuleta urari wa kisekta wa ongezeko la wafanyakazi zaidi ya 500 ambao si haba.

Lakini suala la ajira kama kigezo cha kukua, ni tete kwani huathirika na mengi ikiwamo kustaafu, kuhamia kwingineko kitu ambacho hutokea mara nyingi kwenye sekta hii nyeti kwa uchumi. Tutanukuu baadhi yake.



Mapato yazidi kuimarika

Benki ya NMB yenye matawi 187, katika robo ya nne ya mwaka jana ilipata faida ya Sh bilioni 31.81 kufanya faida ya Sh bilioni 154.22 kwa mwaka mzima ikilinganishwa na Sh bilioni 150.29 mwaka 2015 na kuajiri wafanyakazi 269.



CRDB yenye utandawaa mkubwa ndani na nje ya nchi, imepata faida kidogo kulingana na mwaka uliotangulia kwani  kwa mwaka jana benki ilitengeneza faida ya Sh bilioni 73.42, ikiwa ni pungufu kwa Sh bilioni 50, ikilinganishwa na Sh bilioni 122.37 iliyopatikana mwaka uliotangulia. Benki iliongeza idadi ya watumishi wake kutoka 3,163 mpaka 3,432 na matawi 13 na kufikia 187.



CRDB Group ikimaanisha pamoja na Microfinance, imepata faida ya Sh bilioni 78.84 ambayo ni pungufu ikilinganishwa na Sh bilioni 128.98 zilizopatikana mwaka 2015, ingawa shughuli ziliongezeka kwa matawi yake kuongezeka kutoka 199 hadi kuwa 250.



Faida si Hoja



Licha ya faida zilizoripotiwa na mabenki  mengi, inatakiwa kutazama hali hiyo kwa kina kwani kuna uwezekano mkubwa wa kupungua kwa mikopo kutoka kwenye taasisi hizo kama wafanyabiashara wengi  nchini wanavyolalamika kukosa mikopo, au kubadilika kwa masharti ya mikopo na kuwa kandamizi  na ya kiunyonyaji kama ilivyo sasa kwa kutokuwezesha; kwa kutoza kila aina ya huduma inayotolewa nazo.

Benki zinatoza kila kitu ikiwamo hata akiba! Ni sawa na kula na uji wa mgonjwa.



Ukweli ni kwamba benki inaweza kuwa inapata faida inayopungua, hii si nzuri kwa mwenendo na mustakabali wake, kwani unahitaji uwe ni ule unaoongezeka kila mara ili kuwa na ukuaji endelevu na kuweza kukopesha.



Hali hiyo tata  inajionesha kidogo  kwenye Benki ya FNB ambayo imeongeza wafanyakazi wake kutoka 233 mpaka 284 wa kuhudumia matawi yake 10, kwani iliongeza matawi mawili mwaka juzi  na ilipata hasara ya Sh bilioni 21.64  na mwaka jana ilipungua na kuwa hasara ya Sh bilioni 20.



CRDB na gharama za shughuli zake Benki kwa ujumla wake zimekuwa mbogo na kuzidisha bei ya huduma  zake mbalimbali ili kufidia pengo la mapato ya ‘dezo’ ya awali kutoka akiba na amana za Serikali kwao.



Mfano huu tunautoa kwa CRDB Group si ndiyo yenye gharama kubwa  sana, bali ni kuonesha kwa kiasi gani benki zimeathirika na hali ya kukanganya itokanayo na sintofahamu kwa Serikali kuhodhi fedha zake na kuweka mazingira ambayo mabenki yanaona kuwa si rafiki kwao.



MTANZANIA msimamo wake ni kuwa pande hizi mbili; Serikali na benki ziingie majadiliano ya kuwezekana kufanyika yafuatayo ambayo yamekuwa msingi wa kutoaminiana.



Awali ya yote, benki zitapakae na kwenda vijijini kutoa mikopo na ushauri unaohitajika sana kwa wajasiriamali wahitaji kwa kuwa wabunifu na kuweka masharti nafuu, yakizingatia hali halisi ya kuwa na washirika wa kufanya nao kazi na mikopo iwekewe bima ya utekelezaji (business performance assurance) na kuzingatia zaidi ukubwa wa wazo la mradi badala ya vigezo vya mali zisizohamishika.



Pili, mazungumzo ya kina yanatakiwa kufanywa na Benki Kuu kupunguza baadhi ya vigezo na gharama za mikopo amabazo zinalalamikiwa na wakulima na wafanyabiashara wadogo ambao hutozwa viwango vikubwa vya riba kuliko wafanyabiashara wakubwa.



Tatu, Serikali kuondoa na  kuhodhi fedha yake ndio imeleta mdororo kwa benki na kujenga uhasama usiotakikana na kuleta msuguano wa masilahi ya sekta ya benki.



Wao kama benki wanatakiwa kutoa kauli thabiti kuhusu ukweli wa mambo  kama wana mawazo tofauti ya yale ya Serikali, badala ya kukaa kimya na kuzira kwa hali ilivyo sasa?



Nne, benki lazima iwe na mawazo tofauti na Serikali kwamba walikuwa wanajikaanga na mafuta yao wenyewe? Itafute njia bora kufanya kazi na Serikali badala ya kuiachia kila kitu.



Tano, kunatakiwa kupitia upya gharama na tozo mbalimbali za mabenki kwa wateja wao ambazo zinaonesha kuwanyonya, ukizingatia matumizi ya Tehama na huduma mbadala ya simbanking  na miamala kupitia simu za mikononi.

Sita, Mtazamo wa jumla ni kuwa gharama za benki na faida ya taasisi hizo ni kubwa zisizotakikana na zimekuwa zikiwakandamiza watu na wajasiriamali wa kipato cha chini na hivyo kuwa kinyume cha dhamira ya Serikali iliyoko madarakani ya Rais Dk. John Magufuli ambaye amedai anafanyia kazi kuinua wanyonge na walio masikini.

“Mabenki yajitazame upya ili kuwa karibu na dhamira ya Serikali,” ni kauli thabiti ya Waziri Dk. Philip Mpango alipokuwa Arusha kwenye Mkutano wa Wadau wa Sekta ya Benki na Benki Kuu mwaka jana.



Baadhi ya tozo ambazo ni kero kwa wateja kama ilivyotangazwa mwaka jana na Gazeti la Serikali la Daily News Oktoba 28 mwaka jana, ni pamoja na

Stetimenti ya muda Sh 25,000, gharama kutoa pesa Sh 3,000 na haswa utoaji wa pesa nyingi zaidi ya Sh milioni tano kwa malipo ya ya Sh150,000 ambayo awali haikuwepo na sasa kwanini wanataka notisi?

Akaunti ya Cheki (stetiment yake ni Sh 30,000 na karatasi ya kitabu cha cheki ni Sh 20,000 kila ukurasa. Wakati cheki ikikataliwa (dishonoured)  kwa sababu yoyote ile, ni Sh 350,000 na malipo ya fedha taslimu kwa mtu watatu  bila kuwa na orodha ya walipwaji (Cash payment to 3rd party without cheque list)     ni  asilimia  1 ya kiasi na chini ni 150,000  au kima cha juu ni Sh 300,000 ( 1% min 150,000 max 300,000)

Kutoa pesa nyingi taslimu zaidi ya Sh milioni 20 gharama yake ni asilimia 0.2 na kiwango cha chini ni Sh 2,000 wakati kusimamisha malipo kwa cheki iliyokwishaandikwa na kuwasilishwa  ni asilimia 1 na kiwango cha juu ni Sh 150,000, wakati kwenye benki hiyo hiyo moja ni asilimia 1 kima cha chini  50,000 na cha juu ni Sh 300,000 kama tozo.

Benki inatoza gharama kwa kuweka maagizo ya kudumu ndani ya benki moja (Standing orders within the same bank) tozo ni  asilimia 1  ya thamani kwa kiwango kidogo cha tozo ya Sh 50,000 au kiwango cha  juu kisichozidi  300,000,  wakati kwa benki nyinginezo maagizo ni Sh  4,000 na kushughulikia mishara ni  Sh 50,000.



Katika kauli yake hiyo, Dk Charle Kimei alinukuu kukua kwa kipato cha CRDB Group kwa  asilimia 22 na miundombinu madhubuti kwenye mtandao kuwezesha benki kwa uwakala  (agent banking ) kwa chapa ya Fahari Huduma kufikia mawakala  zaidi ya 2500, matawi 250 na ATM 478, ikiwa ni pamoja na uwepo wa huduma ya kidijitali ya SimBanking pamoja na ile ya  Intetaneti.



Wadadisi wanadai kuwa CRDB ina wafanyakazi wengi kupita inavyowahitaji na ingekuwa bora kwake kupunguza wengine  ili  isonge mbele.

Dk Kimei anadai benki yake ina mizania nzuri ya mali ya Sh trilioni 5.4 na amana za trilioni 4.1 kufikia mwishoni mwa robo ya tatu mwaka jana ambazo hakuna wa kuzifikia lakini cha kushangaza ni gharama zake kwa wateja kuwa kubwa na kama vile kuna ukimbizi fulani.

Maono yake ni biashara iliyostawi ya benki na fedha nchini.

Post a Comment

 
Top