0
Mnamsahau Vipi Mchizi Roma....!!

Na Malle Hanzi
©2017
____________

Tukiwa bado tunajiuliza kama taifa ni wapi alipo Ben Saa nane. Miezi kadhaa ikiwa imepita tangu alipotoweka mwishoni mwa mwaka jana. Mpaka leo hakuna habari kamili juu ya kupotea kwake. Si chama chake, marafiki zake wala ndugu zake wenye taarifa za wapi alipo Ben Saanane. Wananchi wamebaki kutegemea taarifa kutoka katika vyombo vya dola lakini mpaka leo hata serikali haijasema wapi Ben alipo.? Ikumbukwe mpaka dakika ya mwisho Ben anapotea alikuwa akihoji uhalali wa PHD ya kiongozi mkubwa.

Tukiwa tunaendelea kuuliza wapi Ben Alipo. Tunapata habari kuna miili ya watu imeokotwa mto ruvu. Mamlaka zinatueleza ni miili ya wahamiaji haramu. Tunabaki kujiuliza wahamiaji haramu ndio wanapaswa kuuawa na kisa kuwekwa katika mifuko ya sandarusi na kutupwa katika mto ruvu. Mto ambao unatupatia maji safi wakazi wa Dar es salaam na mkoa wa pwani.

Ni wakati huu huu tukiwa tunaendelea kushuhudia upindishwaji wa taaluma ya habari na usumbufu mbalimbali unaowapata waandishi wa habari hasa waandishi wa habari za kiuchunguzi. Tusisahau mwezi wa 12 mwaka jana mwandishi wa habari wa ITV alikamatwa na polisi walioagizwa na DC kwa kosa linalodaiwa kuripoti habari inayohusiana na ukosefu wa maji kwa wananchi wa wilaya hiyo.

Tusisahau pia tuhuma za mkuu wa mkoa kuvamiwa ofisi za clouds mwezi uliopita na akiwa watu wanaosemekana ni polisi wakiongozwa na mkuu huyo wa mkoa kufanya kile kinachotajwa kushinikiza kurushwa kwa kipindi kinachomhusu Askofu Gwajima. Unapotaka kujiuliza ulipo uhuru wa vyombo vya habari tafadhali rejea kauli hii inayosema "mnahisi mna uhuru wa kujieleza but not to that extent".

Wakati tukizidi kujiuliza maswali anatokea msanii aitwaye Nikki Mbishi anamuomba msamaha Raisi Aliyepita katika kibao chake kiitwacho "Im sorry JK". Anaelezea kwamba bora uongozi wake kuliko huu wa sasa. Watu wenye mamlaka zao wanamuita na kumtaka awatangazie mashabiki wake kwamba kibao chake kimefungiwa na hakiruhusiwi kusambazwa na kweli akafanya hivyo huku akionya kwamba hatahusika na yeyote atayekamatwa akisambaza wimbo huo. Ukimya unaigubika sanaa na wasanii wanaanza kuhisi mambo ya siasa na mustakabali wa taifa hayawahusu.

Anatokea msanii mwingine aitwaye Ney wa Mitego anatoa kibao kiitwacho Wapo ambacho kimeelezea moja kwa moja bila kuficha madhaifu mbalimbali yaliyo katika jamii. Katika sanaa ilifika wakati alitakiwa atokee mtu ambaye atasema wazi bila kuficha ficha kuhusu mambo yanayoendelea katika jamii. Wasanii wengi walikuwa wameshaingia woga wa ku-vunja ukimya. Ney aliibuka kama Ice Breaker. Na hii imewapa wasanii wengine confidence ya kuanza kukemea.

Mara tukasikia wimbo wake umefungiwa sababu ya uchochezi. Hatujakaa vizuri akakamatwa na kusafirishwa kutoka morogoro to Dar na kufikishwa central kwa mahojiano. Mara Likatoka tamko kutoka ikulu jamaa aachiwe wimbo wake uko poa tu ni mzuri na mkuu akataka amuongezee mambo ya kuimba. Wakati huo huo waziri mwenye dhamana akatoa tamko la kuufungulia wimbo uendelee kuchezwa.

Haya yalikuwa maajabu. Nikabaki kujiuliza hivi kati ya Basata na Mwakiembe nani mwenye ujuzi na mambo ya sanaa.? Kati ya Im Sorry JK na Wapo upi ni wimbo wa unaokosoa wazi wazi? Anayeweza kujua msanii amefanya kosa la kichochezi ni Ikulu au Mahakama? Kama Taifa bado tuna safari ndefu sana ya Maendeleo.

Kinachonisikitisha zaidi ni hizi taarifa zilizoanza kusambaa juzi kwamba msanii Roma, Moni, Prodyuza Belo bin Laden na Kijana wa usafi katika studio za Tongwe zilizopo masaki kukamatwa na watu wasiojulikana baada ya kuvamia studio hizo juzi. Taarifa hizi zimethibitishwa na Mmiliki wa studio hizo bwana J Murder na mke wa Roma. Mpaka leo hii watu hao hawajulikani walipo na polisi hawana taarifa yoyote juu ya watu hao kwa mujibu wa mke wa Roma.

Kiukweli itafikia wakati katika taifa watu/mtu anapotea na watu watakuwa hawashtuki kabisa kama jitihada za makusudi hazitafanyika kukomesha hii hali. Serikali yetu imeendelea kuwa kimya katika masuala haya. Simsikii waziri mwenye dhamana akitupa way forwad wapi alipo Ben na sasa wapi alipo Roma na wenzake. Kama naziona familia za hawa watu zinavyopitia katika kipindi kigumu kwa sasa. Kwakweli mwenyezi mungu awatie nguvu.

Mheshimiwa Mkuu wa mkoa ukiwa kama mlezi wa wasanii na mwenyekiti wa ulinzi na usalama wa mkoa nimekusikia ukiwa na wasanii mkizungumzia kuhusu maharamia wanaoiba kazi za wasanii. Sijakusikia ukizungumzia kuhusu wasanii wako walioko katika mkoa wako waliopotea katika mazingira tatanishi juzi katika viunga vya masaki. Tunataka serikali ioneshe nia ya dhati katika upatikanaji wa watu hawa.

MALLE HANZI
Kinachokera zaidi ni wasanii kutokuwa wamoja katika hili. Hawa wanaoumia kuhusu kupotea kwa Roma na wenzie wengine wako na viongozi wa serikali wakitangaza vitu visivyo na priority kulingana na nyakati husika. Hivi uhai wa Roma na wenzie unaweza kurudishwa vipi kama ukipotea. Hivi mnadhani kwa sababu Roma ni rapper na nyinyi ni waigizaji au wachonga vinyago n.k kwa hiyo hawahusu. Wote ni wanasanaa mzani wenu ni mmoja licha ya tofauti zenu.

Wakati Ben Saanane alipopotea kuna Gazeti moja lilitoa habari kwamba Ben hajapotea ila amejipoteza ili apate kiki. Vivyo hivyo kuna baadhi ya wasanii nawaona mitandaoni wakisema kuwa na Roma na wenzie wanatafuta kiki pia hawajapotea wala nini. Hivi unawezaje kutafuta kiki ya namna hii kwenye Era ya Magu. Hivi mna akili timamu kweli.

Huko nyuma nimewahi na wengine pia wamewahi kumkosoa Roma hasa kwenye upangaji wa vina vya Hip Hop mpaka alipobadilika. Though baadhi ya watu wanamchukulia sio Hip Hop lakini hii haiwafanyi muone sio muhimu kupaza sauti zenu kuhusu hili linalomkumba. Ukiacha utofauti wa mifumo ya muziki au mifumo ya sanaa bado serikali inawatambua kama wanasanaa kwa pamoja. Msipojisimamia kwa sauti moja hakuna atakayekuja kusimama na nyinyi.

Leo imemtokea Roma na wenzie Kesho itakuwa zamu yako. Ukiwaruhusu leo wampoteze Roma kimchezo mchezo namna hii kesho na wewe utapotezwa kimasihara masihara hivi hivi. Siamini kama huu ndio mwisho wa Roma na Wenzie. I Hope watarudi Kujumuika na ndugu, marafiki na familia zao.

Kesho Itakuwa Zamu Yako. Kwenye Maombi na Sala zako Tafadhali usimsahau mchizi Roma na wenzie. Nauskiza huu wimbo wao uitwao "Msimsahau Mchizi" wa Roma na Moni ukitayarishwa na Bello alafu leo wote walioshiriki wamepotea nahisi kama walijitabiria yanayowatokea leo. May God Protect Them. Amen.
#Justice4Roma
#Justice4Moni
#Justice4Bello
#Justice4Ben

Post a Comment

 
Top