0
UGOMVI wa kugombea chakula kati ya mfanyakazi wa ndani, Mary Simon (16) na watoto wa mwenye nyumba umesababisha binti huyo kujinyonga.


Tukio hilo la aina yake lilitokea juzi saa 9 jioni katika Kata ya Olasiti iliyopo Halmashauri ya Jiji la Arusha.


Akizungumza ofisini kwake mjini hapa jana Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo alithibitisha kutokea kwa kifo cha binti huyo.

Akifafanua mazingira ya kifo hicho Kamanda Mkumbo alisema, Novemba 2, Mwaka huu majira ya saa 7 mchana Mary alikuwa akila chakula cha mchana na watoto wa mwenye nyumba.

Alidai kwamba wakiwa wanaendelea kula binti huyo aliwaeleza watoto hao kuwa ameshiba, hivyo asingeweza kuendelea kula.

“Baada ya Mary kudai kuwa ametosheka na chakula, alimfuata mmoja wa watoto hao Julius Thomas na kumpiga kichwani.

“Hata hivyo baada ya kuulizwa kwanini amefanya hivyo Mary alijibu “samahani”, ndipo Julius naye aliamua kumrudishia kwa kumpiga kofi,” alisema Kamanda Mkumbo.

Alisema baada ya mvutano huo binti huyo aliingia chumbani, kisha akajifungia mlango, ambapo baadaye simu yake ya mkononi ilianza kuita.

“Mtoto mmoja Enoth Frank alichukua simu ile kwa ajili ya kumpelekea hata hivyo alikuta mlango ukiwa umefungwa na aliamua kuzungukia dirishani.

“Alipochungulia kwa ndani alimwona Mary  akiwa amening’inia kwenye kabati la nguo kwa kutumia mtandio,”alisema Kamanda Mkumbo.

Kamanda huyo alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Mount Meru kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Post a Comment

 
Top