0
KUNDI la wataalamu wa afya kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, limewasili wilayani Ngorongoro mkoani Arusha katika Kata ya Pinyinyi, kuchunguza ugonjwa wa kutapika damu ulioua watu 21.


Kuwasili wa wataalamu hao, kumethibitishwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo na Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Omari Sukari. Gambo alilieleza gazeti hili kuwa timu hiyo iliwasili kijijini Pinyinyi wiki iliyopita.


Alisema hajui timu hiyo itakaa siku ngapi kijijini humo kuchunguza ugonjwa huo, lakini anachojua imeshawasili na imeshaanza kufanya kazi kwa kuwatafuta wale waliougua na wanaogua ugonjwa huo wa ajabu. Alisema baada ya kukamilisha uchunguzi wao na kupima kila mwananchi aliyepatwa ugonjwa huo na kupona, watatoa taarifa rasmi.

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Sukari alikiri kufika kwa timu hiyo, lakini hakuwa tayari kusema chochote kwani yeye sio msemaji wa kundi hilo la wataalamu.

Kujulikana kwa ugonjwa huo, kulitokana na ziara ya Gambo katika kijiji hicho na Mtendaji wa kata hiyo, James Mushi katika risala yake alieleza jinsi ugonjwa huo unavyoua wananchi.

Post a Comment

 
Top