0
Tatizo la madawa ya kulevya limetokea kuwa janga kubwa duniani kote, watu wengi wameathirika na janga hili. jinsia zote wanaume, wanawake, na vilevile rika zote vijana na wazee pia. 



Hapa tutaongelea aina mbili za madawa ya kulevya yaani Cocaine na Heroin.




Cocaine 

Hutokana na majani ya mmea uitwao kitaalamu Erythroxylum coca bush. 



Aina hii ya dawa ya kulevya hutolewa kwa mifumo ifuatayo;


Unga ambapo mitaani hujulikana kama ‘coke’ na hutumika kwa kuvutwa puani kama unga, au kuyeyushwa na maji na kuchomwa kwenye mshipa wa damu.


Crack ambapo mitaani hujulikana kwa jina hilohilo crack au rock, na hutengenezwa kwa kuchanganywa na kemikali. Na hutumika kwa kuvutwa kama sigara.


Cocaine pindi inapoingia kwenye damu huenda kwenye ubongo na kuzuia ufyonzwaji wa vihisishi vifuatavyo: dopamine, norepinephrine na serotonin, kutoka kwenye ubongo. Hivyo ubakia kwenye ubongo. Na vihisishi hivi husababisha ile hali ya furaha, mchangamfu na kujisikia mwenye nguvu kitaalamu euphoria. Na huweza kuwa kwenye hali hii kwa nusu saa tu.


Mara tu baada kutumia dawa hii dalili zifuatazo hutokea



  • Mishipa ya damu husinyaa (constricted blood vessels)
  • Joto la mwili huongezeka
  • Mapigo ya moyo huongezeka
  • Shinikizo la damu
  • Dilated pupils


Matumizi ya muda mrefu ya dawa hii ya kulevya huleta madhara yafuatayo;


Pamoja na kwenda kwenye ubongo husambaa sehemu nyingine za mwili na mzunguko wa damu


Moyo - Kwenye moyo huweza kuleta Shambulizi la moyo (heart attack) na vilevile mapigo ya moyo yasiyo na mpangilio (Arrhythmia) hivyo unaweza kufa ghafla tu.


Ubongo - Mishipa ya damu kwenye ubongo inaweza kusinyaa na kupelekea kupata Kiharusi, hata kwa kijana. Vilevile unaweza kupata ugonjwa wa akili (substance abuse pyschosis).


Mapafu na mfumo wa hewa - Uvutaji kupitia pua huweza kupelekea tatizo sugu la kutokwa damu puani kila wakati na mafua yasiyo pona, kupoteza mfumo wa harufu, na ikivutwa kama sigara kuharibu mapafu moja kwa moja.


Mfumo wa chakula - Cocaine husababisha kusinyaa kwa mishipa ya damu kwenye tumbo na utumbo hivyo kusababisha vidonda na kuweza kuharibu kabisa mfumo huu kwa utumbo kuoza.


Mafigo - kutokana na shinikizo la damu mafigo yanaweza kushindwa kufanya kazi vizuri, vilevile cocaine inaweza kuleta madahara moja kwa moja kwenye mafigo kitaalamu Rhabdomyolysis.


Ngono - ingawa cocaine huweza kutumika kama njia ya kuongeza hamu ya ngono huweza kusababisha kushindwa kumaliza kile ulichokianza.


Matumizi sugu ya dawa hii ya kulevya huleta madhara kwa jinsia zote yani kwa wanaume na wanawake.

Kabla na Baada ya Athari

Na vilevile huweza kufanya kuwa tegemezi wa dawa hii.


Kwa wanaotumia sindano na kushea wanaweza kupata maambukizi ya virusi ya hepatitis na vya ukimwi.


Nini hutokea baada ya matumizi ya muda mrefu ya kokeni?


Baada ya kutumia cocaine kwa muda mrefu punde unapoacha tu kutumia dalili zifuatazo hutokea;



  • Unyogovu
  • Uchovu
  • Kushindwa kuzingatia na kutokuwa makini
  • Kukosa uwezo wa kuwa na furaha au kusikia raha
  • Kuongezeka kwa tama zaidi ya kutumia cocaine
  • Kujisikia kuumwa, maumivu, baridi na kutetemeka.


Ikitokea mtu akitumia zaidi ya kiwango kinachotakiwa kwa muda mfupi yaani overdose, kifo cha ghafla huweza kutokea kutokana na madhara yafuatayo;



  • Moyo kushindwa kufanya kazi
  • Kiharusi
  • Degedege mara kwa mara
  • Mfumo wa hewa kushindwa kufanya kazi


Heroin

Hujulikana vilevile kama diamorphine, hutokana na mmea huitwao kitaalamu opium poppy. Heroin kwa mfumo wa Morphine hutumiwa hospitalini kama dawa ya maumivu makali ya ghafla (acute pain) kwenye maumivu makali ya kifua wakati wa shambulizi la moyo, na kwa maumivu ya mtu aliyepata ajali, vilevile baada ya upasuaji, na maumivu sugu kwenye kansa. Hivyo hutolewa kwa kuangalifu mkubwa.



Aina hii ya dawa ya kulevya huweza kutumika kwa kuvuta kwa pua, kuvuta kama sigara na kwa kuchoma kwenye mshipa. Siku hizi watu hutumia njia ya haja kubwa na kwenye uke, ambapo kuta hufyonza heroin na kuanza kufanya kazi ndani ya sekunde arobaini.


Heroin mara tu baada ya kuingia kwenye damu kuenda kwenye mfumo wa neva na kukandamiza ufanyaji kazi wake, ndio huweza kutumika kupunguza maumivu.



Dalili za mtu aliyetumia heroin


Dalili ambazo hutokea mara tu anapotumia Heroin:



  • Kujisikia mwenye furaha na raha
  • Kupishana Kusikia hali usingizi na tahadhari
  • Midomo kuwa mikavu
  • Misuli kuishiwa nguvu
  • Kuhema polepole
  • Warm skin flushing
  • Mikono na miguu kuwa mizito
  • kope za macho kulegea


Nini madhara ya matumizi ya muda mrefu ya heroin?


Madhara ya matumizi ya muda mrefu wa dawa hii ya kulevya hutokana zaidi na matumizi ya sindano na vifaa vingine visivyo salama



  • Maambukizi kwenye kuta na milango ya moyo
  • Maambukizi ya ini na virusi (kama hepatitis C na HIV),
  • Maambukizi ya figo
  • Maambukizi ya mfumo wa hewa
  • Maambukizi ya ngozi na majipu



Dalili ambazo hutokea mara tu unapoacha kutumia heroin;



  • Kutotulia
  • Maumivu ya misuli na mifupa
  • Kutapika


Dalili hizi hufikia kilele ndani ya masaa 48 hadi 72 na hufika kikomo baada ya wiki.


ATHARI ZA MATUMIZI YA DAWA ZA KULEVYA


Matumizi na biashara ya dawa za kulevya yameendelea kusababisha madhara makubwa mbalimbali nchini yakiwemo ya kiafya, kijamii, kiuchumi, kimazingira, kisiasa na kiusalama.


KIAFYA:

Dawa za kulevya zimeendelea kuleta madhara makubwa kiafya yakiwemo magonjwa ya akili, utegemezi wa dawa za kulevya, magonjwa ya mapafu, moyo, ini na figo. Aidha, matumizi ya dawa za kulevya yaliendelea kusababisha vifo vya ghafl a hasa miongoni mwa wajidunga kutokana kuzidisha dozi. Pia, matumizi ya dawa hizo yameendelea kuchangia kuenea kwa maambukizi ya VVU, kifua kikuu na virusi vya homa ya ini aina ya B na C. Watumiaji wengi wameendelea kukabiliwa na magonjwa ya meno na ngozi yakiwemo majipu, vidonda na ukurutu. Dawa za kulevya zimeendelea kusababisha kupungua kwa nguvu za kiume, ugumba, utasa na kuzaliwa kwa watoto wenye ulemavu, njiti na wenye matatizo ya ukuaji wa kiakili na kimwili. Jedwali Na.8 linaonesha viwango vya maambukizi ya magonjwa mbalimbali kwa watumiaji waliojitokeza kupata matibabu kwenye hospitali za Muhimbili.

KICHUMI:

Matumizi ya dawa za kulevya huongeza mzigo kwa taifa kwa kuwa hupunguza nguvu kazi na husababisha uharibifu wa mali. Vilevile, gharama za udhibiti zikiwemo utoaji wa elimu kwa umma, uteketezaji wa mashamba ya bangi, uendeshaji wa kesi, kuwatunza wafungwa magerezani na kuwatibu watumiaji huongeza mzigo kwa taifa na jamii kwa ujumla.

Biashara ya dawa za kulevya husababisha mfumuko wa bei unaotokana na fedha za biashara hiyo kuingizwa kwenye mfumo halali. Aidha, matumizi ya dawa zakulevya husababisha utoro mashuleni au kazini, kusitisha masomo au kufukuzwa kazi. Kwa ujumla, matumizi na biashara ya dawa za kulevya vimeendelea kuchangia kuongeza umaskini nchini.


KIJAMII:

Dawa za kulevya zimeendelea kusababisha mmomonyoko wa maadili katika jamii. Utumiaji na biashara ya dawa za kulevya mitaani husababisha tabia hiyo kuzoeleka na hivyo kuwavutia watu wengine hasa watoto kujiingiza kwenye tatizo hilo na kuchangia kuharibika kwa kizazi kijacho.Aidha, matumizi ya dawa ya hizo huchangia migogoro ya kifamilia katika jamii jambo linaloweza kuzisambaratisha kabisa. Wazazi ambao hutumia dawa za kulevya, huonesha mfano mbaya kwa watoto wao na jamii kwa ujumla. Pia, kumekuwepo na ajali zilizosababishwa na uendeshaji wa magari na mashine huku waendesha vyombo hivyo wakiwa wametumia dawa za kulevya. Ajali hizo mara kwa mara zimekuwa zikisababisha ulemavu na vifo vingi. Wajidunga hutupa ovyo mabomba ambayo huweza kusababisha majeraha kwa wapita njia au maambukizi ya magonjwa mbalimbali.

Watumiaji wamekuwa wakijihusisha na tabia na vitendo viovu vikiwemo wizi, uporaji, biashara ya ngono na ubakaji. Jamii imekuwa ikiamini kuwa matumizi ya dawa za kulevya ni jambo la kujitakia, hivyo kuwanyanyapaa na kuwabagua watumiaji. Vitendo na muonekano wao huwafanya wasikubalike katika jamii jambo linalosababisha kuendeleza vitendo vyao vya uhalifu na utumiaji wa dawa za kulevya. Halikadhalika, kosa la kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya huambatana na adhabu kali ikiwemo kifungo cha maisha jambo ambalo linawatenga wahusika na familia zao pamoja na jamii. Biashara ya dawa za kulevya huhusisha rushwa kubwa ambayo huathiri utoaji haki kwa wananchi na utawala bora. Wafanyabishara wa dawa za kulevya hutumia sehemu ya faida wanayopata kusaidia jamii ambayo huwaonea aibu kuwachukulia hatua pindi wanapojihusisha na vitendo viovu.


Wafanyabiashara hujitumbukiza kwenye vitendo vya kihalifu kama utekaji nyara, ugaidi, mauaji ya kikatili, vita vya wenyewe kwa wenyewe na ujambazi, hivyo kusababisha uvunjifu wa amani. Vilevile, wafanyabiashara wa dawa za kulevya huweza kuwarubuni watendaji wa vyombo vya udhibiti wa dawa za kulevya kuvujisha siri hivyo kuhatarisha maisha ya watendaji na raia wema.


KISIASA:

Wafanyabiashara wa dawa za kulevya huweza kuwashawishi wapiga kura kwa kutumia rushwa kuwachagua viongozi watakaosimamia maslahi yao pindi watakapokuwa madarakani. Biashara ya dawa za kulevya huweza kuchochea machafuko ya kisiasa na kuweza kupindua serikali iliyopo madarakani. Halikadhalika, nchi inayojihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya huharibu taswira ya nchikimataifa na kusababisha madhara mbalimbali ikiwemo raia wake kutoaminika na kupata usumbufu mkubwa wanapokuwa kwenye nchi nyingine.

KIMAZINGIRA:

Kilimo cha bangi kinachofanyika kwenye vyanzo vya maji na kwenye ardhi oevu husababisha kukauka kwa mito na kuleta ukame. Pia, ukataji miti ovyo na uchomaji moto wa misitu kwa ajili ya kuandaa mashamba ya bangi husababisha mmomonyoko wa udongo.

Kila ifikapo tarehe 26 mwezi wa 6 kila mwaka,hua ni siku ya kupiga vita matumizi ya dawa za kulevya duniani.




Nikushukuru ndugu mpekuzi wa DAKIKA ZA MADINI kwa kuungana nami mwanzo mpaka mwisho wa Makala hii, usikose kufatilia makala nyingi za kuelimisha kwa kubofya kipengele cha MADINI. Ulikuwa nami BIN'OTTO THE'OTTONATURE, nikwambie tu, DAKIKA ZA MADINI ndio sehem sahihi ya wewe kupata ujuzi, nasi tuko nawe mpaka ufanikiwe. Kama una tatizo, maoni au ushauri, tuandikie kupitia dakikazamadini@gmail.com



Post a Comment

 
Top