Mwenyekiti wa kamati hiyo, Jasson Rweikiza alitoa ushauri huo jana mjini hapa kwenye kikao kati ya wajumbe wa kamati hiyo na viongozi na watendaji wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa wakiongozwa na Naibu Waziri, Selemani Jafo.
Kikao hicho kilikuwa ni cha kamati kupokea na kujadili taarifa ya tathmini ya utekelezaji wa mpango wa ofisi hiyo wa utoaji elimu bila malipo katika kipindi cha Januari hadi Juni mwaka huu ambako suala la uhaba wa walimu liliibuliwa na wajumbe.
“Walimu waajiriwe...ni vyema mumuone rais, angalau afungulie kibali cha walimu pekee...wanafunzi wanaongezeka mara mbili, lakini walimu hakuna,” alisema Rweikiza.
Awali, akijibu hoja za wajumbe juu ya changamoto ya uhaba wa walimu, hususan wa Sayansi na Hisabati, Jafo alikiri hali hiyo kuikumba serikali na kusema ndiyo maana walilenga kutoa ajira 35,000 kabla ya rais kusimamisha vibali vya ajira kwa watumishi wote.
Hata hivyo, alisema uamuzi wa Rais ni wa nia njema kuwezesha uhakiki wa watumishi hewa.
Alisema katika kauli ya hivi karibuni ya Rais John Magufuli, alisema wakati wowote kibali kitatolewa.
Jafo alisisitiza kuwa kibali kitakapotolewa, kipaumbele itakuwa ni ajira kwa walimu wa Sayansi ya Hisabati.
Akielezea namna ya kuziba mapengo ya walimu wa masomo hayo, Jafo alisema serikali itafikiria pia watu wengine wanaoweza kufaa katika kufundisha masomo hayo wakiwemo walimu wastaafu na wahitimu wa fani nyingine.
Post a Comment