0
KUUAWA kwa aliyekuwa Kamanda wa Kikosi Maalum cha Kupambana na Uhalifu, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Thomas Muniko anayedaiwa kupigwa risasi na majambazi eneo la Vikindu, Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani kumeibua maswali magumu kuhusu mazingira halisi ya kifo chake.

Kifo hicho kimetokea mwezi mmoja baada ya kuhamishiwa Kanda Maalum ya Dar es Salaam akitokea Mirerani, wilayani Simajiro, Mkoa wa Manyara alikokuwa akiongoza kikosi cha kupambana na ujangili.


Kachero huyo ambaye aliaminika zaidi kwa utendaji wa kazi, katika tukio la juzi, alikuwa  akiongoza kikosi kazi kilichotumwa Vikindu kusaka majambazi walioua  polisi wanne waliokuwa wakilinda   Benki ya CRDB, tawi la Mbande,   Mbagala, jijini Dar es Salaam.

Taarifa mbalimbali zilizokusanywa na timu ya MTANZANIA kutoka Vikindu mkoani Pwani na vyanzo vingine, zinazidi kuzua maswali yenye utata.

Maswali hayo ni  hususan eneo alilokuwa jambazi anayedaiwa kutekeleza unyama huo na baadaye kutoroka bila kukamatwa na polisi waliokuwa wamejiandaa kukabiliana na wahalifu hao.

Chanzo chetu kutoka moja ya taasisi nyeti nchini, kiliiambia MTANZANIA kuwa huenda Muniko aliuawa na wenzake kwa bahati mbaya wakati akiwaongoza wapiganaji wake kushambulia nyumba hiyo iliyodhaniwa kuwa na majambazi.

Chanzo hicho kilidai kuwa  hadi polisi wanaanza kuizingira   na hatimaye kuanza mapambano ya risasi   eneo lote linalozunguka nyumba hiyo lilikuwa  mikononi mwa  askari hao.

Kwa maana hiyo, hata kama jambazi angefanikiwa kutekeleza mauaji hayo, asingeweza  kutoroka kwa urahisi kama inavyoelezwa.

Chanzo hicho kilisema  katika tukio hilo la mwishoni wiki lililosababisha nyumba hiyo kuchakazwa kwa risasi zisizo na idadi, hakukuwa na majibizano yoyote kutoka upande wa pili kama inavyoelezwa.

Chanzo hicho kilinukuliwa kikisema ‘no any fire exchange’ (hakukuwapo na majibizano yoyote ya risasi) na kwamba  risasi zote zilizopigwa zilikuwa za upande mmoja.

“Katika ‘tention’ kama ile, kuumia na hata kuuawa kwa makosa si jambo la ajabu, maana ile ilikuwa kama vita. Jiulize mpaka askari wanapoamua kuzingira mahali kama pale maana yake wamekwisha kujihakikishia ulinzi wa kutosha.

“Sasa basi, kwa mazingira hayo kama jambazi aliweza kutekeleza mauaji tena kwa kiongozi wa mapambano na hatimaye kutoroka, basi zinahitajika juhudi na mabadiliko makubwa katika Jeshi la Polisi,” kilisema chanzo hicho.

Shuhuda ambaye anaishi eneo ilipo nyumba iliyodhaniwa kuhifadhi majambazi, Omar Seif, alisema alisikia milio ya risasi na alipojaribu kutoka nje ya nyumba yake, aliwaona askari wamelala chini na kumtaka arudi ndani haraka.

“Nikiwa ndani, risasi za rasharabsha ziliendelea, nikiwa tayari nimeingiwa na hofu, nilisikia kwa nje mtu kama anajikokota au anakokotwa nilipochungulia dirishani ndipo nikamuona askari amelala chali pale kwenye mti wa mwembe huku akitoa sauti ya kuugulia maumivu makali na pembeni akiwapo askari mwingine mmoja,” alisema Seif.

Taarifa zilizopatikana kutoka kwa watu waliokuwa karibu na kachero huyo aliyeuawa, zilisema  tangu ahamishiwe Dar es Salaam, alikuwa akiishi hotelini.

Utata kuagwa mwili wa Muniko

Wakati hali ikiwa hivyo, mwili wa marehemu Muniko uliagwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) jana asubuhi huku kukiwa na hali ya usiri tofauti na ilivyofanyika kwa askari wanne waliouawa wiki iliyopita wakiwa lindoni Benki ya CRDB, Mbande, Mbagala.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Huduma kwa Wateja wa Hospitali ya Muhimbili, Aminiel Eligaesha, alipopigiwa simu kueleza jinsi mwili wa marehemu unavyoagwa, alisema yupo likizo na hata wasaidizi wake walipopigiwa hawakupokea simu.

Hata hivyo, mmoja wa wahudumu wa chumba cha kuhifadhi maiti hospitalini hapo ambaye hakutaka jina lake litajwe, aliiambia MTANZANIA kuwa mwili wa marehemu Muniko ulichukuliwa na kuagwa mapema jana saa mbili asubuhi na hakukuwa na taratibu zozote za jeshi kama ilivyofanyika kwa askari wanne ambao waliagwa juzi katika Viwanja vya Barabara ya Kilwa, Dar es Salaam.

Wasemaji wa polisi

Kamanda wa Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro alipopigiwa simu, simu zake ziliita bila kupokelewa ingawa siku mbili zilizopita aliahidi kutoa taarifa rasmi za tukio hilo kwa maana ya juzi au jana.

Hata  Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Ernest Mangu azungumzie suala hilo, alikataa na kumtaka mwandishi wetu amtafute Kamanda Sirro.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba akizungumzia mauaji ya askari huyo, alisema si kweli kwamba aliuawa na wenzake kwa habati mbaya.

Alisema habari hizo ni za uongo na uzushi unaosambazwa na watu wasiolitakia mema Taifa.

“Jambo hili halina ukweli wowote kwa sababu askari yeyote anapokuwa front line (mstari wa mbele), huwa wana ‘signal’ (alama) zao ambazo zinawaongoza.

“Hajapigwa kwa bahati mbaya na wenzake…ifike hatua Watanzania waache tabia ya kuzusha uongo.

“Ila kama kuna mtu yeyote alishuhudia tukio hilo usiku wa manane ni bora akajitokeza kutoa ushahidi  kulisaidia Jeshi la Polisi.

“Kama usiku ule wa manane kulikuwa na mtu anashuhudia hayo wanayosema, namuomba ajitokeze atusaidie ushahidi katika jambo hili,”alisema Waziri Mwigulu.

Alipoulizwa kwa nini Serikali haijatoa kauli yoyote kuhusu mauaji ya Muniko na watu waliokamatwa, alisema kila jambo linafanyika kwa utaratibu wake.

“Nakuhakikishia kwamba Serikali haijawa nzito kuzungumzia tukio hili, natambua Watanzania wengi wana shauku ya kutaka kujua kilichotokea.

“Operesheni  inaendelea si vizuri kutoa taarifa ambazo zinaweza kumpa mwanya adui,”alisema.

Kuhusu kuagwa kwa mwili wa marehemu Muniko kimyakimya, alisema si jambo geni kufanywa hivyo, kwa sababu  taratibu zote za jeshi zilifuatwa.

“Unajua ndugu yangu katika kuaga mwili kuna taratibu za jeshi na sisi Watanzania na waafrika tuna mila na desturi zinazotuongoza.

“Ndiyo maana hata siku ile pale Barracks, Kilwa Road, tuliaga miili mitatu kati ya minne ya askari wetu waliouawa eneo la Mbande,” alisema.

Kuhusu hali ya usalama kwa ujumla, alisema imedhibitiwa vya kutosha na kuwataka wananchi kuendelea na majukumu yao kama kawaida.

Mwili wa Muniko ulitarajiwa kuagwa katika makazi yake   eneo la Magugu, Mirerani na baadaye kusafirishwa kwenda nyumbani kwao  mkoani Mara, kwa ajili ya mazishi.

Post a Comment

 
Top