0
Habari rafiki?
Naamini uko vizuri sana na unaendelea kuweka juhudi kubwa kwenye maisha yako na kwenye kile unachofanya ili uweze kupata matokeo bora yatakayokuletea mafanikio. Nikukumbushe tu ya kwamba kila kitu unachotaka kwenye maisha yako, kinaanza na wewe mwenyewe, hivyo kama kuna mahali unataka kufika, ni lazima uamue wewe mwenyewe na uweke juhudi ili kufika pale.
Karibu kwenye mazungumzo yetu ya leo rafiki yangu ambapo mimi na wewe tunakwenda kushirikishana mambo muhimu kuhusu maisha ili tuweze kufanya maamuzi sahihi kwenye maisha yetu. Maisha ni mchezo ambao una vitu vingi sana, na kama ilivyo kwenye mchezo wowote unahitaji kuzijua sheria za mchezo ili kuweza kuucheza vizuri na kupata matokeo mazuri. Maisha nayo yana sheria zake ambazo ni muhimu kuzizingatia ili kuweza kupata matokeo bora. Tatizo ni kwamba hatupati kufundishwa sheria hizi moja kwa moja na badala yake tunajifunza wenyewe baada ya kufanya makosa.



Leo tunakwenda kuangalia eneo moja, na eneo hili ni la kurubuniwa au kudanganywa. Unarubuniwa pale ambapo unashawishiwa kufanya kitu ambacho huenda siyo bora kwako lakini unalazimika kufanya. Jamii zetu zimejaa watu ambao wanaturubuni kila wakati, na sisi kwa kutokujua tumekuwa tunafanya yale tunayorubuniwa kufanya japo hayana faida yoyote kwetu. Na kitu kinachotumika kuwarubuni watu ni HOFU.

Nilijifunza mbinu hii ya urubuni kupitia watoto, mara kwa mara nimekuwa nikiwaangalia watoto hasa wanapocheza, aina ya tabia ambazo wanaonesha baina yao wenyewe, pale wanapokuwa huru na wanajua hakuna mtu anayewafuatilia. Kuna kitu kimoja cha kushangaza sana nimekuwa nakiona. Kwa mfano kama watoto wanacheza, halafu mmoja akawa anataka kitu kutoka kwa mwenzake na yule mwenzake akakataa, basi yule mtoto aliyekuwa anataka kitu anatumia kauli moja, SICHEZI NA WEWE, kwa kusikia kauli hii yule ambaye amekataa anakubali haraka sana.

Ni jambo la kushangaza sana kwani hata mtoto ambaye ni mkorofi kiasi gani, akiambiwa na wenzake kauli hiyo ya SICHEZI NA WEWE analainika na kufanya kile ambacho mwenzake au wenzake wanamtaka afanye.

Hata wakubwa wanakataa kucheza na wewe.
Unaweza kuona hilo ni sawa kwa watoto, kwamba ni watoto tu wanacheza na hawajui kile wanachokifanya. Lakini ukweli ni kwamba wanajua vizuri sana na ndiyo maana wanatumia mbinu hiyo. Hata sisi watu wazima tumekuwa tunatumia mbinu hii kuwarubuni wengine, na umekuwa unarubuniwa sana kwa mbinu hiyo.

Kwa kuwa wewe ni mtu mzima, hutaambiwa SICHEZI NA WEWE, badala yake utaambiwa UNATENGWA, au UTAKUWA MPWEKE na kauli nyingine zinazoendana na hizo.

Tumekuwa tunavutiwa sana na kuwa ndani ya jamii fulani, na hivyo tumekuwa tayari kufanya mambo ambayo hayana faida kwetu ili tu tuendelee kuwa kwenye jamii hizo. Na hapa ndipo nguvu hiyo ya kurubuniwa inapotumika.

Wafanyabiashara wanatumia mbinu hiyo kukurubuni, watakuambia wajanja wote wanatumia hii, tumia na wewe pia. Unasukumwa kununua hata kama kitu siyo muhimu kwako, kwa sababu unataka uwe kama wajanja wenzako.

Wapo watu ambao wamekuwa walevi siyo kwa sababu wanapenda, au kwa sababu wana matatizo yanayowasukua walewe, ila kwa sababu wanataka wawe karibu na marafiki zao ambao ni walevi. Hivyo wanaona wasipotumia kile wanachotumia hawatakubalika.

Wapo watu ambao wanalazimika kufanya kazi ambazo hazina maana kwao, hawazipendi na haziwasaidii kuboresha maisha yao, ila hawawezi kuondoka kwa sababu wanaona watachukuliwaje na wale ambao wanawazunguka.

Nguvu hii ya kurubuni kupitia mahusiano ya kijamii imekuwa inatumika kuwazuia wengi kufanya yale ambayo ni makubwa na bora kwao.

Ninachotaka tujifunze hapa rafiki yangu ni kukataa urubuni huu wa wengine kupitia ushirikiano wetu. Usikubali kufanya kitu kwa sababu tu unataka kukubalika na wengine, au kwa sababu unaogopa usipofanya utatengwa na hao wengine.
Unahitaji kufanya kitu ambacho unakiamini, kitu ambacho unaweza kukisimamia, kitu ambacho unajua ni sahihi kwako na kwa wengine pia.

Usihofu kwamba ulionao watakutenga, kama watakutenga basi hawakupaswa kuwa na wewe na hivyo unahitaji kuwapata wale ambao ni sahihi kwako.

Na jambo moja la kushangaza ni kwamba ukishaacha kujali sana kama wengine wanakubaliana na wewe au la, unaanza kuwavutia wale ambao wanakukubali vile ulivyo.
Ishi yale maisha yenye maana kwako na kwa wengine, fanya kile ambacho unajua ni sahihi na hutaishia kuwa mpweke, badala yake utawaondoa wale watu feki kwenye maisha yako na kubaki na watu halisi.

Huhitaji kucheza na kila mtu, hivyo chagua ni watu gani wapo tayari kucheza na wewe kwa kuishi maisha halisi kwako.

Nakutakia wakati mwema rafiki yangu, kumbuka kufanya jambo sahihi wakati wote.

Post a Comment

 
Top