0
Mtandao wa intaneti umeleta mapinduzi makubwa sana kwenye kila eneo la maisha yetu. Mtandao huu umefanya maisha kuwa rahisi kwa kutoa huduma ambazo hapo mwanzo hazikuwa zikipatikana. Kwa mfano mawasiliano, kupitia mtandao wa intaneti unaweza kuwasiliana na mtu popote pale alipo duniani kwa gharama ndogo. 

Mtandao huu wa intaneti una nguvu kubwa katika kuanzisha na kukuza biashara. Pamoja na nguvu hii kubwa bado watu wengi hawajaweza kuutumia vizuri mtandao huu kwenye biashara zao. Inakadiriwa ya kwamba ziadi ya watanzania milioni 12 wanatumia mtandao wa intaneti. Na idadi hii inaongezeka kila siku kutokana na ujio wa simu za gharama ndogo ambazo zinaweza kutumia mtandao wa intaneti. 



Je unawezaje kuutumia mtandao huu wa intaneti kibiashara? 
Kuna njia mbili ambazo unaweza kuzitumia kwenye mtandao huu wa intaneti kibiashara. Njia ya kwanza ni kufanya mtandao wa intaneti kuwa ndiyo njia kuu ya kufanya biashara yako. Pili ni kutumia mtandao wa intaneti kukuza biashara yako ambayo haifanyiki kwa njia ya intaneti.

Kufanya mtandao wa intaneti kuwa njia kuu ya kufanya biashara.
Hapa unautumia mtandao wa intaneti moja kwa moja kujiingizia kipato. Hii ni njia rahisi ya kuanzisha biashara ambayo haina vikwazo vingi kama njia za kawaida. Kupitia njia hii, mtandao wa intaneti unakuwa ndiyo sehemu kuu ya biashara yako.
Hapa unaanzisha biashara yako kwenye mtandao huu wa intaneti, unapata wateja kupitia mtandao huu na pia unatoa huduma au bidhaa zako kupitia mtandao wa intaneti.

Hii ni nia rahisi ya kufanya biashara kwa sababu huhitaji kuwa na sehemu maalumu ya kufanyia biashara yako, hivyo unapunguza gharama za kibiashara, unaweza kuendesha biashara ukiwa hata nyumbani kwako. Pia huhitaji kuwa na bidhaa unayozalisha wewe, unaweza kumuunganisha muuzaji na mnunuaji na wewe ukapata faida yako.
Pia unahitaji gharama ndogo kuanzisha biashara ya aina hii, ukishakuwa na kompyuta na uwezo wa kuunganishwa kwenye mtandao wa intaneti tayari una nafasi kubwa ya kuanzisha biashara kupitia mtandao huu.

Baadhi ya biashara unazoweza kufanya kwenye mtandao wa intaneti.
1. Unaweza kufanya biashara ya kutoa taarifa kuhusu jambo fulani. Inawezekana taarifa za matukio, au taarifa za kibiashara, au mafunzo mbalimbali ambayo watu wanayahitaji. Kwa njia hii unaweza kujitengenezea kipato kupitia matangazo ambayo watu wanaweza kuweka kwenye mtandao wako. Pia unaweza kuwatoza watu ada ya kupata taarifa unazotoa.

2. Unaweza kutengeneza duka lako kwenye mtandao wa intaneti, watu wakafika pale, wakajichagulia bidhaa, wakaziagiza na kisha wewe kuwatumia. Hapa unakuwa na bidhaa zako au za wengine ambapo unatumia mtandao kama duka lako. Hapo utaweka maelezo ya bidhaa hizo pamoja na bei zake. Pia utaweza utaratibu wa malipo na watu wanajua jinsi ya kuzipata.

3. Unaweza kutoa huduma zako mwenyewe kupitia mtandao huu. Kama wewe ni mshauri, unaweza kutumia mtandao wa intaneti kuwafikia watu ambao wanahitaji huduma yako ya ushauri. Pia unaweza kutumia njia hii ya mtandao katika kutoa huduma zako moja kwa moja na watu wakakulipa.

Kutumia mtandao wa intaneti kukuza biashara yako.
Hata kama biashara yako haifanyiki moja kwa moja kwa njia ya intaneti, bado unaweza kutumia mtandao huu kuikuza ziadi. Hapa namaanisha biashara yako inafanyika kwa njia za kawaida, ili mteja apate bidhaa au huduma ni lazima aje kwenye eneo unalofanyia biashara. Kwa njia hii biashara yako i akuwa haitegemei mtandao wa intaneti moja kwa moja. Unaweza kukuza biashara yako kwa njia zifuatazo;

1. Unaweza kutumia mtandao kutangaza biashara yako na kufikia wateja wengi zaidi. Hapa utaweka matangazo na maelezo ya biashara yako kwenye mtandao na watu wanapokuwa na uhitaji, wanatafuta na kukutana na taarifa zako. Hii ni njia rahisi ya kutangaza biashara ukilinganisha na njia nyingine za kutangaza.

2. Unaweza kutumia mtandao kutoa taarifa muhimu kwa wateja wako kuhusu biashara yako. hapa unawafahamisha wateja wako kuhusu kinachoendelea kwenye biashara yako. Hii inawafanya wateja kuwa na taarifa sahihi kuhusu biashara yako ili kuweza kufanya maamuzi sahihi.

3. Unaweza kutumia mtandao wa intaneti kujenga jamii ya wateja wa biashara yako. hapa unaweza kutengeneza makundi kwenye mitandao ya intaneti ambayo yanawaleta pamoja wateja wa biashara yako. Kwa umoja wao unaweza kuwapa taarifa muhimu na pia kuweza kutatua changamoto ambazo wateja wanakutana nazo kwenye biashara yako.

Post a Comment

 
Top