Na Askofu Zakary Kakobe.
Mpendwa msomaji, Je umewahi kuchukua muda japo mfupi, kuwaza sababu inayowafanya wanadamu kushidwa kuacha maovu? Kila kukicha, mahakama zote nchini zinatoa adhabu kali kwa watu wanaofanya maovu mbalimbali; lakini maovu hayo hayaishi katika jamii, bali yanaongezeka. Magereza yamejaa wafungwa hata nafasi ya kuwaweka haitoshi, lakini pamoja na hayo, maovu hayaishi.
Wako watu wengine wanaohukumiwa kunyongwa kwa sababu ya mauaji, na hilo ungeweza kufikiri lingepunguza idadi ya makosa ya mauaji, lakini ni kinyume, yanaongezeka. Ziko nchi nyingine duniani ambako wezi wanapewa hukumu ya kukatwa mikono, lakini wizi hauishi. Sehemu nyingi katika miji ya nchi yetu, siku hizi, wezi wengine wanapokamatwa na wananchi wenye hasira, kinyume cha sheria, wanachomwa moto kwa mafuta ya taa na kiberiti, wangali hai; na kufa kifo kibaya sana. Katika hali ya kawaida, baada ya matukio haya, tungetazamia kuona wezi wakipungua katika jamii yetu, lakini, ni kinyume, wanaongezeka, bila kujali yatakayowapata!
Kwa mtazamo huuhuu, tungelitazamia kuisha kwa ubakaji na ulawiti baada ya kipitishwa sheria kali ya kujamiiana ambayo inawafanya walawiti na wabakaji wa watoto wadogo, kufungwa gerezani maisha; lakini wapi! Watu wanabaka na kulawiti mchana kweupe kama vile hawajui yatakayowapata! Watu wengi sana wanakufa kwa Ukimwi. Karibu kila familia katika nchi yetu, imepoteza mtu mmoja au zaidi kutokana na janga la Ukimwi. Katika hali ya nzito ya namna hii, tungetarajia kwamba watu wangeacha uasherati na uzinzi! Lakini ni kinyume kabisa! Idadi ya makahaba wanaouza miili yao imeongezeka kuliko, na uasherati umekithiri! Mpendwa msomaji, unafikiria kiini cha tatizo ni nini? Kwa nini wanadamu wanashindwa kuacha dhambi?
. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .
Ingawa wezi wanachomwa moto, wizi haushi. Kwa nini?
. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .
Kiini cha tatizo, ni dhambi ya asili iliyomo ndani ya kila mwanadamu. Kila mwanadamu anazaliwa akiwa na asili ya dhambi ndani mwake. Asili ya dhambi inamfanya kila mwanadamu kufanya dhambi. Asili ya dhambi iliyomo ndani ya mwanadamu, ndiyo mzizi wa dhambi zote anazozifanya mwanadamu. Kumpa adhabu yoyote mwanadamu na kufikiri ataacha ouvu, ni kama kukata matawi ya mti na kufikiri hayatachipua tena, wakati mizizi ya mti haikuguswa.
Biblia inasema katika ZABURI 51:5,”Tazama mimi naliumbwa katika hali ya uovu; mama yangu alinichukua mimba hatiani”. Tunasoma pia katika ZABURI 58:3, “Wasio haki wamejitenga tangu kuzaliwa kwao; tangu tumboni wamepotea, wakisema uongo”. Unaona hapa! Wanadamu wote tangu tumboni mwa mama zetu tunakuwa na asili ya dhambi. Asili hii ya dhambi inatokana na mtu wa kwanza kuwako duniani aliyeitwa Adamu, aliyefanya dhambi katika bustani ya Edeni. Tunasoma katika WARUMI 5:12,”Kwa hiyo, kama kwa mtu mmoja dhambi iliingia ulimwenguni, na kwa dhambi hiyo mauti; na hivyo mauti ikawafikia watu wote kwa sababu wote wamefanya dhambi”. Asili hii ya dhambi ndiyo inayomfanya mwanadamu kutenda dhambi tangu kuzaliwa kwake.
Mpendwa msomaji, kwa muda mfupi, hebu jaribu kuwaza juu ya watoto wadogo. Mtoto mdogo akinyimwa titi na mamaye, atakasirika, kiasi cha kutumia mkono wake mdogo kumpiga kofi mamaye. Hasira hizi zinatoka wapi kwa mtoto mdogo? Baba mmoja akamtuma mtoto mdogo kwenda kununua majani ya chai dukani. Badala ya kununua majani ya chai, mtoto huyo mdogo atanunua maandazi na kula hukohuko. Kisha mtoto huyo atarudi nyumbani huku midomo imejaa mafuta ya maandazi. Ataulizwa, “Yako wapi majani ya chai?” Atajibu, “Zile fedha nimenyang’anywa njiani.” “Wewe mwongo, umenunua maandazi, huoni midomo yako imejaa mafuta? Na vipande nya maandazi hivi hapa kwenye mashavu.” “Hapana Baba, sijanunua maandazi”. Mtoto mdogo, uongo amefundishwa na nani?
Watakuwepo watoto wadogo wawili katika familia. Ni wakati wa sikukuu, na hivyo mama yao atawanunulia nguo za sikukuu. Kila mmoja atanunuliwa nguo tofauti na mwenzake. Watoto hao sasa watavaa nguo hizo, na kisha watatoka kwenda kutembea. Huko watakutana na mtoto mmoja mwingine ambaye atapiga kelele na kumwambia mmoja kati ya wale wawili waliovaa nguo mpya, “Hilooo, nguo yako siyo nzuri kama ya mwenzako!” Tayari, mtoto huyo atakimbia moja kwa moja mpaka kwa mama yake na kuanza kujigaragaza chini kwenye vumbi huku akivua nguo zake na kusema, ”Sitaki nguo hizi mbaya, nataka kama za mwenzangu”. Wivu huu kwa watoto wadogo, unatoka wapi?
. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .
Wewe mwongo, umenunua maandazi, huoni midomo yako imejaa mafuta?
. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .
Hebu mpe kitumbuamtoto mdogo, halafu mwambie amgawie mtoto mwenzie. Itakushangaza Mtoto huyo atamgawia kipande kidogo sana kiasi ya kwamba hata akimpa hakishikiki mkononi. Ukimwambia amgawie kipande kikubwa, atatikisa mabega na kusema, ”Sitaki”. Choyo hii kwa watoto wadogo inatoka wapi? Hii ndiyo dhambi ya asili anayozaliwa nayo kila mwanadamu. Dhambi hii ya asili ndiyo itakayomfanya mtoto mdogo kuwa na hasira, chuki, wivu, kusema uongo, kupenda maovu kuliko kwenda kusali n.k. Dhambi hii ya asili, itamfanya mtoto mdogo kutikisa viuno na kucheza dansi bila hata kufundishwa.
Kutokana na dhambi ya asili iliyomo ndani ya mwanadamu, mwanadamu anaweza akatamani kutenda mema yanayompendeza Mungu lakini akashindwa, akajikuta anafanya mabaya. Biblia inaelezea juu ya hali hii katika WARUMI 7:15, 17-20, ”Maana sijui nifanyalo; kwa sababu lile nilipendalo, silitendi; bali lile nilichukialo ndilo ninalolitenda, Basi sasa si mimi nafsi yangu ninayetenda hilo, bali ni ile dhambi ikaayo ndani yangu. Kwa maana najua ya kuwa ndani yangu, yaani ndani ya mwili wangu, halikai neno jema; kwa kuwa nataka, bali kutenda lililo jema sipati. Kwa maana lile jema nilipendalo, silitendi; bali lile baya nisilolipenda ndilo nilitendalo. Basi kama lile nisilolipenda ndilo nilitendalo, si mimi nafsi yangu nilitendaye, bali ni ile dhambi ikaayo ndani yangu”.
Namkumbuka dada mmoja aliniandikia barua na kutoa maelezo yafuatayo, “Mtumishi wa Mungu, mimi ni kahaba mkubwa sana, nashindwa kutulia na mwanaume mmoja. Ninatembea na wanaume wengi sana kwa siku moja. Maisha haya ya umalaya siyapendi, maana ni hatari sana kwa afya yangu hasa nikiwaza juu ya ugonjwa mbaya wa kisasa usiokuwa na dawa. Kuna wakati huwa naamua nisifanye tena umalaya, lakini wapi, muda mfupi tu najikuta narudia maisha yaleyale mabaya. Mtumishi wa Mungu, nifanye nini ili niweze kutulia na kuwa kama wanawake wengine waliojituliza?
Lile nilipendalo, silitendi bali lile nilichukialo ndilo
ninalolitenda
. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .
Mpendwa msomaji, najua unapenda kuishi maisha yanayompendeza Mungu, na kukaa naye milele mbinguni, ndiyo maana una dini; na wakati mwingine unajitahidi sana kusali. Hata hivyo huenda wewe nawe unakutana na hali hii katika maisha yako. Unatamani kuishi maisha yanayompendeza Mungu, lakini unajikuta unafanya maovu yanayomchukiza Mungu; na unawaza ufanye nini, kama dada huyu aliyeniandikia barua. Ndiyo maana “note” hii imeletwa kwako, kwa makusudi kamili ya Mungu; ili ujue yanayokupasa kufanya, na kukwepa kutupwa katika moto wa milele; maana watenda dhambi wote mahali pao ni katika ziwa liwakalo moto na kiberiti (UFUNUO 21:8).
Kama tulivyoona, mwanadamu anashindwa kuacha dhambi kwa sababu ya asili ya dhambi iliyomo ndani yake. Njia pekee inayomuwezesha mtu kushinda dhambi, ni kuwa na asili mpya, kwa kuzaliwa upya au kuzaliwa mara ya pili. Ndiyo maana Biblia inasema katika YOHANA 3:3, ”Yesu akajibu, akamwambia, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu”. Kuzaliwa mara ya pili, kwa maneno mengine, ni kuzaliwa kwa Roho (YOHANA 3:6). Yesu Kristo, alipokuwa duniani, alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote bila kutenda dhambi (WAEBRANIA 4:14-15). Siri ya yeye kushinda dhambi duniani, ilikuwa ni kwa sababu alizaliwa kwa Roho Mtakatifu (MATHAYO 1:18). Asili ya dhambi kwa mwanadamu inatokana na mtu mmoja Adamu. Katika kuzaliwa kwa Yesu, kutokana na bikira Mariamu kuchukua mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, mbegu ya mwanaume haikuwa na nafasi, hivyo asili ya dhambi ya Adamu haikuwamo ndani ya Yesu. Vivyo hivyo sisi nasi tukizaliwa kwa Roho, tutapata uwezo wa kushinda dhambi tukiwa hapahapa duniani. Watu wanaosema haiwezekani kuokoka duniani, hawajui kwamba hatuwezi kuokoka duniani tukiwa katika hali hii ya asili, mpaka tuzaliwe mara ya pili, kwa Roho.
Tunazaliwaje mara ya pili au kwa roho? Jibu, ni rahisi sana. Jambo hili linafanyika kwa imani tu! Kwa imani, tunakiri kwambi sisi ni wenye dhambi, kisha tunaungama dhambi zetu zote kwa kumaanisha kuziacha na kuomba kwamba tuumbwe upya katika Kristo Yesu ili tuweze kutenda matendo mema (WAEFESO 2:8-10; MITHALI 28:13). Tukifanya hivi, kwa ghafla tunakuwa viumbe vipya na ndani mwetu kunakuwa na asili mpya inayotuwezesha kushinda dhambi bila jitihada zozote! Kuokoka ni muujiza wa ajabu.
Je, uko tayari kuokoka au kuzaliwa mara ya pili? Najua uko tayari. Basi fuatisha sala hii kwa dhati. “Mungu wangu, hakika mimi ni mwenye dhambi, kwa kuzaliwa na kwa kutenda. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha. Mungu wangu, nisamehe dhambi zangu zote, na kuniumba upya katika Kristo Yesu, ili nizaliwe mara ya pili sasa, nikiwa na asili mpya inayoniwezesha kushinda dhambi. Kwa imani, napokea msamaha na kuamini kwamba nimezaliwa mara ya pili sasa katika Jina la Yesu. Amen”. Mpendwa, tayari sasa umeokoka. Ili uzidi kuwa na ushindi dhidi ya dhambi, inakupasa kuhudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu (ZABURI 119:11). MUNGU AKUBARIKI!!!
Post a Comment