0

Ndugu, sipendi muache kufahamu kuwa ule mshale unaonichoma kama moto sio jambo geni bali tu ni kawaida kwa awaye yote aliyezaliwa na mwanamke ili apate kuthibitika kama kweli amekuwa imara kwa kuzaa matunda ya uvumilivu katika pendo lisilo na unafiki.

Sikiliza mzee mwenzangu, amini usiamini, lisemwalo lipo kama halipo ujue muda wowote linaweza kupanda treni na kuja mtaani kwako alafu ukabaki unashangaa na kujikuta unajuta ya kwamba kwa nini ile siku ulikuwa mbishi kama HIV kwenye mwili wa mwanadam.

Baada ya kujua hilo, siku zote nimekuwa nikijiepusha sana na kupinga hoja ambazo sina uthibitisho nazo badala yake nikiziona ni za msingi huwa najitahidi kufanya upelelezi na majibu yake nikihisi yana faida kwako ndipo huwa nakumegea kupitia hapa Madini Media.

Mara zote tumekuwa pamoja sana katika uchambuzi wa kukosoa ambapo tulihisi jambo flani halipo sawa, zaidi pia tumekuwa tukipongeza kwa makofi mengi pale mambo yalipoonekana kwenda murua, na hii tulifanya kwa serikali na wengine, leo ni zamu yangu, mdogo wenu.

Ndugu na jirani zangu, inakuwaje swala la kuwanyanyapaa watu wenye udhaifu linakuwa sehemu ya maisha yetu, bila hofu tunawadhihaki wazi-wazi kwa habari ya mapungufu waliyonayo kana kwamba sisi tumekamilika na hayo hayawezi kutupata kwa namna yeyote ile.

Wewe una nini cha kujivunia, wewe mwanamke mrembo unayeucheka weusi wa house-girl wangu na kusahau kuwa unasaga nyama ya mwili wako, ulimi wako unamezwa na kutapikwa, umeguswa kila eneo mpaka kwenye mboni ya jicho ndio maana umekuwa kipofu, na laana juu.

Una nini mwanaume mwenye macho ya uzinzi, wenzio tunapagawa na utamu wa matunda wewe mwenzetu unapagawa na utamu wa takataka unazolamba bila kinyaa katika mifereji inayopitisha maji machafu yaliyojaa kila aina ya uozo toka ndani na nje ya mwili wa binadam.

Huyo mwanamke na huyu mwanamume niliowataja hapo juu, hivi kweli kuna vilema duniani zaidi ya hao?, ni nani aliye kipofu kuliko huyo mwanamke asiyeona hiyo mauti inayomtafuna?, ni nani kichaa zaidi ya huyo mume anunuaye uozo hata mizoga na kuutafuna kwa furaha?

Sikilizeni, kila mmoja ana mapungufu yake tena yasiyoonekana yaweza kuwa makubwa kuliko ya yule yanayoonekana, upofu wa akili ni heri upofu wa macho, na kusema hivi sijitetei kwa ile hoja yenu juu yangu ya kunidhihaki tena niliipokea kwa furaha na nina amani katika hili.

Sikufahamu ua lilipokuwa ila nilikutana tu harufu yake iliyoenea kila kona ya shule, kwa walimu na wanafunzi wa day na hostel eti “Bin’Otto hana nguvu za kiume kabisa kabisa, u-handsome wake haumfaidii chochote hata sasa tunajuta kwanini tulimchagua kuwa kiranja wa taaluma”. 

Hao ni watoto wa kike, usiombe kuskia kauli za boys waliosema, “Sasa unaishije asee, siungemwambia baba yako akakupeleka shule za boys tu, maana wewe kwetu ni kama mbuzi wa kuchinjwa (aliyehasiwa), alafu unawezaje kuendelea na shule wakati umeshajijua kuwa uko hivo”

Jamani jamani enyi mabinti, kweli mtu asiye na nguvu za kiume hafai hata kuwa kiongozi?, mpaka mnajuta mkisaidiana na boys wanaodai eti bila nguvu hizo basi haifai kuendelea na shule wala haifai kuishi, kweli mnanitamkia hivi ana kwa ana zaidi na walimu wanasapoti huo upuuzi.

Ndugu zangu, sipendi muache kufahamu kuwa ule mshale unaonichoma kama moto sio jambo geni bali tu ni kawaida kwa awaye yote aliyezaliwa na mwanamke ili apate kuthibitika kama kweli amekuwa imara kwa kuzaa matunda ya uvumilivu katika pendo lisilo na unafiki.

Basi ndugu na jirani wa madini media uliyekubali kufungua page hii na kuwa tayarikuambatana nami hadi mwisho wa mkasa huu, karibu sasa kwa pamoja tuangazie macho yetu juu ya hoja kadhaa, ama tujiulize maswali mawili matatu yatakayotupatia hekima ya juu zaidi.

1/ KUKOSA NGUVU ZA KIUME NI DAMBI?

2/ KUKOSA NGUVU ZA KIUME NI HASARA?

3/ KUKOSA NGUVU ZA KIUME NI AIBU?

4/ IPI IWE TAFSIRI YA NGUVU ZA KIUME?


Katika makabila yetu, imekuwepo kawaida ya kuwa-group watu wenye udhaifu mbali mbali na kuwatenga kabisa katika mambo flani flani wasishiriki na wenzao wakidai kuwa watasababisha laana kubwa, leo nasimama kama mwalimu kuwapeleka darasani watu wote wa jinsi hii.

MOJA: JE, KUKOSA NGUVU ZA KIUME NI DAMBI?

Ndugu zangu ni dhahiri kabisa Mungu anasema, “Ukitenda dhambi hakika utapata Laana”, kumbe ni kweli dhambi zinasababisha laana, hivyo inatubidi tuangalie kwa makini km kukosa nguvu za kiume ni dhambi, na ikiwa kweli mtu huyu na atengwe ili asilete laana.

Yesu ambaye alikuja kuwaokoa watu na dhambi zao hajalitaja hili kama ni dhambi, na zaidi Yesu anayeitwa mshauri wa ajabu, sisi sote ambao hatuna nguvu za kiume anasema “TUMEJALIWA”, iwe ni matowashi kwa hiari au kwa kuzaliwa, haijalishi, nachojua, “TUMEJALIWA”

Waulize walio katika ndoa watakwambia, hata wanafunzi walimwambia Yesu kuwa, “Haifai Kuoa”, lakini Yesu akawambia sio wote wawezao kukubaliana na hili wazo, “Sio wote wawezao kulipokea neno hili, isipokuwa wale waliojaliwa”, hayo ni nimeyachungulia Mathayo 19:3-12.

Na Paulo mtume kafafanua vizuri mambo haya katika 1Kor 7, sasa hapa wengine wasiopenda kujifunza wataanza kunung’unika et heee jamaa analeta mambo ya kidini, mara hooo huu mtandao wa Kikristo..., Acheni kushangaza, “KWANI MLIJUA HUU MTANDAO WA KIPAGANI?”

MBILI: JE, KUKOSA NGUVU ZA KIUME NI HASARA?

Hili sasa hatutatumia maandiko, bali nitawaleta kwenu wote wanaoona kama mimi ni maskini kuliko wote duniani kwa kigezo kwamba et nimefirisiwa nguvu zote za kiume, watatoa hesabu zao za ankra, sie et ee, mapato na matumizi kutokana na wao kuwa na nguvu hizo.

Tuanze na huyu anaelekea kustaafu anaeleza, “Mimi kweli nahitaji dogo-dogo ambaye nitakula nae kiinua-mgongo, maana huyu niliyenae kachoka sana haifai kwenda nae sinema, sababu kazoea wali maharage vya bei nafuu wakati mimi naenda kupata hela nyingi, nawaza itaishaje?”


Yaani baba huyo anawaza jinsi gani apate hasara ya hela ambayo ameihangaikia tangu ujana hadi leo ni mzee wa miaka 59, achana naye kutana na huyu dada, “Baba kafa mama kafa mimi nitakufa na hii mali itabaki ya nani, acha nimtafute kijana mwenye power wa kuniridhisha?

Jamani, hapo aneyetafutwa hapo ni kijana mwenye nguvu hizo mnazosema ili amridhishe huyu binti kwa hichi kipindi ambacho anaishi kwa matumaini, na lengo la binti kwanza ni kutapanya mali kwa hasira na huyu kijana mwenye power kisha wasindikizane wote kwenda kaburini.

TATU: JE, KUKOSA NGUVU ZA KIUME NI AIBU?


Kwanza ikibainika katika hosteli za wasichana kuwa kakangu huna nguvu za kiume, yaani utachekwa na kudharauliwa na kila binti mwenyeji na mgeni, na kila atakayesikia habari zako atahamasika kukuona kwa sababu wewe ni, “kinyago anayetembea, kuongea na kutafuna”

Usishangae kukuta hata boys wameketi chini ya kitanda na mabinti wakikuongea udhaifu wako, na mimi hapo hapo Napata kitu, wewe boy unayeniteta na mabinti ni aibu tosha kwako, mbali na kwamba unazo nguvu za kiume lakini nikupe pole sababu una homoni za kike.

Isitoshe hata pale mmlipomaliza tendo, mbona hamkuweza kutazamana usoni, hii yote aibu ya nini?..., mkumbuke kaka Yule aliyezidiwa akambaka dada yake, ni aibu sio aibu?..., baba zertu mara kibao wanafumaniwa, ndoa zinavunjika, mabinti wanatimuliwa shule, aibu tu yani.

Ni mamilioni ya aibu ambayo ukichunguza chanzo chake utakuta ni mme kuwa na nguvu za kiume ama mke kuhitaji nguvu za kiume, hivo tunapata picha kwamba asiye na nguvu hizi anayo nafasi kubwa na kutohusishwa na aibu ya namna hii, na hii yote ni sababu “AMEJALIWA”.

NNE NA MWISHO, IPI IWE TAFSIRI HALISI YA NGUVU ZA KIUME?

Hata usipoumiza kicha sana, kile kitendo cha kuketi pamoja nami hadi hapa wewe ni mwanaume tosha, pongezi kwako, cha msingi hakikisha unapotoka hapa haya mahusia unayabeba katika uzito wake na kuhakikisha yanabadili ulipokengeuka na yananyoosha kila paliponda bila kujua.

Tafsiri nyingine halisi ya nguvu za kiume, ni ule uwezo wa kubaini wazo kuu la kila jambo linalokuja katika maisha yako, mfano njaa, umaskini, upweke, mtaji, cheo, zawadi na lolote lile la furaha ama huzuni hakikisha unatambua nini maana yake, je ni kukuinua ama kukuangusha.


Vile vile mwanaume hua hapotezei, umesahau “Mzaha mzaha hutumbua usaha”, sio tu kubaini maana ya jambo pia na kuhakikisha unalishughulikia ipasavyo kadiri ya uwezo wako, wengi wanadharau matatizo madogo wanasahau kuwa mbu ndio anaongoza kuua kuliko tembo.

Kumbukeni hapa sijazungumzia swala la jinsia katika sehemu hii, hii tafsriri inatuhusu wote, na awaye yote tutamuita sio tu mwanaume bali mwanaume wa shoka kama atakuwa mwepesi wa kusamehe au kukiri kosa alilotenda na kuomba radhi, huku moyoni akijaa upendo kwa wote.

SASA, CHAGUA KUINGIA KATIKA SAFINA AMA UNGOJE GARIKA.

Ndugu na jirani wa MADINI MEDIA ni dhahiri kuwa tupo duniani, haya mambo tunayojivunia nayo cha kwanza sio yetu, ni ya yeye aliyeumba vyote na sisi tukiwemo, aliyetuumba sisi ndio yule aliyemuumba yule tunayemdhihaki, cha kujiuliza ni je salama yetu ni nini?

Ifike wakati tubadilike, tukubali hofu ya Mungu itawale ndani yetu, tuwe mbali kabisa na jeuri la mali uzuri na fahari tunazojihesabia kuwa ni zetu, tutengwe mbali kabisa na kibuli cha uzima, kasha tuwageukie wenzetu wenye udhaifu nasi basi tujitahidi kuwa sehemu ya udhaifu wao.

Nikisema niongee yote sitaweza kumaliza leo, ni mengi yanayoujaza moyo wangu, sema zaidi natamani kusikia kutoka kwako uliyesoma maandishi haya, natamani kujua maoni yako, nahitaji kusikia ushauri wako natama ukomenti hapo chini mawazo yako, karibu sana ndugu yangu.

Heshima sana kwako mpenzi kwa kutembelea mtandao huu, jitahidi basi kabla hujaondoka upitie vipengele mbalimbali katika blog hii ili uweze kuongeza mbinu za kufaulu katika maisha, lakini pia nakusihi usiache kukagua hapa kila siku ili kujipatia jipya linalokuhusu, naitwa
Bin’Otto.


©M(F)16SP17-05
Source:     Fiacrius K. Otto
Editor:      Samson P. Duttu
Allowed:  Share, copy&paste
Don’t try: To edit any.

Post a Comment

 
Top