- Changamoto ya kimazingira,
- Uzuri wa mazingira.
Changamoto ni kuwa utakutana na mazingira ambayo hujawahi kukutana nayo.
Utajikuta unatakiwa kuanza kuelewana kikazi na watu ambao hukuwa
ukijuana nao hapo kabla.
Uzuri wake ni kuwa utakutana na mazingira mapya utakayotakiwa kuyazoea,
pamoja na watu wapya ambao utajenga nao urafiki mpya wa kikazi.
Watu wapya na mazingira mapya kwa kawaida huwa na mambo yake mazuri
kuliko uliyozoea, vilevile kutakuwapo changamoto mpya ambazo hukuwahi
kuzikabili.
Faida kubwa unapoanza kazi ni kuwa viongozi wako wanakuwa na imani kubwa
nawe kuwa utatenda kazi bora kwa jinsi ambavyo uliweza kufaulu vizuri
usaili wako.
Unapoingia kazini ni rahisi kupendwa. Mkuu wako wa idara hawezi
kuzungumza na wewe kwa ukali, lugha itakayotumika ni ya majadiliano
zaidi kuliko amri. Unachotakiwa ni kuichukua tabia hiyo ili iendelee
kila siku.
Kutoka lugha ya majadiliano mpaka kuanza kufokeana kazini hapo ujue
tayari kuna vitu ambavyo vimeshakaribishwa. Ni wewe kama mfanyakazi
unakuwa umetengeneza mazingira ya kufokewa kutokana na utendaji wako
mbaya au nidhamu mbovu.
Shika muongozo ufuatao ili ukusaidie kujenga mazingira bora ya kazi
kuanzia ukiwa mpya kazini mpaka utakapotajwa kuwa mfanyakazi mzoefu
miongoni mwa wazoefu
Nidhamu binafsi na kazi
Kila siku unatakiwa ujiheshimu na uiheshimu kazi yako. Kipindi ambacho
viongozi wako wanakulea kutokana na upya wako kazini, wewe thibitisha
kwa vitendo nidhamu yako binafsi na ya kazi.
Wafanye viongozi wako wabadili nyakati za kukupenda kwa upya wako mpaka
kuvutiwa na wewe kwa utendaji na nidhamu yako binafsi.
Utashangaa maisha yako kazini yanakuwa mepesi kila siku. Unaweza
kustaajabu bosi ambaye kila mtu anamwogopa kwa ukali na usumbufu
mwingine, akija kwako mnazungumza kwa upendo na kuheshimiana.
Hivyo, jiheshimu, heshimu viongozi pamoja na wafanyakazi wenzako.
Hakikisha uvaaji wako ni mzuri wenye kuendana na mazingira ya kazi yako,
kisha uchape kazi kuzidi kiwango ambacho watu wangekitarajia kutoka kwako.
Unapaswa kuwa mtu mwenye malengo. Jiwekee malengo ya kazi na uyafikie.
Njia hiyo itakufanya uonekane mtu bora zaidi kazini na utamvutia mwajiri
kila siku.
Kuwa sehemu ya wafanyakazi
Ukiingia kazini, usitake kujionyesha kuwa wewe ni jeshi la mtu mmoja. Ni
kweli unatakiwa uzingatie zaidi kile ambacho kimekufanya uajiriwe,
lakini hapo kazini kuna wafanyakazi wenzako ambao kwa namna moja au
nyingine utahitaji ushirikiano wao.
Unaweza kujiona unajitosheleza kikazi, kwa hiyo ukaona huhitaji kuuliza
wala kumshirikisha yeyote kile unachofanya, lakini wewe ni binadamu.
Unaweza kuumwa ghafla kazini na wafanyakazi wenzako ndiyo watakaotakiwa
kukupa msaada.
Hivyo, ukiingia kazini jambo la kwanza hakikisha unafahamiana na
wafanyakazi wenzako. Hakikisha unajuana nao majina, na umwite
unayemhitaji kwa jina lake. Ni kosa kumaliza wiki nzima kazini ukiwa
hujachukua hatua yoyote kujua majina ya wafanyakazi wenzako.
Ukiwa mgeni kazini, hakikisha kila siku katika siku zako za mwanzo, uwe
unatumia angalau dakika 20 kuzungumza na wafanyakazi wenzako japo
wawili, mbadilishane uzoefu kuhusu kazi. Upate kile ambacho wamekuwa
wakifanya kila siku, nawe utoe ulichonacho.
Mazungumzo na wafanyakazi wenzako, yatakusaidia kujua mwajiri wako
anapenda nini na mambo gani hapendi. Utakachokipata kitakusaidia
kujitengenezea njia za kuishi ukiwa kazini.
Hakikisha mahudhurio mazuri
Siku za mwanzo ingia kazini mapema na ujitahidi kutoka kazini ukiwa
umechelewa. Baada ya hapo, hakikisha hiyo ndiyo inakuwa tabia yako siku
zote.
Ukiwa mpya kazini epuka visingizio na maombi ya ruhusa ya hapa na pale.
Onyesha kuwa umeanza kazi rasmi na upo tayari kiakili na kimwili.
Ukianza kutia doa mapema, utamfanya mwajiri wako akuone una upungufu.
Weka vizuri rekodi yako ya mahudhurio. Kumbukumbu za kiofisi zikitazamwa
wewe uonekane hukosi kazini na muda wako wa kuingia ni mapema kisha
huchelewa kutoka.
Una wagonjwa? Watembelee katika muda ambao unakuwa umeshatoka kazini.
Safari nyingine fanya siku zako za mapumziko. Fanya hivyo ili kutetea
rekodi zako za kiofisi hasa kwenye eneo la mahudhurio.
Usishiriki majungu, siasa
Kila ofisi majungu na mazungumzo ya siasa yapo, ni kutokana na
kukutanisha watu wa aina tofauti. Unachotakiwa kutambua ni kuwa umeingia
kazini kufanya kazi na siyo kupiga soga, kusengenya watu na kuendekeza
ubishi wa kisiasa.
Onyesha tofauti kwa kujiweka mbali na vitendo hivyo. Hakuna mwajiri
ambaye anaweza kuwapenda watu ambao muda wa kazi wanakuwa wanabishania
siasa. Ukijiunga nao, unamfanya mwajiri akuchukie ukiwa bado mgeni kazini.
Kama una damu ya siasa na unapenda kuzijadili, siyo vibaya kama
utazipangia muda wake, nyakati za mapumziko ya chakula au kipindi cha
kuupoza ubongo. Siyo unaingia kazini kabla hujashika faili lolote au
hujawasha hata kompyuta unaanza siasa. Ukiwa mtu wa aina hiyo, utayaona
mazingira ya kazi ni magumu na utajishushia heshima mbele ya mwajiri.
Mazungumzo na wafanyakazi wenzako muda wa kazi yawe yanahusu kazi. Siyo
kujadili mfanyakazi mwenzako ana uhusiano wa kimapenzi na nani. Hayo
siyo ambayo yaliwavutia wasaili wako kisha wakakuona unafaa kupewa kazi.
Tengeneza mtandao mzuri
Ni mtandao wa kazi. Ndani ya ofisi na nje. Hiyo ni kukusaidia kutimiza
wajibu wako inavyotakiwa. Itakusaidia wakati wowote pale unapojiona
umekwama kupata msaada wa haraka.
Waajiri wengi wana nongwa, hawapendi kuona mtu anasimama na kutembea
kutoka meza moja kwenda nyingine akiwa kazini. Kwa hiyo, unapohitaji
msaada kutoka kwa mfanyakazi mwenzako, mtumie barua pepe au ujumbe wa
simu, kisha naye akujibu.
Mtambue mfanyakazi mzuri
Ukiwa mgeni kazini unatakiwa kumtambua mfanyakazi mzuri, anayetimiza
wajibu wake na ambaye anamvutia hata mwajiri wako. Ukimshamjua mfanye
kuwa rafiki na mshauri wako wa mambo ya kazi.
Post a Comment
Click to see the code!
To insert emoticon you must added at least one space before the code.