Rais wa Tanzania John Magufuli ametangaza kwamba taifa hilo litanunua ndege zaidi katika juhudi za kufufua shirika la ndege la taifa hilo.
Amesema serikali yake imedhamiria kununua ndege nne zikiwemo ndege kubwa tatu ambazo zitasaidia kuinua "uchumi wa nchi kwa kuwezesha watalii kuja hapa nchini moja kwa moja kutoka nchi zao."
Dkt Magufuli alisema hayo baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Masoko ya Afrika wa Kampuni ya utengenezaji wa ndege ya Boeing yenye makao yake nchini Marekani Bw. Jim Deboo katika ikulu jijini Dar es Salaam.
Amesema Tanzania inpanga kununua ndege aina ya Boeing 787 Dash 8 Dreamliner yenye uwezo wa kuchukua abiria 262 ambayo inatarajiwa kuwasili nchini humo Juni 2018.
Ndege nyingine ambazo Tanzania itazinunua ni ndege moja aina Bombardier Q400 Dash 8 NextGen inayotarajiwa kuwasili Mwezi Juni 2017, ndege 2 aina ya Bombardier CS300 zenye uwezo wa kuchukua kati ya abiria 137 na 150 na zinazotarajiwa kuwasili nchini kati ya Mei na Juni, 2018.
Malipo ya awali kwa ndege hizi yameshafanyika.
Post a Comment