0
Habari mpendwa Rafiki na msomaji wa Amka Mtanzania? natumaini unaendelea vizuri rafiki yangu na karibu katika makala yetu ya leo ambapo leo tutajifunza kwa pamoja tofauti kubwa kati ya kusikia na kusikiliza. 

Dunia ya sasa imejaa kelele nyingi. Na changamoto kubwa ni kupata mtu wa kukusikiliza kwani watu wengi wako bize na mambo yao ya kila siku. Kusikiliza ni kazi ngumu ambayo inawashinda watu wengi sana. Kumekuwa na desturi ya mtu kuongea bila hata ya kukaa kimya na kumsikiliza mwenzake amalize kuongea. Kuongea ni rahisi kuliko kusikiliza na tunashauriwa kwamba tuwe wasikilizaji bora kwani tutajifunza mambo mengi sana kuliko ukiwa mzungumzaji. Kusikiliza ni sayansi ambayo inahitaji kuhusisha mwili na akili vyote kwa wakati mmoja. Na kama ulikuwa hujui ndugu rafiki kuna tofauti kubwa kati ya kusikiliza na kusikia.


Kusikia (hearing) ni nini? Ni uwezo wa asili wa kupokea mawimbi ya sauti au jumbe. Kwa mfano, labda wewe uko darasani unasoma na mwalimu yuko mbele ya ubao anafundisha halafu unasikia nje sauti za magari, ndege na sauti mbalimbali huko nje wakati wewe ukiwa darasani hiyo ndiyo tunaita kusikia (hearing). Kusikia ni kitu ambacho kina kuja tu kiasili wala huwezi hata kukizuia kwa mfano; je wewe unaweza kujizuia kupiga chafya au Kukohoa? Kwa hiyo huwezi kujizuia kusikia, unasikia lakini unakuta akili yako na mwili wako haviko pale. Kwa mfano rafiki yangu hapo ulipo sasa umekaa unasoma makala hii akili yako na mwili wako umevielekeza katika kusoma makala hii lakini husikii watu, au sauti za vitu mbalimbali huko nje au pembeni yako? Sasa hiyo ndio maana halisi ya neno kusikia rafiki yangu.

Rafiki, mpaka sasa umeshajua nini maana ya kusikia. Je kusikiliza (listening) ni nini? Ni mchakato wa kuchagua nini cha kusikia kwa ajili ya kuelewa jambo fulani kwa dhumuni la tukio au shughuli fulani.

Kusikiliza ni kukusudia (intentional) una uwezo wa kuamua kusikiliza au kutokusikiliza. Kusikiliza inahusisha ujuzi ambao mtu anaweza kujifunza au kufundishwa. Kwa mfano, mwanafunzi darasani anasikiliza ili aweze kupata maarifa. Katika mahakama hakimu anasikiliza maelezo ya pande zote mbili kutoka kwa shahidi, mtuhumiwa na mawakili ili aweze kufanya hukumu.
Kwa hiyo, kuna tofauti kati ya kusikia na kusikiliza. Kuna muda mwingine tunasikia hata kama hatuko tayari kusikia kwa mfano, fikiria kelele zinazopigwa pale unapotaka kulala. Lazima utapokea mawimbi ya sauti kwa sababu una uwezo wa kusikia. Tunafanikiwa kusikia kwa sababu sisi siyo viziwi. Na kusikiliza ni kitu ambacho una hiyari nacho kusikia au kutosikiliza yaani una maamuzi ya kufanya. Kusikiliza ni kazi kuliko kusikia. Anza kuwa msikilizaji bora kuanzia leo.

Mbinu Tisa (09) Za Kukuwezesha Kuwa Msikilizaji Bora Sehemu Yoyote Ile

1. Kuwa na shauku ya kusikiliza. 
Vitu vingi tunavyofanya na kufanikiwa mara nyingi vinakuwa ni matokeo ya shauku. Hapa unatakiwa kuiambia akili yako kuwa unatakiwa kuelewa nini mwongeaji anaongea. Pili unatakiwa ujikite katika kile ambacho mwongeaji anasema. Kabla tukio fulani halijaanza kwa mfano semina, basi kitu cha kwanza wewe kuwa na shauku ya kutaka kusikiliza.

2. Kuwa wazi na jenga nia ya kujifunza. 
Kuna muda mwingine akili huwa inakataa kuingiza taarifa mpya hii inatokana na mitazamo mbalimbali tuliyojijengea sisi wenyewe. Unatakiwa kusikiliza vitu hata kama huviamini. Kumbuka kuna vitu hata wewe huwa unaongea na watu hawavipendi lakini wanakusikiliza hivyo basi, kusikilizwa ni hitaji la kila mtu hata kama anaongea kitu ambacho hakina maana. Kila mtu anapaswa kusikilizwa. Weka nia ya kutaka kujifunza na usijiwekee vikwazo katika akili yako ili ushindwe kusikiliza vizuri.

3. Ahirisha kuhukumu. 
Unatakiwa kuahirisha hukumu au kumkosoa mwongeaji kulingana na mwonekano wake. Kwa mfano unatakiwa usijikite katika kuangalia nguo alizovaa mwongeaji, sifa zake, mtindo wa kuongea na kadhalika. Wewe lengo lako ni kujifunza achana na mambo sijui kavaaje, na mengine. Wewe unatakiwa ujikite zaidi kusikiliza na kuchota maarifa. Mfano kama uko kwenye semina hakikisha wewe lengo lako ni kusikiliza na kuelewa yale unayofundishwa na achana na mambo mengine yanayotokea kama kuanza kumhukumu mwongeaji.

4. Jiweke tayari kimwili na kiakili. 
‘’ unatakiwa kujikita (concentrate) kimwili na kiakili hata mwongeaji anapokuangalia anajua unasikiliza. Mwili wako ukae kama vile uko kwenye semina na iambie akili yako kuwa leo unakwenda kusikiliza semina na siyo kusikia semina. Dhibiti kutawanya mawazo kwa mfano, unakuta mtu kimwili yuko hapa lakini kiakili yuko dunia nyingine. Akili yako inakuwa inaruka ruka huku na huko haitulii kama vile nyani au tumbili anavyoruka ruka katika mti.

5. Muangalie mwongeaji usoni.
Unashauriwa hapa kumuangalia pale anapokuwa anaongea. Macho yako na yake yaangaliane yaani muoneshe kuwa kuna mawasiliano kati ya mwongeaji na msikilizaji. Ukimuangalia mwongeaji utajifunza kwa lugha ya mdomo na lugha ya vitendo. Hivyo ni muhimu sana kumuangalia mwongeaji kwani unaweza ukaachwa katika kuelewa jambo pale anapokuwa anatumia lugha ya vitendo.

6. Lenga katika kuelewa mtazamo wa mwongeaji.
Hapa kama msikilizaji unatakiwa kusikiliza kwa lengo la kuelewa ni kitu gani mwongeaji anakiamini. Pale mwongeaji anapokuwa anaongea jambo wewe sikiliza kwa makini kabisa nini mzungumzaji anakiamini katika kile anachokiongea. Muda mwingine mzungumzaji anaweza akakosea akiwa katika jukwaa lakini hupaswi kumkosoa bali unatakiwa kuvumilia. Jaribu kuvuta picha ingekuwa ni wewe je ingekuwaje?

7. Bashiri na uliza maswali. 
Unatakiwa kutabiri au kubashiri maswali na kujiuliza hii njia nzuri itakayokuwezesha wewe kuwa macho na nini kinachoendelea. Bashiri je ni nini mzungumzaji anaweza kusema mbele. Unapokuwa katika semina au darasani jiulize maswali mbalimbali juu ya kitu unachosikiliza, hii itakufanya kukumbuka na kuwa macho na kitu kinachoendelea.

8. Tazama/angalia kama vile unasikiliza.
Unatakiwa kumuonyesha mzungumzaji kuwa unasikiliza yaani uko pale umekaa vizuri kimwili na kiakili. Kwa hiyo, mzungumzaji ataona mwonekano wako kama unasikiliza au la. Kama uko katika semina mzungumzaji anaongea na wewe umelala hii itampa picha mzungumzaji kuwa hamko pamoja. Ukiangalia kama vile unasikiliza unakuwa unampa hamasa mzungumzaji kuwa mko pamoja mnashirikiana. Unashauriwa kukaa vizuri, hakikisha mnaangaliana na mnashirikiana katika mijadala inayotokea katika semina nk.

9. Epuka vitu vitakavyokuletea kero. 
Ukiwa unaenda katika kusikiliza jambo kama ni semina au kitu Fulani hakikisha unavaa kulingana na sehemu husika. Vaa nguo kulingana na hali ya hewa kama unakwenda kwenye semina eneo la baridi hakikisha una vaa nguo za baridi vivyo hivyo katika joto. Kuvaa nguo ya joto sehemu ya baridi itakuletea kero ambayo baadaye inakuwa kama kizuizi na ikakupelekea usishiriki semina vizuri. Usikae karibu na mtu anayependa kuongea kwani atakupunguzia uwezo wa kujikita zaidi katika kusikiliza na kupoteza umakini.

Hivyo basi, kusikia siyo kazi bali kazi ni kusikiliza. Nakutakia utekelezaji mwema katika haya uliyojifunza leo.



Post a Comment

 
Top