0
WATUMISHI watano wa Halmashauri ya Wilaya ya Nzega mkoani Tabora wamefukuzwa kazi na wengine wawili wameshushwa vyeo kwa tuhuma za kutafuna Sh milioni 190.

Kutimuliwa kazi kwa watumishi hao kunatokana na uamuzi uliotolewa na Baraza la Madiwani la Wilaya ya Nzega baada ya uchunguzi kukamilika na kubaini ni kweli walitafuna fedha za Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) pamoja na fedha za chanjo.



Akitangaza uamuzi huo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Nzega, Marco Kiwele alisema watumishi hao walishindwa kuwajibika ipasavyo katika nafasi zao pamoja na kufanya udanganyifu na uzembe ulioisababishia hasara halmashauri hiyo.

Aliwataja waliofukuzwa kazi ni Mweka Hazina Stanslaus Lawrence, Katibu wa Afya Wilaya, Kisusi Sikalwanda, Mratibu wa Chanjo Joel Mjondora, Ofisa Ugavi Selemani Charahani na Mtendaji wa Kijiji, Said Madua.

Kiwele aliwataja walioshushwa vyeo vyao ni aliyekuwa Daktari wa Wilaya ya Nzega, Emmanuel Mihayo na Mhasibu wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Denis Gombeye.

Mwenyekiti huyo wa halmashauri alisema watumishi waliofukuzwa kazi kutokana na ubadhirifu watafikishwa katika mkono wa sheria ili ichukue mkondo wake kutokana na makosa yaliyoyafanyika. Aliwataka watumishi wote kuhakikisha wanafanya kazi kwa kuwajibika ipasavyo.

Post a Comment

 
Top