1. Wazimamoto 10,000 wakabiliana na moto California
Moto huo umeathiri maelfu ya watu kusini mwa jimbo la California
Zaidi ya watu 10,000 wanashiriki katika juhudi za kukabiliana na moto katika jimbo la California ambako kumezuka msururu wa visa vya moto katika maeneo manane.
Maafisa wa kikosi hicho maalumu cha kukabiliana na moto wanasema kuwa sehemu moja kulikozuka moto kumewashinda wahusika kuuzima.
Moto huo umelazimisha kufungwa kwa barabara na reli inayounganisha miji ya Los Angeles na Las Vegas.
2. Ubaguzi dhidi ya weusi Uingereza waongezeka
Ripoti mpya nchini Uingereza imeonya kuwa watu weusi na wale wanaotoka jamii za watu wachache wanakabiliana na kile kilichotajwa kama ubaguzi uliokubalika katika maeneo mengi.
Inadaiwa kuwa hali hiyo imekuwa mbaya zaidi kwa muda wa miaka mitano iliyopita. Ripoti hiyo iliyotolewa na Tume ya Usawa na Haki za Kibinadamu inaeleza masikitiko yake juu ya ongezeko maradufu la makosa ya chuki tangu Uingereza kupiga kura kujiondoa kutoka Umoja wa Ulaya mnamo Juni.
Serikali imesema itaupiga msasa mpango wa haki hivi karibuni.
3. Rais wa Bolivia kufungua chuo cha kushindana na Marekani
Rais wa Bolivia, Evo Morales, amefungua rasmi chuo maalumu cha kijeshi kinachotoa mafunzo yanayoshindana na yale yanayotumiwa na Marekani kujiimarisha katika mataifa yanayostawi duniani.
Bw Morales alisema kuwa chuo hicho kipya kinakusudia kushindana na kile kijulikanacho kama US Army of the Americas kilichokuwa kikitoa mafunzo kwa washirika wa Marekani katika Vita Baridi katika eneo la Latin America.
4. Watu watatu wauawa kwenye shambulio Uturuki
Serikali ya Uturuki inasema watu watatu wameuawa na wengine 40 kujeruhiwa katika bomu lililotegwa katika gari la kulipuliwa karibu na kituo cha polisi na kambi ya jeshi Mashariki mwa Van, karibu na mpaka na Iran.
Picha katika runinga zinaonyesha magari kadhaa ya polisi na ambulansi katika eneo hilo. Haikujulikana mara moja aliyehusika katika shambulio hilo.
5. Cisco kuwafuta kazi wafanyakazi
Kampuni kubwa ya utengenezaji wa vifaa vya kiufundi, Cisco systems, imetangaza mipango ya kuwafuta kazi asilimia saba ya wafanyakazi wake kote duniani, huku ikibadilisha aina ya vifaa inavyotengeneza; kulenga biashara inayozidi kuimarika zaidi katika sekta za usalama na teknolojia ya kikompiuta.
Kupitia taarifa maalumu Cisco wamesema kuwa watawaachisha kazi watu 5,500.
Post a Comment