0
Wapo watu wengi ambao huwa hawafikiri sana kwamba, kujiingiza kwenye madeni mengi ni kitu cha hatari. Watu hawa huja kugundua kwamba wapo kwenye hatari hiyo mara baada ya madeni hayo kuwalemea sababu ya wingi wake.

Kutokana na madeni hayo kuwa mengi, na kushindwa kuyalipa, hapo sasa ndio majuto na kilio huanza kutanda. Na wengi huanza kujilaumu kwa nini walikopa mikopo mingi, mikopo ambayo kama inawatesa kwa sasa, kutokana na kushindwa kuilipa.
Najua umeshawahi kukutana na watu ambao wana mizigo mingi na mikubwa ya madeni. Inawezakana watu hawa walikuwa jirani zako, ndugu au pengine hata wewe mwenyewe. Je, ulishawahi kujiuliza inapokutokea hali kama hii ni kitu gani unachotakiwa kufanya?
Leo kupitia makala haya, twende kwa pamoja kujifunza hatua muhimu za kukusaidia kutoka kwenye madeni.
1. Weka mipango imara.
Hatua ya kwanza itakayokusaidia kutoka kwenye madeni yako, ni kule kuamua kuweka mipango imara ya kukutoa kwenye madeni yako uliyonayo. Utaweza kulifanikisha hili vizuri, ikiwa utakaa chini na kupitia kiwango cha pesa unachotumia, ukilinganisha na kile kinachoingia.

Weka mipango imara ya kutoka kwenye deni ulilonalo.
Kwa mfano, inawezekana kabisa upo kwenye madeni kwa sababu unatumia pesa nyingi hovyo. Kwa hali hiyo hukupelekea matumizi yazidi kipato na kukufanya kukopa. Hivyo, hakuna namna nyingine zaidi ya kuweka mipango imara ya kubana matumizi na kuweza kuondokana na madeni.
2. Tafuta chanzo kingine cha pesa.
Njia nyingine nzuri ya kuweza kuondokana na madeni uliyonayo ni kutafuta chanzo kingine cha pesa. Acha kung’ang’ania kuwa na chanzo kimoja cha pesa, hiyo inaweza ikawa ni hatari sana kwako katika harakati za kujikwamua kutoka kwenye madeni.
Kwa mfano, kama umeajiriwa tafuta namna yoyote ile uwekeze kwenye hiyo biashara. Halikadhalika, kama umejiajri kwa kufanya biashara yako mwenyewe, jitahidi baada ya muda uwe na biashara nyingine. Kwa kufanya hivi itakusaidia kuweza kutoka kwenye madeni.
3. Punguza matumizi yasiyo ya lazima.
Mbali na kuweka mipango imara na kutafuta chanzo kingine cha pesa, pia unaweza kutoka kwenye deni ulilonalo kwa kupunguza matumizi yasiyo ya lazima. Wengi wetu mara nyingi huwa ni watu wa matumizi mengi pasipo kutarajia.
Unawezaje kutoka kwenye matumizi yasiyo ya lazima? Kwanza, unaweza kuepuka matumizi yasiyo ya lazima kwa kuepuka kununua vitu visivyo vya  lazima sana kwako. Pili, ni kuwa makini na kila pesa inayotoka kwa kuiwekea kumbukumbu. Kwa hatua hiyo, inaweza kuwa msaada kwako kukutoa kwenye madeni.
4. Anza kulipa madeni makubwa.
Kama madeni uliyonayo ni mengi, ni vizuri kuya orodhesha madeni yako na kuanza kuyalipa madeni yale makubwa. Kwa kuchukua hatua hiyo utajikuta mahali, umeweza kuuotoa mzigo wa madeni ambao ulikuwa unakusumbua kwa muda mrefu.
Kwa kuhitimisha makala haya, naomba niseme hivi; mikopo ni mizuri ikiwa itatumia vizuri kwa malengo maalumu. Endapo utaitumia vibaya inaweza ikawa ni mzigo mkubwa na kugeuka kuwa deni.
Kama mkopo uliouchukua umekuwa deni, tafadhari hizo ni baadhi ya hatua ambazo unaweza kuzitumia kutoka kwenye madeni uliyonayo. Lililo kubwa kwako, fanyia kazi hicho ulichojifunza na chukua hatua.
Nikutakie siku njema na kila la kheri katika kufikia mafanikio makubwa.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,

Post a Comment

 
Top