0
Habari ndugu Rafiki na Msomaji wa Dakika Za Madini? Natumaini hujambo na karibu katika makala yetu ya leo. Kila siku ni siku mpya kwako hivyo basi, usikubali kupitwa na maarifa yaani usikubali siku kupita bila kujifunza kitu kipya kwako. Na siku nzuri ya kuanza kujifunza ni leo yaani sasa hivi na siyo baadae au kesho kwani kesho na baadae hauna uhakika nazo muda ambao una uhakika nao ni sasa hivi.
Katika jamii zetu tumekuwa tukiaminishwa / kufundishwa kuwachukia watu ambao wametuzidi kimafanikio au kifedha na kujazwa mitazamo hasi isiyohesabika. Wale watu wanaofanya vitu chanya katika jamii ndio watu wanaochukiwa na watu au jamii yenye mtazamo hasi. Watu chanya ni wachache sana katika jamii yetu ndio maana watu wakiwaona watu ambao wapo tofauti nao lazima wawajengee chuki bila sababu. Watu wenye mitazamo hasi ni wengi sana katika jamii yetu hivyo basi, hawapendi kuona mtu akibadilika hata kidogo wanapenda kuona kila siku ufanane na wao.



Ndugu msomaji, leo tutajifunza kwa mifano halisi kabisa katika jamii yetu makundi au aina ya watu wanaochukiwa bila sababu ya msingi na makundi ya watu hao ni kama ifuatavyo;

Watu wanaosema ukweli; Kuna msemo huwa unasema msema ukweli ni mpenzi wa Mungu lakini huyu msema ukweli ambaye ni mpenzi wa Mungu ni mtu ambaye anachukiwa sana katika kila idara ya maisha yetu. Mtu anayesema ukweli na kusimamia ukweli katika jamii anaonekana ni adui mkubwa zaidi ya maadui wakubwa watatu aliyowahi kuwasema Mwalimu Nyerere ambao ni ujinga, maradhi na umasikini. Kwa mfano, unaweza kuwa na rafiki yako na ukamweleza ukweli juu ya mwenendo wake wa maisha labda kuna sehemu amekwenda mrama na wewe lengo lako ni kumrekebisha tu basi ukimwambia ukweli chuki, uadui na wivu ndio unaanzia hapo. Ataona kama wewe siyo mtu mwema kwake kwa kumwambia ukweli. Hamtaweza kuwa marafiki tena kama zamani bali mtakua maadui kama vile paka na panya. Kama mlikuwa mnasalimiana hataweza tena kukusalimia bali atakukua anakusemea maneno hasi katika jamii na kuendelea kukuua kwa ulimi tu.
Watu wanaosimamia ukweli katika maeneo ya kazi wanaonekana ni maadui wakubwa. Wale wanaosema ukweli lazima watatengwa na wenzao hata ufanisi wa kazi utapungua na ushirikiano katika kazi utapungua. Habari itakayokuwa ni kupiga umbea na majungu. Katika kila sehemu ya maisha yetu wale viongozi wa sehemu mbalimbali wanaosema ukweli huwa wanachukiwa tu watu wenye mtazamo hasi.

Hatua ya kuchukua; hatuwezi kupata maendeleo bila kusimamia ukweli. Ukiujua ukweli nao ukweli utakuweka huru. Kwanini sasa tuendelee kutokuwa na uhuru kwa kuogopa kusema ukweli? Kama wewe ni mtu chanya na unapenda kuona mabadiliko katika jamii endelea kusema ukweli na kusimamia ukweli bila kuogopa. Kama ni kanisani, msikitini sema ukweli, kama ni kwenye familia sema ukweli na kusimamia ukweli, sehemu yoyote ile endelea kusema ukweli wala usiogope. Kuficha ukweli ni sawa na mtu anayeingia kwenye tanuri la moto utaendelea kuungua na moto katika nafsi yako na kupata majeraha ya moyo na kukosa uhuru katika maisha yako.

Watu Wanaofanya Kazi Kwa Bidii; wale watu wanaofanya kazi kwa bidii huwa wanakua na matokeo mazuri sana katika kile wanachofanya. Ile juhudi yao ya kufanya kazi kwa kujituma ndio inawatofautisha na wale watu wanaofanya kazi zao kwa mazoea yaani kwa kawaida hatimaye utofauti huo ndio unazaa chuki kati yao. Kama mwenzako amejituma na kupata matokeo mazuri kwa nini na wewe usijitume na kupata matokeo mazuri? Badala ya kuanza kumchukia na kuanza kuoneana wivu bila sababu ya msingi. Kama uko kazini angalia yule mtu anayefanya kazi zake kwa kujituma na kwa muda kama atapendwa na wenzake lazima atachukiwa kwa sababu amejitoa katika kundi hilo hamfanani tena. Kama ulikuwa katika timu ‘bata’ ukaachana nao lazima watakuchukia kwa sababu umewaacha katika sehemu ya hatari na umekwenda katika sehemu ya salama. Ulikuwa katika timu umbea, majungu, kumesengenya na kuhukumu ukabadilika wale wenzako uliowaacha kule lazima watakusemea vibaya na kukuchukia.

Hatua ya kuchukua; Kama ulikuwa ni mtu wa kujituma katika kazi zako endelea kuwasha moto wa kujituma mwisho wa siku watakuja kukuelewa na kuwa mwalimu wao. Usiogope kuchukiwa kwa sababu unajituma katika eneo fulani la maisha yako. Tunahitaji watu wanaojituma ili kuleta maendeleo katika jamii na si vinginevyo.

Watu Waaminifu Na Waadilifu; uaminifu unalipa sana kwenye kila eneo la maisha yetu. Sasa siku hizi uaminifu na uadilifu umekuwa adimu sana katika zama hizi za taarifa. Watu waaminifu wanaonekana ni watu wa ajabu katika jamii yenye mtazamo hasi. Kila mtu anapenda kuwa na mpenzi mwaminifu, mfanyakazi mwaminifu na mwadilifu na n.k. Waajiri wanahangaika kuwatafuta watu waaminifu na waadilifu watakaoweza kufanya nao kazi. Serikali nayo inahangaika kila siku kuwatafuta watu waadilifu na waaminifu katika kazi na kuendelea kusisitiza uaminifu na uadilifu katika kazi. Bila uaminifu na uadilifu mambo lazima yaende mrama. Sasa wale watu ambao ni waaminifu na waadilifu ndio watu wanaochukiwa na kutoungwa mkono katika kusimamia falsafa ya uaminifu na uadilifu. Kwa mfano, wale watu ambao ni waaminifu katika maisha yao ya ndoa wanaonekana ni maadui kwa wale watu ambao wamezoea ‘michepuko’ na kuona ‘michepuko’ ndio dili kuliko uaminifu watakutengenezea mazingira ya kukuandaa na mitego mbalimbali ili uweze kunasa na kuingia katika kundi lao hivyo usikubali kunasa na kuwa katika kundi la watu ambao hawana uaminifu na uadilifu.

Hatua ya kuchukua; bado dunia inahitaji watu waaminifu na waadilifu hivyo ni fursa nzuri ya kuwekeza katika uaminifu na uadilifu. Kama wewe ni mzazi, mlezi, mwalimu anza leo kuwafundisha watoto falsafa ya uaminifu na uadilifu tokea wakiwa wadogo. Uaminifu na uadilifu utakupa faida kubwa katika maisha yako hivyo endelea kuwasha moto wa uaminifu na uadilifu.

Kwa kuhitimisha, tunahitaji watu chanya ili kuendeleza dunia. Watu hasi wapo kwa ajili ya kubomoa jamii na siyo kujenga. Tunatakiwa kuwapenda wale watu wanaoleta mabadiliko chanya katika jamii yetu na kujifunza kupitia kwao na siyo kuwachukia. Mabadiliko yanaletwa na watu chanya hivyo basi, wanahitajika watu chanya wengi ili kujenga jamii. Tusitawaliwe na wivu na tamaa zitakazotupeleka mahali pabaya na ishi katika maisha yanayompendeza Mungu na jamii kwa ujumla na tuendelee kuweka juhudi na maarifa katika kazi tunazofanya.


Post a Comment

 
Top