0
Waandamanaji wakiteketeza kituo cha polisi Kenya
Waandamanaji wamevamia kituo kimoja cha polisi kinachohusishwa na utekaji na kisha mauaji ya wakili mmoja mteja wake na dereva wa teksi katika kisa kilichotikisa idara ya sheria nchini Kenya.

Waandamanaji walioitikia mwito wa chama cha wanasheria nchini Kenya cha kususia vikao vyote vya mahaka hadi wale waliotekeleza unyama huo wafikishwe kizimbani, walifika kwenye kituo hicho cha Syokimau viungani mwa mji wa Nairobi na kuvamia chumba kinachodaiwa kutumika kuwatesa watatu hao kabla yao kukutana na mauti.

Walikiwasha moto licha ya ulinzi mkali wa polisi waliokuwa wameshika zamu kituoni humo ishara ya hasira inayochemka nchini Kenya dhidi ya mauaji ya watatu hao mikononi mwa walinda usalama.

Haijulikani ilikuwaje hadi polisi wakawaruhusu waandamanaji hao kukiteketeza huku wengine wakidai ni njama ya kuficha ushahidi muhimu wa DNA

Wakili Willie Kimani, mteja wake Josephat Mwenda na dereva wao wa teksi Joseph Muiruri walitekwa wakitoka mahakamani Mavoko na kisha wakafungiwa katika kituo cha polisi wa utawala Syokimau.

Bw Kimani na Bw Mwenda walikuwa wameabiri gari la Bw Muiruri baada ya kuhudhuria kesi katika mahakama ya Mavoko 23 Juni, walipotekwa na watu wanaodaiwa kuwa maafisa wa usalama.

Haijulikani ilikuwaje hadi polisi wakawaruhusu waandamanaji hao kukiteketeza huku wengine wakidai ni njama ya kuficha ushahidi muhimu wa DNA
Inadaiwa walizuiliwa kwa muda katika kituo cha polisi wa utawala cha Syokimau.

Miili yao ilipatikana katika mto wa Ol Donyo Sabuk, jimbo la Machakos, mashariki mwa jiji la Nairobi, ikiwa imefungwa mkono na ikionekana kuwa na ishara za majeraha.

Baadhi ya mashirika ya kutetea haki za kibinadamu wanataka mkuu wa Polisi Joseph Boinnet na waziri wa usalama Joseph Nkaissery wajiuzulu.

Kwa mujibu wa shirika lisilo la kiserikali linalofuatilia visa vya ukatili wa polisi dhidi ya raia Kenya la IMLU, mwaka 2015 watu 125 waliuawa kiholela na maafisa wa polisi.
Wanaharakati wa haki za kibinadamu na chama cha wanasheria Kenya LSK walipanga maandamano hayo kufuatia mauaji ya kutisha ya wakili mteja wake na dereva wao



Maafisa wanne wanaoshukiwa kutekeleza unyama huo Fredrick Leliman, Stephen Chebulet, Silvia Wanjiku na Leornard Maina wamefikishwa mahakamani na kuwekwa rumande majuma mawili ilikufanikisha uchunguzi.

Uchunguzi wa maiti yao umebaini kuwa walipigwa kikatili na silaha butu kichwani kabla ya kunyongwa.

Post a Comment

 
Top