0
Habari mpendwa rafiki na msomaji wa Amka Mtanzania? Natumaini unaendelea vema na shughuli za ujenzi wa taifa. Karibu katika makala yetu ya leo ambapo tutazungumzia adhabu zisizostahili katika malezi ya wato

Waswahili wanasema kuzaa sio kazi, bali kazi kulea mwana. Kazi kubwa kwa mtoto iko katika malezi kama ukishindwa kumlea mtoto katika maadili au njia inayofaa basi utakua umemharibu wewe mwenyewe. Mwanasaikolojia Erikison alikuja na nadharia moja ya ukuaji na maendeleo ya mtoto iitwayo trust vs mistrust akiwa na maana ya kwamba nadharia ya kuamini dhidi ya kutoamini. Nadharia hii huwa inatendeka kwa mtoto pindi akiwa na umri wa mwaka mmoja yaani mtoto anapozaliwa katika kipindi cha mwaka mmoja ni kipindi kumjengea kama duniani ni sehemu salama na penye matumaini ya kuishi au la. Kama mtoto akijengewa malezi mazuri na kupokea malezi mazuri yenye uthabiti, yanayotabirika na yanayopatikana atajijengea na kukua na sensi ya uaminifu na kuanzisha mahusiano mazuri na watu wengine na kujihisi kuwa duniani ni sehemu salama na ulinzi dhidi yake. 


Kwa mfano, kama mtoto amelelewa katika mazingira yenye ukatili angali akiwa mdogo mtoto atakua katika sensi au hisia za kutoamini (mistrust) na kujiengea nidhamu ya woga, kutojiamini hapa duniani na atajihisi duniani siyo sehemu sahihi na salama kuishi. Kwa hiyo, mtoto atakua katika woga na kukosa tumaini la maisha na hisia za wasiwasi zitamtawala. Watoto wanaolelewa katika maadili mazuri na hisia za upendo, furaha na amani atakua katika ukuaji mzuri wa akili na kimwili atakua na afya njema. Watoto wanaolelewa kikatili na wazazi wao huwa wanakosa upendo katika maisha yao na wako radhi kujitoa mhanga na kujiingiza katika tabia zisizofaa kama vile kujiingiza katika utumiaji wa madawa ya kulevya na hata vitendo vya ujambazi.
Hivyo basi, leo tutajifunza adhabu ambazo wazazi wengine huzitumia katika malezi ya watoto ambazo siyo rafiki na kustahili kwa mtoto. Zifuatazo ni adhabu zisizostahili na siyo rafiki katika malezi ya watoto.

1. Kumchunia Au Kumnunia Mtoto;
Mzazi kumnunia mtoto wako ni kumnyima haki ya kimsingi ya yeye kujielezea kama kuna kitu kibaya kinamsibu. Kama ukimchunia mtoto wako kwa kutoongea naye utakua unamsababishia mtoto kujiuliza maswali mengi ya kwa nini yasiyokuwa na majibu hatimaye kumwathiri kisaikolojia. Mtoto akikukosea hutakiwi kumchunia bali ongea naye na mwelekeze njia sahihi kwani wewe ndiyo mwalimu wa kwanza katika malezi ya mtoto. Unapomnyamazia mtoto unataka aende kwa nani akamuelezee matatizo yake? Kwa hiyo, kama mzazi tafuta mbinu nyingine ya kumwadhibu mtoto badala ya kumpatia adhabu mbadala kama hii ya kumnunia au kumchunia mtoto kwani jinsi unavyomchunia mtoto ndivyo unavyozidi kumwathiri mtoto wako na kumharibu mwenyewe.

2. Kumfungia Mtoto Ndani;
Mzazi anaona adhabu ya kumfungia mtoto chumbani ni njia nzuri ya kumwadhibu mtoto. Unapomfungia mtoto ndani kwa bahati mbaya akipatwa na dharura huko chumbani wakati wewe haupo utakuja kumlaumu nani? Ni jinsi gani mzazi unakosa utu kabisa na kumnyima mtoto haki yake ya kimsingi ya kucheza na kufurahia maisha. Kama ulikuwa na tabia hii acha mara moja kumfungia mtoto chumbani. Mtoto anahisi dunia ni sehemu hatari na siyo salama kuishi unamtengenezea hofu, woga na hali ya kutojiamini pale mtoto anapoharibikiwa utaanza kutumia gharama nyingi za kujitakia. Hivyo, epuka adhabu hii mbadala ya kumwadhibu mtoto.

3. Kumfokea Mtoto;
Kumfokea mtoto ni fedheha, hakuna mtoto anayefurahia kufokewa mbele ya watu. Mtoto atajihisi ni mtu wa kudharauliwa ambaye hastahili kuambiwa kwa upendo pale anapokua amekosea. Mtoto akifanya kosa mkanye na muelekeze kwa utaratibu ndio njia sahihi lakini siyo kumfokea kwa kupayuka payuka hovyo. Wewe ni mzazi na mwalimu wa kwanza katika malezi ya mtoto wako unapomfundisha vema naye atakwenda kuwafundisha vema kizazi chake na hatimaye kuwa na misingi mizuri katika familia itakayokwenda kujenga jamii bora.

4. Kumzomea Mtoto;
Kama wewe ni mzazi, mwalimu acha adhabu hii mbadala katika malezi ya mtoto. Mtoto anapokosa mzazi anamzomea mtoto badala ya kumfundisha. Usimfanyie mtoto kile ambacho wewe hukufanyiwa wakati ukiwa mtoto. Mfano kuna baadhi ya watoto huwa wanajikojolea kitandani sasa mzazi anachukua hatua ya kuwaambiwa watoto wenzake wamzomee mtoto mwenzao kwakua amejikojolea yaani hapa kama mzazi unakuwa unaongeza tatizo juu ya tatizo. Hata mashuleni baadhi ya walimu huwapatia wanafunzi wao adhabu hii ya kuzomea pale mwanafunzi anapofanya kosa au anapofanya vibaya katika maendeleo yake ya kitaaluma. Mwalimu anayewaambiwa wanafunzi wamzomee mwanafunzi mwenzao anakuwa anamharibu mwanafunzi badala ya kumrekebisha vizuri.

KITABU; JINSI YA KUFAIDIKA NA MABADILIKO YANAYOTOKEA KWENYE MAISHA.

5. Kumtukana Mtoto;
Kumlea mtoto katika hali ya kumtukana kila siku anapofanya kosa ni kuwaathiri kisaikolojia. Mtoto akifanya kosa tu utasikia mzazi akimtukana wewe mbwa, paka, mpuuzi, mshenzi, huna akili, kichwa kama mama, baba yako, fala wewe, na matusi mengine mengi ambayo hayastahili kumtukana mtoto hadharani. Mtoto hapaswi kuelekezwa kwa matusi bali mtoto anatakiwa kuelekezwa kwa lugha nzuri ya upendo na utaratibu mzuri. Hii siyo adhabu kwa mtoto bali ni kumuongezea matatizo na mizigo mikubwa akilini mwake. Ukiwa na hasira na mtoto amekukosea tulia kwanza na pumua hasira ziishe kwani matokeo ya hasira ni mabaya pale unapotenda ukiwa na hasira.

6. Kumfinya Mtoto Na Vitu;
Watoto wanapata malezi ya mateso sana kujiona hawastahili kuishi hapa duniani. Wazazi wanamfinya mtoto na vitu kama vile kisu hatimaye kusababishia majeraha makali sehemu zake za mwili. Huu ni ukatili mbaya sana kwa mtoto kuwa balozi mzuri wa kukemea na kuwafundisha watu juu ya hili. Tafuta njia nzuri ya kumkanya mtoto anapofanya kosa na siyo kumpa adhabu za kikatili.

7. Kumchoma Mtoto na Vitu Vyenye Moto;
Wazazi wengine wanaweka kisu jikoni kikipata moto mkali wanamchomea mtoto sehemu zake za mwili. Ukiwaona baadhi ya watoto miili yao imejaa vidonda na majeraha mbalimbali. Watoto wanakosa raha katika maisha yao hawafurahii uwepo wao hapa duniani. Kwa hiyo, wazazi na walezi kiujumla hamtakiwi kuwachukulia adhabu hii watoto wanapokosa badala yake tumia njia ambayo haina madhara ya kumkanya mtoto anapokosa.

Mwisho, watoto walelewe katika malezi bora. Familia ndio msingi wa jamii bora hivyo wazazi ni muhimu kuwa na familia bora ili kujenga jamii bora. Nakuacha na kauli mbiu ya malezi ambayo ni mtoto ni malezi, kuwa balozi mzuri katika jamii uliyopo dhidi ya adhabu hizi kali wanazopatiwa watoto kwa kuwaelimisha pale unapoona wanazitumia.
Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com au unaweza kutembelea tovuti yake www.actualizeyourdream.blogspot.com



Post a Comment

 
Top