Rais John Magufuli akihutubia Baraza la Idd el Fitr lililofanyika katika viwanja vya Karimjee Dar es Salaam jana. |
Pia amesema endapo Waislamu nchini watadumisha mafundisho waliyoyapata katika mwezi Mtukufu wa Ramadhan, upo uwezekano mkubwa kwa Taifa kuondokana na vitendo vya rushwa, ufisadi, ujambazi na hatimaye
kudumisha amani na utulivu.
Aidha, amesema endapo Watanzania wataongeza bidii katika kufanya kazi, kilio cha ukosefu wa fedha kilichoanza kusikika mitaani hivi sasa, kitatoweka. Aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akihutubia katika Baraza la Idd el Fitr lililofanyika katika viwanja vya Karimjee na kuwajumuisha viongozi mbalimbali akiwemo, Mufti wa Tanzania, Shehe Mkuu Aboubakar Zuberi Ally.
Wengine waliohudhuria Baraza hilo ni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Shehe Suleiman Lolila, Shehe wa Mkoa wa Dar es Salam Alhad Mussa Salum, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, mabalozi na wabunge.
Ufunguzi wa Baraza la Idd, ulitanguliwa na usomaji wa kiwango cha juu wa Kurani Tukufu uliofanywa na Ustaadh Simau Mussa ambaye ataiwakilisha Tanzania katika mashindano ya kusoma Kurani nchini Urusi hivi karibuni na tafsiri yake ilifanywa na Shehe Masoud Jongo.
Kuhusu umuhimu wa kufanya kazi kwa bidii ili kujipatia kipato, Rais Magufuli aliwaomba viongozi wa waislamu nchini kuwahamasisha wananchi kujenga utamaduni wa kufanya kazi kwa bidii ili kuweza kujipatia kipato.
“Waliokuwa wamezoea fedha za bure bure wameanza kulalamika kwamba fedha zimepotea mitaani. Fedha haziji bila kufanya kazi, Tanzania ni yetu sote, kila mtu ana wajibu wa kufanya kazi, fedha zitajaa mitaani kama tutaongeza jitihada katika kufanya kazi,” alisema.
Kuhusu umoja na mshikamano, Rais Magufuli pamoja na mambo mengine alisisitiza kuwa kama alivyoahidi wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka jana, wakati akizindua Bunge na katika mikutano mbalimbali, atahakikisha anakuwa Rais wa Watanzania wote bila kujali tofauti zao za kidini, kisiasa, rangi na jinsia.
“Nimefurahishwa sana na kitendo chako Mufti cha kuwakaribisha waumini wa madhehebu mbalimbali katika Baraza hili la Idd. Bakwata ya leo ni tofauti sana na Bakwata ya huko nyuma na napenda kukuahidi kuwa chini ya Awamu ya Tano ya Serikali, nitawaunga mkono kwa nguvu zangu zote,” alisema.
Aidha Rais Magufuli alisema wakati wa kampeni aliahidi kuwa angefanya kazi ya kuongoza Taifa kwa manufaa ya Watanzania wote; na alitumia Baraza hilo la Idd kumuomba Mungu, aweze kumsaidia katika kufikia azma yake hiyo.
Kuhusu mfungo wa mwezi wa Ramadhan, Rais Magufuli pamoja na kuwapongeza Waislamu waliofanikiwa kufunga, pia aliwataka kuendelea kufanya matendo ya kumpendeza Mungu na kuongeza kuwa endapo dini nyingine zitaungana na waislamu katika hilo, nchi itaondokana na changamoto mbalimbali.
“Kama waislamu nchini kote wataendeleza matendo mema ya kumpendeza Mungu, hatua hiyo itasaidia kuondoa changamoto nyingi zinazolikabili Taifa letu kama rushwa, ufisadi, dhuluma na ujambazi,” alisema.
Akizungumzia suala la amani, Rais alisema suala la amani ni muhimu na aliwataka waislamu nchini kote, kushirikiana na madhehebu mengine katika kuitunza amani kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.
“Napenda nisisitize kuwa serikali itahakikisha inasimamia kwa nguvu zake zote suala la amani na napenda kuzipongeza taasisi za dini ambazo zimekuwa zinafanya kazi kubwa katika kutekeleza majukumu ya kuhamasisha amani ya nchi yetu,” alisema.
Aidha Rais alisema kwa kutambua kuwa Bakwata, imekuwa inatekeleza majukumu ya kuisaidia serikali katika kutekeleza miradi ya kijamii kama afya na elimu, serikali itatoa ushirikiano na misaada ya hali na mali ili kuhakikisha kuwa malengo ya Bakwata katika utekelezaji wa miradi yake yanafikiwa bila kikwazo chochote.
Katika hatua nyingine, Rais alionya vitendo vya baadhi ya wenye mali kuingia ubia na taasisi za dini ili kutekeleza miradi mbalimbali lakini bila kuzingatia makubaliano na kusababisha mali za taasisi za dini kupotea na alisema serikali itashirikiana na taasisi hizo ili kurejesha mali zilizopotea kwa ulaghai.
“Napenda nitoe ushauri kwa Bakwata na madhehebu mengine ya dini ili vitendo hivi vikomeshwe haraka maana wahusika wanaoingia mikataba kama hii wapo miongoni mwetu. Viongozi hawa wamekuwa wanaingia mikataba ya utapeli na mali za taasisi za dini kupotea. Nakuamini Mufti, nawaamini viongozi wa dini, basi msaidiane na serikali katika kusimamia mali zilizo chini yenu.
“Napenda kuona mali za Waislamu au taasisi zingine za dini zisiwe chanzo cha migogoro na kuvunjika kwa amani. Tunapenda wawekezaji lakini utapeli kwenye mali za madhehebu hatutakubali maana wakati mwingine wanachoahidi hawatekelezi, na kufanya hivyo ni kumkosea Mungu. “Napenda kuahidi kuwa tutashirikiana na viongozi wa waislamu na dini nyingine ili tuweze kukomboa mali zao pale itakapohitajika kwa kuzingatia sheria, haikubaliki na kamwe haitakubalika kwa watu wenye mali na uwezo kutumia fursa hiyo kudhulumu mali za taasisi za dini,” alisema Rais Magufuli.
Rais alisema pia kuwa Serikali ya Awamu ya Tano tangu ilipoingia madarakani, imekuwa ikitekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ya utoaji wa elimu bure, kujenga nidhamu ya utumishi serikalini na kudhibiti mapao.
Alisema kazi nyingine ni kupambana na rushwa na ufisadi, na kuboresha huduma za jamii na kwamba kama Taifa, Tanzania inao uwezo mkubwa wa kujitegemea kutokana kuwa na rasilimali nyingi na kwamba maombi yanayotolewa na wananchi yanatoa hamasa kwa viongozi katika kuwatumikia.
“Bado tuna uwezo wa kuitengeneza Tanzania mpya. Maombi yenu ni muhimu kwani yanaendelea kutupa hamasa, msichoke kutuombea tumeamua kufanya kazi na kwa maombi yenu tutafika. Lengo ni kuifikisha Tanzania pazuri na wala hatuna lengo la kumuonea mtu yeyote.
“Tanzania ni nchi tajiri, juzi juzi tu hapa imegundulika gesi ya Helium, tena tani za kutosha, lakini pia kila madini yapo Tanzania ni kwa nini sasa tuwe masikini? Ndio maana tumeamua sisi wengine kwa niaba yenu turudishe heshima ya nchi hii na katika kufanya hivyo wapo watu watakaoguswa, ndio maana ninawaomba waislamu na madhehebu mengine tushirikiane ili tuipeleke nchi yetu mbele,” alisema Rais.
Rais Magufuli pia alimpongeza Mufti wa Tanzania, Shehe Zubeir kwa juhudi zake za kuwaunganisha waislamu wote na kupanua uwigo wa Bakwata kutoa huduma za kijamii na ameahidi kuwa serikali ya awamu ya tano itaunga mkono juhudi hizo.
Magufuli alisema kitendo cha kuwaunganisha waislamu wote katika Baraza la Idd el Fitr, kinafungua ukurasa mpya na ni moja ya hatua muhimu za kuimarisha amani, umoja na mshikamano miongoni mwa Waislamu wa makundi mbalimbali pamoja na watanzania wengine waisio Waislamu.
Aidha, Rais Magufuli alizungumzia juhudi zinazofanywa na Bakwata katika kuimarisha taasisi zake zinazotoa huduma za kijamii na kulinda mali zake, akisema serikali itahakikisha mali zote za waislamu zinakuwa salama na kwamba wote waliodhulumu mali za waislamu watazirejesha.
Kwa upande wake, Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakary Zubeir alisema Waislamu nchini wanaunga mkono kwa dhati jitihada zinazofanywa na serikali katika kujenga umoja na mshikamano, mapambano dhidi ya rushwa, ufisadi, ndoa za jinsia moja na ugaidi.
Mufti Zubeir alisema katika siku za hivi karibuni kumekuwepo na viashiria vya uvunjifu wa amani nchini kutokana na kuibuka kwa vitendo mbalimbali vya uvunjifu wa amani vinavyoegemea katika mwavuli wa dini.
“Sisi kama jumuiya ya Waislamu tunachotaka ni umoja na mshikamano bila kujali itikadi zetu za kidini ili kuifanya Tanzania kuwa sehemu salama,” alisema Mufti.
Mufti alimshukuru Rais Magufuli kwa kuongoza bila ubaguzi na aliwataka Watanzania kuunga mkono juhudi za serikali kupinga matendo maovu, ikiwemo rushwa na ufisadi na pia alilaani ndoa za jinsia moja, akisema ni kinyume na maadili ya dini.
Awali akisoma taarifa, Katibu Mkuu wa Bakwata, Alhaji Suleiman Lolila alisema Bakwata inatarajia kupanua huduma za kijamii kwa lengo la kuwahudumia wananchi, ikiwemo kujenga Chuo Kikuu mkoani Dodoma.
Pia, alimpongeza Rais Magufuli kwa juhudi zake za kuondoa umasikini huku akimtaka asikatishwe tamaa na wachache watakaoudhika kwa kuguswa na hatua zinazochukuliwa.
Post a Comment