0
Ili mtu aweze kufanikiwa katika maisha yake, anahitaji kuwa na vitu vingine zaidi ya juhudi ya kutenda kama kutokukata tamaa. Najua mambo mengi sana yanatajwa linapokuja suala la kutafuta mafanikio ikiwemo hata na bahati. Lakini, pamoja na mambo yote hayo huwezi kuacha kuhusisha kutokukata tamaa hasa pale unapotafuta mafanikio.
Tambua upo uhusiano mkubwa sana kati ya mafanikio na kuwa king’ang’anizi wa ndoto  zako. Hiyo ikiwa na maana kuwa, huwezi kufanikiwa kwa chochote katika hii dunia kama wewe ni mtu wa kukata tamaa mapema. Ili uweze kufanikiwa unatakiwa kujijengea tabia ya ung’ang’anizi hata itokee mambo yako yamekwama vipi.
Hebu jaribu kuangalia kidogo maisha ya watu waliofanikiwa yakoje? Bila shaka utagundua ni watu wasiochoka kutafuta mafanikio hata pale wanapokutana na changamoto. Kwa lugha rahisi ni watu wasiokata tamaa mapema. Pamoja na kukutana na changamoto nyingi katika maisha au  biashara, ikiwemo hata na kufilisika kabisa, lakini wao huamua kuwa ving’ang’anizi hadi kufanikiwa.
Kitu cha kujiuliza ni kitu gani ambacho huwafanya watu hawa kuwa ving’ang’anizi na kujiku
ta hawakati tamaa mapema? Ni siri au jeuri gani ambayo watu hawa huitumia kuwaongoza hadi kuwa ving’ang’anizi wa mafanikio? Je, watu hawa wana uwezo wa ziada au sifa zinazowafanya wawe ni watu wa kutokukata tamaa?
Majibu yote ya maswali hayo yamo ndani ya makala haya, yakiwa yamendikwa kwa ufasaha mkubwa. Kwa kutenga muda mchache kupitia makala haya, utajifunza sifa za watu wasiokata tamaa katika maisha. Kwa kuwa na sifa hizi, huwasaidia sana kufanikiwa. Naamini una hamu ya kutaka kujua sifa za watu wasiokata tamaa, kama kiu yako ndiyo hiyo karibu na twende pamoja kujifunza.

1. Wanaziona changamoto kama hatua.
Wakati wengine wanaona changamoto kama ndio mwisho wa mafanikio, lakini watu wasiokata tamaa huziona changamoto hizo kama njia au hatua mpya ya kuelekea kwenye mafanikio. Pale wanapokuwa wanakutana na changamoto huweza kukaa chini na kutafuta majibu ya changamoto hizo na sio kulalamika hovyo.
Tuchukulie kwa mfano biashara zao zinaposhindwa, hukaa chini na kujiuliza nini hasa tatizo, wapi wanapokosea na kujikuta wamepata majibu ya yale yaliyo ya msingi kuwasaidia kusonga mbele. Kwa kupata majibu hayo changamoto hiyo inakuwa imewasaidia kuwa kama ngazi au hatua ya kuelekea kwenye mafanikio. Hii ni sifa muhimu sana unayotakiwa kuijua na kuifanyia kazi.

Kuwa mtu wa kujifunza na kusonga mbele.

2. Hawakatishwi tamaa na neno “HAPANA”.
Watu wasiokata tamaa mara nyingi hawakatishwi tamaa na maneno ya wengine. Ni watu wa kujiamini na kusikiliza kile kilichondani yao na sio nje yao. Haijalishi watu wengine huwa wanasema au wanaongelea nini juu yao, wanachokijua wao ni kufuata ndoto zao na kuzifanikisha. Ni watu ambao kama wameziba masikio kutokusikiliza kelele za nje ambazo hazina msaada kwao.
Halikadhalika, hata wewe ukitaka kufanikiwa hii ni sifa muhimu sana unayotakiwa kuwa nayo. Ikiwa kuna mtu atakukatalia au kukwambia huwezi kwa kile unachokifanya, tumia kukataliwa huko kama nguvu ya kukusogeza mbele. Usikubali “HAPANA” yoyote ikuzuie kufanikiwa. Haijalishi “HAPANA” hiyo imetoka wapi, kwa bosi wako au getini unapoenda kuomba kazi.

3. Hawajui kushindwa.
Sifa kubwa nyingine kubwa ya watu wasiokata tamaa, vichwani mwao hawana msamiati wa neno kushindwa. Wao wanakuwa wanatafuta mafanikio kwa kujua kwamba ni lazima wafanikiwe. Hata hivyo kwa kuwa hawajui kushindwa, hiyo haimaanishi maisha yao sikuzote huwa yamewanyookea, hapana.
Inapotokea wameshindwa kwa jambo lolote hupuuza kushindwa huko na kutumia kama funzo la kuwasidia kuendelea na si kukata tamaa. Hufanya hivi kwa sababu wanajua hakuna katika hii dunia ambaye amewahi kufanikiwa bila kushindwa. Hivyo, falsafa yao kubwa ni kuchapa kazi na kufanikiwa, ikitokea kushindwa hiyo ni ‘ajali’ tu.


4. Ni watu wa kujifunza kila siku.
Pia watu wasiokata tamaa mara nyingi sio wajuaji. Ni watu wakutaka kujifunza kila siku. Pale wanapokuwa wamekosea hukubali makosa hayo na kuamua kuyatumia kama njia mojawapo nzuri ya kuweza kuwasaidia kusonga mbele. Kitu hiki huwasaidia wao kuweza kujifunza kutoka kwa wengine wanaopitia magumu pengine zaidi yao na kuwapa nguvu ya kutokata tamaa mapema.
Kumbuka, hizo ndizo sifa za watu wasiokata tamaa kwenye maisha. Kwa kuzifanyia kazi sifa hizo zitakusaidia hata wewe kuweza kufikia mafanikio makubwa katika maisha yako.
Tunakutakia kila la kheri na endelea kujifunza kupitia mtandao wako wa DAKIKA ZA MADINI kila siku.

Post a Comment

 
Top