Habari rafiki na mpenzi msomaji wa Dakika Za Madini? Natumaini unaendelea vizuri na shughuli zako za kimaendeleo. Karibu tena katika safu hii, leo tutajifunza kuhusu lugha tano muhimu katika mahusiano yetu. Kama tunavyojua siku zote Upendo huanzia nyumbani. Upendo mlionao wakati wa uchumba ndio huohuo mnatakiwa kuuendeleza baada ya ndoa na kupata watoto.
Pia kuna watoto wanaokuzwa kwa upendo, wanaohitajiwa na wanaothaminiwa. Pia kuna watoto wanaokuzwa kwa kutokupendwa, kutokuhitajiwa na kutokuthaminiwa. Watoto wanaopendwa na w
azazi wao na jumuiya zao watakuwa na hisia za upendo kutegemea saikolojia zao na upendo waliooneshwa na wazazi wao. Watoto ambao hawajakuzwa kwa upendo hawawezi kuwa na upendo kutegemea na saikolojia zao za kukosa upendo toka kwa wazazi wao na jamii inayowazunguka. Wazungu wanasema ‘’Love makes the world go round’’ (Mapenzi yanaifanya dunia izunguke). Kwa hiyo hatuna budi kuishi kwa upendo ili kuwa na maisha yenye furaha na amani. Zifuatazo ni lugha tano za upendo ;
1. Maneno Yenye Kufariji Na Kutia Hamasa (Words of affirmation/ Verbal Compliments). Unapoongea na mpenzi wa moyo wako mpe maneno yenye kufariji ili umpe furaha. Jaribu kuongea naye kwa upole, maana utamfanya ajisikie raha na kupendwa. Usipende kumkaripia. Pale mpenzi wako anapofanya vizuri mpongeze mfano kama amevaa nguo amependeza jaribu kumsifia kwani unaongeza upendo na kujiamini kwake. Pia akiwaletea zawadi nyumbani mpe maneno mazuri mwambie hata asante kwa zawadi nzuri na usianze tu kuzikosoa hata kama hujazipenda. Usihesabu mabaya maana upendo hauhesabu yaliyo mabaya (Love doesn’t keep a score of wrongs). Pia upendo hauhesabu makosa ya zamani, hakuna mtu miongoni mwetu ambae ni mkamilifu. Upendo unaombwa na sio kulazimisha na kutoa amri. Ukilazimisha na kumuamrisha mpenzi wako unakuwa mzazi na yeye unamgeuza kuwa mtoto.
Kama tunataka kujenga uhusiano ulio bora lazima tujue kila mtu anapendelea nini. Kama tunataka kupendana lazima tujue nini mwenzako anataka. Kitu ambacho tunaweza kufanya na matatizo yaliyokwisha kutokea ni kuyaacha yawe historia, ndio yalitokea, inauma lakini mpenzi wako amekubali kosa na kukuomba msamaha wako. Kwa hiyo msamaha sio mpaka ujisikie bali ni kujizatiti au kujitoa (forgiveness is not a feeling, it is a commitment). Msamaha ni matendo ya huruma na sio kushikilia kosa la yule aliyekosea. Msamaha unaonesha upendo. Mwanasaikolojia William James alisema kwamba ‘‘Hitaji kubwa la binadamu ni kujisikia anathaminiwa’’ kwa hiyo maneno yenye kufariji na kutia moyo ndio yanaweza kujaza upendo kwa watu wengi katika mahusiano yetu.
2. Kuwa na Muda mzuri (Quality Time). Unatakiwa uwe na muda mzuri na mpenzi wako, tenga muda wa kukaa na mpenzi wako, msikilize anasema nini na anapenda nini. Sio unakaa na mpenzi wako mnaangalia televisheni halafu unajisemea umempa muda mpenzi wako. Unapokuwa umekaa na mpenzi wako hutakiwi ufanye kitu kingine zaidi ya kuwa naye, hakikisha unamwangalia machoni mpenzi wako wakati anaongea. Usimsikilize mpenzi wako huku unafanya kitu kingine kwa wakati huohuo, sikiliza kwa hisia, pia jaribu kuangalia lugha za mwili ili uweze kuelewa kile mpenzi wako anakueleza mfano kukonyeza, kukuminya mguu au hata kufumba macho. Vilevile Usipende kuingilia wakati mpenzi wako anaongea, mwache aongee mpaka amalize ndipo na wewe uongee. Unapaswa kujaza tanki la mapenzi kwa mwenzako kulingana na hisia zake pamoja na mawazo kulingana na muda.
Pia mnapaswa kufanya shughuli mbalimbali pamoja mfano, kusikiliza mziki, chukueni muda wa kucheza, kuongea kufanya mazoezi ya mwili kusoma vitabu na kushirikishana yale mliojifunza, kaeni muongee kama vile mnatongozana, kuleni pamoja, ulizaneni maswali ya hapo zamani mfano wakati unasoma elimu ya msingi ulikuwa unapendelea somo gani? Kwa kufanya hivyo, utakuwa umejaza tanki la upendo kwa mwenza wako ambaye anajisikia kupendwa pale unapompa muda.
3. Kupokea Zawadi (Receiving Gifts). Kuna wapenzi wengine wanajisikia upendo pale wanapoletewa zawadi na wenza wao. Kwa mfano, pete ni kitu kinachoonekana na ni ishara ya upendo na muunganiko wa nafsi mbili katika upendo ambao hauna ukomo. Zawadi ni alama zinazoonesha upendo. Mpe mpenzi wako zawadi na kama akikuuliza mjibu ‘najaribu kujaza tanki lako la upendo, unapompa mpenzi wako zawadi anajisikia upendo na sio lazima umnunulie vitu vya bei kubwa. Unaweza hata ukachuma ua la rose na kumpa mpenzi wako wakati unatoka kazini kwako, huwezi jua kiasi gani utakuwa umemfurahisha ila ni yeye mwenyewe ndio ataona kiasi gani umeonesha kumjali na kumthamini. Unaweza ukamtengenezea mpenzi wako kadi kwa kutumia mkasi na karatasi, kata karatasi hilo hata umbo la mduara au kopa na andika maneno I loveYou.
Kwa kufanya hivyo utakuwa umefanya jambo la maana na la msingi sana. Utazidi kumfanya mpenzi wako ajisikie raha na kuona hakuna kama yeye katika dunia hii. Kuonesha upendo kwa njia ya zawadi sio lazima uwe na fedha nyingi ili uweze kununua zawadi kubwa kubwa kama gari au nguo bali unaweza hata kununua pipi ya shilingi mia moja au chokoleti kama mpenzi wako anapenda vitu hivyo. Usikae chini usubiri mpaka upate hela ili labda umnunulie mpenzi wako zawadi ya nguo, anza sasa kwa vitu vidogo vidogo visivyohitaji pesa nyingi. Pia kuna watoto wengine wanapenda sana zawadi hivyo basi unapotoka kazini usiache kumletea mwanao zawadi mfano, ua, box la kuchezea, jani au kitu chochote ili ajisikie kupendwa na wewe mzazi ujaze tenki la upendo kwa mwanao.
4. Kusaidiana Katika Mambo Mbalimbali (Acts of Service). Kama wapenzi mnatakiwa kusaidiana kufanya shughuli mbalimbali. Saidianeni kwa upendo (Serve one another in love), Kama wapenzi mnatakiwa kusaidiana kufanya mambo mbalimbali mfano mama akiwa jikoni anapika baba anaweza akatoka nje na kukata majani yaliyopo kwenye uwanja wenu wa nyumba. Au mama akiwa anafua nguo za watoto baba anaweza kukaa na mtoto au watoto na hata kuwabadilisha nepi au pampasi. Kwa kufanya hivyo upendo unazidi kuimarika na tenki la upendo la mwenza wako ambae anapenda kusaidiwa kazi litakuwa limejaa na hata kuweza kufurika (full tank and overflowing).
5. Kuguswa Kimwili (Physical Touch). Risechi nyingi zimehitimisha kuwa watoto wanaokumbatiwa, kupakatwa na kubusiwa wanakuwa na afya nzuri ya kihisia kuliko wale ambao wanaachwa kwa muda mrefu bila kuwa na mguso wa kimwili. Kujamiiana ndio lahaja pekee katika mapenzi. Kama mume wako anapenda kukutana kimwili usimkatalie mpe ili ujaze tanki lake la upendo mpaka lifurike. Mume anaweza akawa hapendi kula vyakula mbalimbali na kitu chake kikubwa anachopenda ni tendo la ndoa hivyo basi wewe kama mke usihangaike kupika vyakula vya kila aina ukafikiri mume wako ndio atajisikia kupendwa. Kama lugha ya upendo ni kuguswa kimwili basi jitahidi kumpa mume wako muda mwingi huko kulikoni kitu kingine na vivyo hivyo na atendewe mke. Sio mke anataka mguso wa kimwili na mume wake halafu mume yuko bize na kompyuta au simu. Kufanya hivyo utakuwa umemuumiza mwenza wako na utamfanya ajisikie kukosa upendo.
Mguso wa kimwili unaweza kujenga au kubomoa uhusiano. Kugusa mwili wa mpenzi wako ni kumgusa yeye na kutomgusa mwili mpenzi wako ni kujiweka naye mbali kihisia. Hivyo basi ili mahusiano yadumu mguso wa mwili ndio kitu kikubwa na chenye umuhimu hivyo wanandoa au wapenzi hawana budi kugusana miili yao ili kuimarisha upendo. Kama unaweza kumkumbatia au kumbusu mpenzi wako mfanyie wala hauhitaji ruhusa wala mtaji katika hili.
Kwa kuhitimisha, upendo ni chaguo na upendo hauchagui, wapende hata maadui zako na wale wasiopendwa. Unapaswa ujue lugha yako ya upendo na hata ile ya mwenza wako ili muweze kujaza matenki yenu ya upendo mpaka yamwagikie na kufurika (overflowing love) na pia muweze kuishi kwa upendo ulio mkuu. Kama bado hujajua lugha ya upendo ya mpenzi wako mfano kupokea zawadi, kuguswa kimwili au hata kuwa na muda mzuri na mpenzi wako anza sasa kuijua ili uweze kumtimizia vile vitu anavyopenda na usije ukawa unapoteza muda kwenye kitu ambacho hakipendi. Hivyo ni muhimu kujua lugha ya upendo ya mwenzako ili kila mmoja awe na uelewa unaoshabihiana yaani mutual understanding
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post a Comment